Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-20 15:19:47    
Mafanikio ya mwanzo yamepatikana katika juhudi za kupambana na ukiukaji wa hakimiliki ya mtandao wa internet

cri

Ofisa wa Idara Kuu ya Hakimiliki ya China tarehe 15 kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema mapambano dhidi ya ukiukaji hakimiliki ya mtandao wa internet yaliyoanzishwa mwaka jana, yamepata mafanikio ya mwanzo. Alisema, China itaanzisha mfumo wa kudumu wa kuzuia ukiukaji wa hakimiliki ya mtandao wa internet nchini China.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Idara Kuu ya Hakimiliki ya China ilitangaza mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya ukiukaji wa hakimiliki. Tokea mwezi Septemba hadi Desemba mwaka jana, vyombo husika vya serikali vilianzisha mapambano dhidi ya ukiukaji wa hakimiliki ya kutangaza maandishi, audio na video kwenye mtandao wa internet bila idhidi ya wamiliki wa hakimiliki, na vyombo hivyo viligundua na kuadhibu baadhi ya matukio makubwa ya kutangaza filamu, muziki na software kwenye mtandao wa internet kwa lengo la kujipatia faida.

Naibu mkurugenzi wa Idara Kuu ya Hakimiliki ya China Bw. Yan Xiahong alieleza, "Hadi kufikia tarehe 31 Desemba mwaka jana, idara za hakimiliki za sehemu mbalimbali nchini China kwa kushirikiana na polisi, ziligundua na kuadhibu matukio makubwa 172 ya kukiuka hakimiliki, baada ya kuwa na ushahidi bayana zilifunga tovuti 76 zilizoendeshwa bila leseni, na zilizitoza faini tovuti 29, na zilifikisha mahakamani kesi 18 zinazohusika na makosa ya jinai."

Kati ya matukio hayo, 14 yalishitakiwa na watu au jumuyia kutoka nchi za nje. Shirikisho la Filamu la Marekani lilishitaki tovuti ya On Line Every Day kwa kutangaza filamu za The Pacifier na Troy kwenye mtandao wake, Idara ya Hakimiliki ya Beijing ilisimamisha kitendo chake cha kukiuka hakimiliki na kuitoza faini tovuti hiyo.

Matukio ya kukiuka hakimiliki ya mtandao wa internet yaliyozuka ni donda ndugu lililotokea wakati tovuti za mtandao wa internet zinapoongezeka kwa kasi nchini China. Kutokana na takwimu, hivi sasa wanamtandao wa internet nchini China wamefikia milioni 110 na tovuti zimezidi laki 6.9, mtandao wa internet umehusika maisha ya watu wa China katika sehemu mbalimbali. Kwa sababu mtandao wa internet hauna mpaka wa nchi na una idadi kubwa ya habari na kuenea kwa kasi, ukiukaji wa hakimiliki ya mtandao wa internet umekuwa ukishamiri na umeathiri soko la audio, video na software nchini China, na hali hiyo imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya mashirika ya mtandao wa internet nchini China.

Mapambano dhidi ya ukiukaji wa hakimiliki ya mtandao wa internet yanasifiwa na watu nchini China na nchi za nje. Shirikisho la Filamu la Marekani na Shirikisho la Kimataifa la Santuri za Muziki yaliiandikia barua Idara Kuu ya Hakimiliki ya China ikisema mapambano hayo nchini China ni magumu lakini yamepata mafanikio kiasi. Mashirikisho hayo yalisema, yatashirikiana zaidi katika mapambano hayo.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari Bw. Yan Xiaohong alisema, ingawa mapambano hayo yamepata mafanikio kiasi, hata hivyo kutokana na kuwa suala hilo ni la dunia nzima, mpaka sasa hakuna hata nchi moja iliyotatua kabisa tatizo hilo. Kwa hiyo mapambano hayo nchini China yatakuwa magumu na ya muda mrefu. Bw. Yan Xiaohong alieleza, "Ingawa kipindi cha mapambano dhidi ya ukiukaji wa hakimiliki ya mtandao wa internet kimemalizika, lakini kazi yetu ya kupinga ukiukaji huo inaendelea. Kwa upande mmoja tunaendelea kushughulika na matukio ya ukiukaji huo na kwa upande mwingine tunaendelea kuwasiliana na kushirikiana na mashirika ya nchi za nje ili kupata mazingira bora kwa ajili ya hifadhi ya hakimiliki na kuwapatia watu urahisi wa kupata habari, elimu na burudani."

Ofisa huyo alidokeza kuwa mwaka huu China itatunga sheria ya hifadhi ya hakimiliki ya mtandao wa internet, ili kazi za kupinga ukiukaji huo itekelezwe kwa mujibu wa sheria.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-20