Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-21 14:45:08    
Sekta ya usafirishaji barua na vifurushi kwa haraka yapata maendeleo makubwa

cri

Kutokana na maendeleo ya uchumi na biashara ya nje ya China, sekta ya usafirishaji barua na vifurushi nayo imeimarika kwa haraka. Hivi sasa nchini China kuna kampuni za aina hiyo zaidi ya laki moja. Watu wa sekta hiyo wamesema, baada ya kampuni maarufu za usafirishaji barua na vifurushi kwa haraka za nchi za nje kuingia kwenye soko la China, kampuni za aina hiyo nchini hazina budi kuinua ubora wa huduma zao ili zipate maendeleo katika ushindani na kampuni hizo za kutoka nje.

Bw. Jin Xun ni mkurugenzi mkuu wa kampuni binafsi ya usafirishaji barua na vifurushi kwa haraka mjini Shanghai inajulikana kwa kampuni ya Meiya. Kabla ya miaka michache iliyopita kampuni yake ya nguo iliingia hasara ya dola za kimarekani laki 1 kutokana na makosa ya kampuni moja ya usafirishaji barua na vifurushi kwa haraka, kutokana na hali hiyo Bw. Jin Xun akaamua yeye mwenyewe aanzishe kampuni ya usafirishaji barua na vifurushi. Kampuni yake ni mpya, haina uwezo kushindana na kampuni kubwa maarufu za kimataifa za aina hiyo, licha ya hayo, kampuni nyingine kubwa na ndogo za aina hiyo za nchini pia zilianzishwa miaka mingi iliyopita, hivyo nafasi iliyobaki ni ndogo sana. Baada ya kutafakari, Bw. Jin Xun alifanya uamuzi, alitaka kampuni yake ishughulikie katika njia maalumu kati ya Marekani na China.

Baada ya kupita miaka kadhaa, uamuzi huo wa Bw. Jin Xun uliochukuliwa kuwa ni wa hatari na wenzao wa sekta hiyo, sasa unathibitishwa kuwa ni uamuzi sahihi. Kutokana na ongezeko la kasi la uchumi wa China na maendeleo ya biashara kati ya China na Marekani, huduma za usafirishaji barua na vifurushi kati ya China na Marekani zinapendwa na watu wengi.

Bw. Jin Xun alisema,

"Kwa mfano, wateja wetu walioko nchini Marekani wakitaka kusafirisha vitu hadi nchini China, sisi siyo kama kampuni nyingine za usafirishaji, ambazo zinachambua vitu vinavyosafirishwa hadi viwe vingi kiasi, kisha zinasafirisha vitu vile vinavyotakiwa kufikishwa China. Tunavyofanya sisi ni kuwa kila siku tunasafirisha vinavyotakiwa kupelekwa China mnamo saa 1 au 2 usiku, tunavikimbiza hadi uwanja wa ndege. Hivyo vitu tunavyosafirisha vinafika China kwa haraka zaidi kama kwa nusu siku au siku moja kuliko kampuni nyingine za usafirishaji. Huo ndio umaalumu wa njia maalumu kati ya China na Marekani, baada ya kupita muda, tuliona idadi ya wateja iliongezeka kwa haraka hata katika mwaka ule wa kwanza baada ya kampuni yetu kuanzishwa."

Katika miaka zaidi ya kumi iliyopita, karibu kila mwaka kulikuwa na wafanyabiashara kama Jin Xun waliojishughulisha na kazi hiyo ya usafirishaji wa barua na vifurushi. Takwimu zinaonesha kuwa mbali na kampuni za usafirishaji barua na vifurushi za taifa, hivi sasa nchini China kuna kampuni binafsi laki kadhaa, na idadi ya wafanyakazi wa kampuni hizo imefikia milioni kadhaa. Kwa upande mwingine kampuni 4 kubwa maarufu za kigeni za DHL, FEDEX, UPS na TNT ziliingia kwenye soko la China kwa nyakati tofauti, na hivi sasa zinaimarisha mifumo yao ya usafirishaji wa haraka.

Kitu kinachovutia kampuni kubwa za usafirishaji za nchini na nchi za nje kwenye soko la usafirishaji wa haraka, ni nafasi kubwa ya biashara ambayo bado haijatumika. Inakadiriwa kuwa hivi sasa ukubwa wa soko la usafirishaji wa haraka ni Yuan za Renminbi bilioni 20 kwa mwaka, lakini katika miaka kadhaa ijayo, soko la usafirishaji wa haraka wa vifurushi litakuwa na ongezeko la zaidi ya 25% kwa mwaka.

Kampuni kubwa za usafirishaji wa haraka duniani zilianza kuingia soko la China mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita. Kutokana na kanuni za kisheria za wakati ule kuhusu uwekezaji wa wafanyabiashara wa nchi za nje, kampuni za nchi za nje nchini China ilikuwa ni lazima zishirikiane na kampuni za China, tena China iwe na hisa nyingi zaidi, lakini baada ya mwezi Desemba mwaka 2005, kikwazo hicho kiliondolewa, kampuni yoyote ya kigeni ya usafirishaji wa barua na vifurushi kwa haraka iliruhusiwa kuwa na umiliki hisa wa peke yake, tena ziliruhusiwa kuendesha shughuli zao kwa mtindo wa nchi za nje. Kuondolewa kwa "sera za hifadhi" kulileta shinikizo kubwa kwa kampuni za usafirishaji za China.

Kiongozi wa shirika la jarida lijulikanalo kwa "Usafirishaji Bidhaa wa Kimataifa nchini China" Bw. Hu Chengsheng amesema, hivi sasa kampuni za usafirishaji wa barua na vifurushi za China zinatakiwa kushindana na kampuni za nje uso kwa uso, na kuondoa upungufu wa aina tatu.

"Kwanza, sekta hiyo inatakiwa kuwa na uzoefu wa kiwango fulani. Inatakiwa kuwa na mfumo wake, ni dhahiri kuwa ukubwa wa mfumo bado ni mdogo ukilinganishwa na kampuni za nchi za nje. Pili, upungufu katika maarifa na usimamizi wa shughuli za usafirishaji wa haraka. Tatu, kuna kampuni nyingi za usafirishaji wa haraka nchini, ambazo zinaendesha shughuli zao kiholela."

Tokea mwaka uliopita, kampuni za FEDEX, DHL na UPS zilibuni mipango ya uwekezaji na ujenzi wa mifumo yao katika eneo la China, zikitarajia kuchukua nafasi kubwa katika ushindani wa duru jipya. Watu wa sekta hiyo wanaona kuwa kwa kipindi kisicho kirefu shabaha muhimu ya huduma zao ni kampuni za kimataifa zilizoko nchini China, hivyo athari ya kampuni za usafirishaji wa haraka za China bado siyo kubwa. Lakini kwa kipindi kirefu, endapo kampuni za nchini hazitaweza kujiimarisha katika pande za wazo la huduma, mtindo wa huduma, kigezo cha huduma na eneo la huduma, basi zitakabiliwa na changamoto na shinikizo kubwa zaidi na zaidi. Hata hivyo, mratibu mkuu wa kamati ya usafirishaji wa haraka ya jumuiya ya wakala wa uchukuzi wa mizigo baharini ya China Bw. Liu Jianxin alisema, maendeleo ya sekta ya usafirishaji wa barua na vifurushi kwa haraka ya China hayatakuwa madogo kama yanavyokadiriwa hivi sasa, bado wana ubora katika ushindani.

Ubora wao mkubwa ni kwamba wao ni wenyeji, wanafahamu vizuri hali ya soko la China, wanafahamu zaidi mazoea, mawazo na uhusiano kati ya watu vya wachina. Jadi ya utamaduni huo unawawezesha kuwa rahisi zaidi kwao kukubaliwa na wateja wa China."

Habari zinasema, ingawa kampuni kubwa za usafirishaji wa haraka za kimataifa zilianzishwa miaka mingi iliyopita, zimekuwa na mitaji mikubwa na usimamizi wa kisasa, lakini maendeleo ya haraka ya kampuni za China katika miaka ya karibuni yamefanya kampuni za China kuwa na ubora wake maalumu. Kwa mfano, kampuni za usafirishaji wa haraka za nchini zina nguvu kubwa ya ushindani katika shughuli za usafirishaji za nchini zikilinganishwa na kampuni za kimataifa.

Watu wa sekta hiyo wamesema, ili kushindana na kampuni za usafirishaji wa haraka wa barua na vifurushi za nchi za nje, kampuni za usafirishaji za nchini, ambazo bado ni ndogo na hazina mitaji ya kutosha, zinatakiwa kuimarisha ushirikiano wao na kuanzisha muungano ili kupanua maeneo ya huduma na kuongeza uwezo wa ushindani.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-21