Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-21 15:46:39    
Mkoa wa Shandong, China yaharakisha ujenzi wa mabomba ya maji vijijini

cri
Ofisi ya Maji ya mkoa wa Shandong China inasema kuwa, mwaka huu mkoa wa Shandong utatumia Yuan bilioni 3 katika kuharakisha ujenzi wa mabomba ya maji vijijini, hatua ambayo itawanufaisha watu milioni 9.

Mwaka 2005 mkoa wa Shandong ulitumia jumla ya Yuan bilioni 1.5 kujenga mabomba ya maji kwenye sehemu 4,673 kwa kutoa maji safi vijijini, hatua ambayo iliwanufaisha watu milioni 6, na idadi hiyo inachukua asilimia 52 ya wanavijiji wote mkoani humo. Mwaka huu, mkoa wa Shandong utaongeza nguvu katika kuhimiza ujenzi wa mabomba ya utoaji wa maji vijijini, ili kuwawezesha asilimia 70 ya wanavijiji wapate huduma ya maji safi.

Shandong ni mkoa wenye idadi kubwa ya watu nchini China, zaidi ya watu milioni 70 wa mkoa huo wanaishi vijijini. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2004, asilimia 42.6 ya wanavijiji walitumia maji safi, lakini wengine zaidi ya milioni 37 bado walikuwa hawajapatiwa maji safi. Imefahamika kuwa, mkoa wa Shandong ulianzisha ujenzi wa mabomba ya utoaji wa maji vijijini kuanzia mwaka 2005, ili kufanya juhudi za kuviwezesha zaidi ya asilimia 80 ya vijiji kutumia maji safi na salama ndani ya miaka mitatu.

Wakati wa kutekeleza ujenzi huo, mkoa wa Shandong umejitafutia njia mwafaka ya kupata maendeleo, yaani kufanya uendeshaji na usimamizi wa ujenzi huo kutokana na vigezo na utaratibu wa soko. Kutokana na suala la ukosefu wa fedha za ujenzi, mkoa wa Shandong ulilegeza masharti ya kuingia kwenye soko la utoaji wa maji safi vijijini, kuingiza utaratibu wa kisoko na kuhimiza wakulima kuanzisha ushirika wa utoaji maji, pia kuhimiza mashirika kuwekeza vitega uchumi katika shughuli za utoaji wa maji safi vijijini. Aidha mkoa huo ulitoa ruzuku kwa mikopo ya ujenzi wa utoaji maji safi vijijini kwa miaka miwili mfululizo.

Katika mkoa mwingine wa China Henan, baada ya kutatuliwa kimsingi tatizo la utoaji maji safi vijijini mkoani humo, mwaka 2005 mkoa huo ulitumia Yuan milioni 323 kuchimba visima 721, na kutatua suala la usalama na usafi wa maji kwenye vijiji 965 vyenye wakazi milioni 1.5 ambavyo vilikuwa na hali mbaya zaidi ya uchafuzi wa maji mkoani humo.

Imefahamika kuwa kuanzia mwaka 2001 hadi mwishoni mwa mwaka 2003, mkoa wa Henan ulitumia jumla ya Yuan bilioni 1, kujenga mradi laki 1 za utoaji wa maji safi vijijini, na kutatua kwa kimsingi tatizo la maji vijijini mkoani humo. Lakini kutokana na sababu mbalimbali, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2004, watu milioni 20 mkoani humo bado hawajaweza kutumia maji salama.

Ili kuondoa kabisa hali mbaya ya uchafuzi wa maji kwenye sehemu kadhaa mkoani Henan, na kuhakikisha usalama wa maji ya kunywa, mwaka 2004 serikali ya mkoa wa Henan ilitoa uamuzi wa kutumia Yuan milioni 240, kutatua suala la usalama wa maji ya kunywa kwa watu milioni 1.2 walioko kwenye vijiji 800 vyenye hali mbaya zaidi ya uchafuzi wa maji.

Katibu wa Kamati ya chama cha mkoa wa Henan Bw. Xu Guangchun alifanya ukaguzi mara kwa mara kwenye sehemu unapofanyika ujenzi, na serikali ya mkoa wa Henan ilifanya mikutano mara nyingi ili kutatua matatizo yaliyopo kwenye hatua ya utekelezaji wa ujenzi huo.

Mkuu wa Ofisi ya maji ya Mkoa wa Henan Bw. Zhang Haiqin alieleza kuwa, baada ya juhudi za ngazi mbalimbali za kamati za chama na idara za maji, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005, mkoa wa Henan ulitumia jumla ya Yuan milioni 323, kuchimba visima 721 na kutatua suala la usalama wa maji ya kunywa kwa watu milioni 1.5 walioko kwenye sehemu zenye hali mbaya za uchafuzi wa maji.

Idhaa ya Kiswahili 2006-02-21