Hivi karibuni maambukizi ya homa ya mafua ya ndege inayoenea kwa kasi yamefuatiliwa na jumuiya ya kimataifa, ambayo inajitahidi kuimarisha udhibiti kuhusu maambukizi hayo. Wataalamu husika wametoa wito wa dharura wakitaka nchi mbalimbali zijitahidi kutokomeza virusi vya homa ya mafua ya ndege vinavyogunduliwa hivi sasa, kufanikisha mapema iwezekanavyo utafiti kuhusu mabadiliko ya virusi vya ugonjwa huo na kutengeneza chanjo yenye ufanisi zaidi.
Tokea mwishoni mwa majira ya joto na mwanzoni mwa majira ya mpukutiko, duru jipya la maambukizi ya homa ya mafua ya ndege liliibuka, hususan tokea mwezi Februari mwaka huu, homa ya mafua ya ndege iliibuka kwa nyakati mbalimbali katika nchi na sehemu nyingi za mabara matatu ya Ulaya, Asia na Afrika. Hadi sasa maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yamethibitishwa kuibuka kwa nyakati tofauti katika nchi nyingi za Ulaya zikiwemo Italia, Ugiriki, Austria, Ujerumani, Slovenia, Ufaransa, na kwenye nchi za Malaysia, Iran, India na Azerbaijan. Nchini Uturuki na Indonesia watu wengi wamekufa kutokana na kuambukizwa virusi hivyo. Lilifuata bara la Afrika, baada ya kuibuka maambukizi ya homa ya mafua ya ndege tarehe 8 mwezi huu nchini Nigeria, sehemu ya Afrika ya magharibi, habari mbaya zilisikika kuhusu maambukizi ya homa ya mafua ya ndege nchini Misri iliyoko sehemu ya kaskazini ya bara hilo. Hivi sasa maambukizi ya ugonjwa huo yanaelekea kuenea zaidi.
Baada ya kuibuka kwa duru jipya la maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, shirika la afya duniani pamoja na mashirika ya kikanda na serikali za nchi husika zilichukua hatua kwa haraka zikiwa ni pamoja na kuitisha mikutano ya kimataifa na kubuni sera mpya za udhibiti wa maambukizi ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo. Mkutano wa uchangishaji fedha wa udhibiti wa maambukizi ya homa ya mafua ya ndege duniani ulifanikiwa kufanyika mwezi Januari mwaka huu hapa Beijing, ambapo washiriki walikuwa na maoni ya namna moja kuhusu udhibiti wa maambukizi ya homa ya mafua ya ndege duniani. Mkutano wa madaktari wa mifugo wa Ulaya uliofanyika katikati ya mwezi huu umeimarisha udhibiti kuhusu uagizaji wa kuku, mabata na vitu vingine kutokana na nyama zao, na kutaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zichinje kuku na mabata wote walioambukizwa au wanaodhaniwa kuwa wameambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege, na kutaka kamati ya umoja wa Ulaya itenge fedha kuzisaidia nchi wanachama zitekeleze mpango mmoja wa udhibiti kuhusu maambukizi ya homa ya mafua ya ndege.
Hivi sasa bara la Afrika ni sehemu inayokabiliwa changamoto kali zaidi. Kutokana na upungufu wa fedha, zana za usimamizi, teknolojia, mazingira hafifu ya usafi na ufahamu kuhusu maambukizi husika, nchi za Afrika licha ya kujitahidi zenyewe pia zinahitaji misaada ya kimataifa. Hivi sasa hali ya hewa inaanza kubadilika kati ya sehemu ya kusini na kaskazini, hivyo ndege wenye virusi wataanza kuhamia sehemu ya kaskazini, katika hali hiyo, nchi zote zinatakiwa kushirikiana ili kushinda vita hiyo dhidi ya maambukizi ya homa ya mafua ya ndege.
Maofisa, wataalamu na wasomi husika wamesema, hivi sasa kipaumbele kingewekwa katika pande zifuatazo: Kwanza, kuchinja kuku na mabata wote walioambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege, kudhibiti biashara na uchukuzi wa kuku na mabata, kuepusha kukutana kati ya kuku na mabata wanaoshukiwa kuambukizwa virusi na binadamu, ili kuteketeza kwa kiwango cha juu zaidi virusi vya asili vya homa ya mafua ya ndege na kuzuia kadiri iwezekanavyo virusi vya aina ya H5N1 kubadilika na kuenea zaidi. Pili kuharakisha uzalishaji wa chanjo dhidi ya virusi vya aina ya H5N1. Tatu, tuwe na tahadhari kuhusu maambukizi ya virusi hivyo. Na nne ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kutoa misaada kwa haraka kusaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto hiyo.
|