Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-23 15:19:17    
Waandishi hodari wa Kabila la Wamulao

cri

Watu wa kabila la Wamulao wanaishi katika mkoa wa Guangxi, kusini mwa China. Kabila hilo lina watu wapatao laki moja na elfu 50 kwa hivi sasa, lakini miongoni mwao wamejitokeza waandishi hodari zaidi ya 50 ambao wanatunga fasihi kuhusu maisha ya watu wa kabila la Wamulao.

Wilaya inayojiendesha ya kabila la Wamulao inaitwa Luocheng, iko milimani katika mkoa wa Guangxi wa kusini mwa China. Wilaya hiyo inazungukwa na milima, ambapo mto mmoja unapita katikati ya milima hiyo. Katika kando mbili za mto huo, kuna mashamba yenye rutuba na misitu ya mianzi. Watu wa kabila la Wamulao wanakaa katika mazingira hayo ambayo ni kama pepo kizazi baada ya kizazi. Na katika ngano ya kabila hilo, sehemu hiyo ni maskani ya Fenghuang, aina ya ndege mtakatifu anayetajwa mara kwa mara katika hadithi za kale za China.

Hivi sasa kuna waandishi zaidi ya 50 wa kabila la Wamulao wanaojulikana katika uwanja wa fasihi nchini China. Hali hii inatokana na utamaduni wa kabila hilo wa kupenda fasihi, kujifunza kutoka tamaduni nyingine na kutilia maanani elimu.

Katika historia kabila la Wamulao na kabila la Wahan ni majirani. Wamulao walijifunza mengi kutoka kwa tamaduni za kabila la Wahan na makabila mengine madogomadogo. Kwa hiyo Wamulao walijitia katika utamaduni wa Kichina tangu zamani, na kufuatia desturi ya kuheshimu walimu na kutilia maanani zaidi elimu. Mwandishi maarufu wa vitabu wa kabila hilo ambaye ni mjumbe wa Shirikisho la waandishi wa vitabu la China Bw. Pan Qi alifafanua kuwa, watu wa kabila la Mulao wanaheshimu sana utamaduni.

"Hapo mwanzoni watu wa kabila la Wamulao walitekeleza utaratibu wa kulima 'mashamba ya mafunzo'. Maana yake ni kuwa, katika kila kijiji kulikuwa na shamba lenye ukubwa wa hekta 0.7 hivi, lililotengwa kuwa shamba la mafunzo. Wanavijiji walishika zamu ya kulima shamba hilo, na mavuno yake yaliwekwa kuwa ada za masomo ya watoto wote wa kijiji hicho. Utaratibu huo unafanana na mfuko wa masomo wa hivi sasa. Kwa hiyo kuenzi utamaduni na kupenda kusoma ni mtindo wa kabila la Wamulao. "

Licha ya kujifunza kutoka kwenye tamaduni nyingine, kabila la Wamulao lina utamaduni wake maalumu kwamba, watu wa kabila hilo wanapenda kuimba nyimbo walizotunga wenyewe. Na hiki pia ni chanzo kimoja cha kuleta ustawi wa fasihi. Mahala wanapoishi Wamulao hujulikana kama maskani ya nyimbo za kienyeji, ambapo kila mtu anajua kuimba, na nyimbo huimbwa katika matukio mbalimbali na mahala popote. Kuimba nyimbo ni sehemu ya maisha ya watu wa kabila la Wamulao. Kutokana na utamaduni wa namna hii, katika vijiji vya Wamulao, watu waliopata elimu wanapenda kutunga kazi za fasihi kwa mujibu wa nyimbo walizosikia utotoni mwao, kwa hiyo wamejitokeza waandishi wengi wa vitabu wa kabila la Wamulao.

Kati ya waandishi hao, mshairi maarufu Bw. Bao Yutang alijifunza mengi kutoka kwa nyimbo za kienyeji. Mzee huyo ana umri wa miaka 72, alizaliwa katika familia ya wakulima na kuvutiwa na fasihi tokea utotoni mwake. Akikumbusha alisema, "Utotoni mwangu nilijifunza mengi kutoka kwa utamaduni wa kabila langu. Babu na bibi walitusimulia hadhithi, wakati tulipopumzika katika siku za joto au tulipokuwa tunaota moto katika siku za baridi. Mbali na hadithi, kitu kingine muhimu ni nyimbo za kienyeji. Nyimbo hizo ni nyingi sana katika maeneo wanapoishi watu wa kabila la Wamulao. Wakati wa mwaka mpya, sikukuu, ndoa na mazishi, tunaimbaimba na kuimba nyimbo ndio mazungumzo."

Inasemekana kuwa, Bw. Bao Yutang alipokuwa na umri zaidi ya miaka 10, majambazi walishambulia maskani yake mara kwa mara. Ili wanavijiji wanzake watambue uhalifu wa majambazi, mtoto huyo alitunga wimbo mmoja ambao ulifahamika sana. Hapo baadaye mkuu wa majambazi alishindwa na kutoroka, alipokaribia kwenye kijiji kingine alisikia wimbo wa kumsaka, hakuthubutu kurudi nyumbani na akakamatwa na wanavijiji. Kwa kuoneshwa nguvu kubwa ya nyimbo za kienyeji, Bao Yutang alijitia zaidi katika utungaji wa nyimbo na akawa maarufu nchini China katika kutunga maneno ya nyimbo.

Bw. Bao ana watoto wawili wa kiume, ambao pia ni waandishi wa vitabu hodari miongoni mwa wanafasihi wa vitabu wa China. Mmoja ni mwandishi wa makala na mwingine ni mshairi.

Katika jukwaa la fasihi nchini China, waandishi wa vitabu wa kabila la Wamulao wana sifa maalumu. Wameingia katika karibu nyanja zote za fasihi, mashairi, riwaya, makala na michezo ya kuigiza, na kupata mafanikio. Naibu mkurugenzi wa Shirikisho la waandishi wa vitabu la mkoa wa Guangxi Bw. Tang Zhengzhu alitoa tathmini kwa waandishi hao.

"Waandishi wengi maarufu wakiwemo Pan Qi, Gui Zi na Bao Yutang wanatoka kabila la Wamulao. Waandishi hao ni maarufu mkoani Guangxi na nchini China, wametoa mchango muhimu kwa ustawi wa utamaduni wa China. Katika kazi zao za fasihi, tunaona sifa yao ya pamoja, ambayo imeambatanisha vizuri umaalumu wa utamaduni wa kabila lau, msingi wa utamaduni huo na mitindo ya fasihi ya kisasa. Kazi hizo zinaonesha muungano wa umaalumu wa kikabila na wa enzi hii."

Tukizungumzia waandishi wa vitabu wa kabila la Wamulao, hatuwezi kuepuka jina la Gui Zi. Mwandishi huyo anayekaribia umri wa miaka 50, yupo katika kilele cha kazi yake, pia ana athari kubwa katika jukwaa la fasihi la China kwa hivi sasa. Katika kitabu kiitwacho "Fasihi maarufu duniani katika karne ya 20" kilichochapishwa na Chuo Kikuu cha ualimu cha Beijing, katika sehemu ya riwaya za China, ni waandishi wa vitabu wapato 16 tu na kazi zao waliopewa sifa ya kuchaguliwa, mmojawapo ni Gui Zi. Riwaya yake iliwahi kupewa tuzo ya fasihi ya Luxun, ambayo ni tuzo ya juu zaidi ya fasihi nchini China. Hii ni ishara kuwa, kwa niaba ya waandishi wa vitabu wa kabila la Wamulao, amefika kilele cha fasihi za China.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-23