Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-23 15:30:33    
Kijana Mjerumani na maisha yake nchini China

cri

Bw. Andreas Fulda ni Mjerumani, anafahamu kuongea Kichina. Hata Wachina wenyewe waliosikia maelezo yake hawakuamini mgeni alikuwa anaongea Kichina sanifu namna hii. Mgeni huyo Bw. Andreas Fulda ni kijana mwenye umri wa miaka 28.

Bw. Faulda sasa anafanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali nchini China. Shirika hilo linalenga kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo ya watu maskini ya China, hasa linashughulikia kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini China na nje ya China katika mambo ya kuondoa umaskini, kuhifadhi mazingira na maendeleo ya jamii. Katika jumuiya hiyo, kazi ya Xiao Fu ni kutoa mapendekezo kwa miradi mbalimbali na kuendeleza ushirikiano na vyombo vya kimataifa.

Alimwambia mwandishi wa habari kuwa, alivutiwa na China kwa sababu ya mwanafunzi mwenzake msichana aliyekuwa anasoma kwenye shule ya sekondari.

"Yeye ni msichana mrembo mwenye asili ya Kichina. Alifuatana na wazazi wake waliokuwa wanafanya kazi nchini Ujerumani, na tulisoma shule moja ya sekondari. Msichana huyo ndiye aliyenipa hamu ya kuifahamu China."

Kwa kijana Faulda, msichana huyo kutoka Mashariki alikuwa tofauti na Wajerumani wenzake. Bw. Fulda akaanza kuvutiwa na utamaduni wa Mashariki hasa utamaduni wa China wenye sifa ya uvumilivu na utulivu. Baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, alipata uungaji mkono wa kaka yake na kujiunga na kitivo cha sanaa ya Mashariki cha Chuo Kikuu cha Cologne, Ujerumani. Bw. Faulda alikuja Beijing miaka minne iliyopita na kuanza kufanya kazi ya msaidizi wa kimataifa katika shirika hilo lisilo la kiserikali.

"Naona katika maisha yangu ya siku zilizopita na kazi yangu, kulikuwa na mambo mengi yaliyonihusisha na China. Nina bahati nzuri ya kupata nafasi ya kuifahamu nchi hiyo kutoka kwa pande mbalimbali, jambo ambalo linanifurahisha."

Bw. Faulda anapenda sana kazi yake nchini China, pia ana bidii katika kazi hiyo. Shirika analofanyia kazi liko mjini Beijing, pia anakwenda sehemu nyingine za China mara kwa mara kushiriki kwenye mikutano au kufanya utafiti. Kutokana na kazi hiyo, anakutana na Wachina wa kawaida. Kwa hiyo alizoea kwa haraka maisha nchini China.

Marafiki zake Wachina wanamwita Xiao Fu kwa desturi ya Kichina. Wafanyakazi wenzake wanamchukulia kuwa ni mtu mwenye unyofu. Wanapojadiliana masuala mbalimbali, Xiao Fu anatoa maoni yake bila kuficha. Akiona jambo ni zuri anasema zuri, akiona jambo si zuri anasema si zuri, hajui kuficha ili kuwafurahisha wengine. Mbali na hayo, Xiao Fu anafanya kazi kwa makini na kuzingatia mshikamano na ushirikiano na wenzake, kwa hiyo wafanyakazi wenzake Wachina wanamkubali na kumpenda. Bosi wake Bw. Huang Haoming ambaye ni katibu mkuu wa shirika hilo alimsifu, akisema "Anafanya kazi kwa makini na kufuata utaratibu. Anajitetea kuwa, ingawa mimi ni Mjerumani lakini nawajibika kwa shirika la kuhimiza ushirikiano wa jumuiya za kiraia, sio mimi mwenyewe. Labda nina maoni tofauti, lakini inanibidi kulinda maslahi ya shirika hilo."

Katika muda alioishi na kufanya kazi nchini China, Bw. Faulda sio tu amekuwa akiaminiwa na wafanyakazi wenzake Wachina, bali pia amepata marafiki wengi Wachina. Bi. Song Qinghua anayefanya kazi katika shirika lingine lisilo la kiserikali ni miongoni mwa marafiki zake. Bi. Song ni mkubwa zaidi kuliko Bw. Faulda, kwa hiyo akiwa na matatizo huwa anamwomba ushauri wa dada huyo mkubwa, hata ikiwa ni matatizo ya binafsi likiwemo tatizo la yeye na mchumba wake.

Alipomzungumzia Bw. Faulda, Bi. Song alisema "Picha ya kwanza niliyopata kuhusu Faulda ni kuwa anajua kuongea Kichina sanifu, hakuna matatizo ya kuwasiliana naye. Akiwa mgeni anafuatilia sana maendeleo ya China. Watu wanasema Wajerumani wanafanya kazi kwa makini sana . Kweli nimeona sifa hiyo kutokana na hali yake ya kuchapa kazi."

Katika muda aliyoishi hapa Beijing, maendeleo ya kasi katika jamii ya China siku zote yalimvutia Bw. Faulda. Alisema anafurahia kwenda kazini kila asubuhi. Wakati wa mapumziko, anapenda kupiga picha za maisha ya Wachina wa kawaida, na kwenda mihakawani kuonja chakula kizuri cha Kichina. Pia amejifunza kuimba nyimbo ya kienyeji ya Kichina.

Bw. Faulda hajafunga ndoa. Alisema anawapendelea wasichana wanaofuata mila na desturi za jadi za China, ambao wanaonekana ni wapole na wachapa kazi, labda atamwoa Mchina. Ni miaka 10 imepita tangu alipoanza kujifunza lugha ya Kichina, Bw. Faulda anaona utamaduni wa China umekuwa sehemu ya maisha yake, awe yupo China au awe Ujerumani.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-23