Baada ya msikiti wa Ali al-Hadi kubomolewa kwa mabomu, mgongano kati ya madhehebu ya Shiyah na Suni umekuwa mkali, na watu karibu mia moja wamepoteza maisha yao katika mgogoro uliotokea tarehe 23. kutokana na hali hiyo, madhehebu ya Suni yameamua kuacha kuendelea na mazungumzo kuhusu kuundwa kwa serikali.
Baada ya tukio hilo kutokea, rais Jalal Talabani na waziri mkuu Ibrahim al-Jaafari wa Iraq, kiongozi wa madhehebu ya Shiah Ali al-Sistani na baraza la wazee la madhehebu ya Suni pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan na jumuyia ya kimataifa wote walilaani vikali tukio hilo na kutaka watu wa Iraq wavumilie na wasichukue hatua za kulipa kisasi.
Hata hivyo, tukio hilo limesababisha mashambulizi kwa mara nyingine tena nchini Iraq. Misikiti na waumini wa madhehebu ya Suni wamekuwa shabaha ya kushambuliwa na waislamu wa madhehebu ya Shiah waliokasirika. Baraza la wazee la madhehebu ya Suni lilisema kuwa katika siku mbili za karibuni misikiti 168 ilishambuliwa, katika mashambulizi hayo mashehe kumi waliuawa na maimamu 15 walitekwa nyara. Wizara ya Mambo ya Ndani ilitangaza kuwa mjini Baghdad tu misikiti 90 ilishambuliwa.
Pamoja na mashambulizi hayo, watu wenye silaha wasiofahamika walitumia fursa hiyo kufanya rabsha na kushambulia askari polisi, jeshi la Marekani nchini humo, waandishi wa habari na raia na kiasi cha watu 130 waliuawa.
Mgongano uliokuwepo kati ya madhehebu ya dini umezidi kuwa mkali na mashambulizi ya kisilaha yamesababisha msukosuko mpya wa kisiasa na mazungumzo kuuhusu kuundwa kwa serikali yaliyokuwa yakiendelea yalipaswa kusimama. Chama kikubwa cha madhehebu ya Suni "Iraqi Accordance Front' kilichopata nafasi 44 kati ya nafasi 275 katika bunge tarehe 23 kilitangaza kuwa hakitahudhuria mkutano wa dharura wa viongozi wa makundi yote ulioitishwa na rais Talabani katika siku hiyo, na kilisimamisha mazungumzo kuhusu kuundwa kwa serikali ili kulaani mashambulizi ya misikiti ya madhehebu ya Suni. Msemaji wa chama hicho alisema, serikali ya mpito na jeshi linalokalia nchini Iraq lazima wabebe lawama kutokana na hali mbaya ya usalama, na kujenga upya misikiti iliyoharibiwa na kutoa fidia kwa watu walioathirika na kuwaadhibu watu waliohusika.
Ingawa hadi sasa bado hakuna jumuyia yoyote iliyotangaza kuwajibika na mashambulizi ya msikiti wa Ali al-Hadi, lakini mshauri wa usalama wa taifa wa Iraq Rubaie na mratibu wa sera za Iraq katika Baraza la Serikali ya Marekani Mames Jeffrey wote wanaona kuwa Kundi la al-Qaeda lilipanga mashambuzi hayo, ili kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iraq na kuharibu kuundwa kwa serikali na hali mbaya ya sasa katika usalama na siasa yumkini itasababisha vita hivyo.
Ili kuzuia hali isizidi kuwa mbaya, hatua nyingi zimechukuliwa. Wizara ya mambo ya ndani ya Iraq tarehe 23 ilitangaza kufuta siku zote za mapumziko za askari polisi na jeshi na kurefusha muda wa kutoruhusu kutembea mjini Baghdad. Rais Talabani ameyataka makundi yote yavumilie na kuzuia kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Vyombo vya habari vinaona kuwa mgongano kati ya mashehebu ya Shiah na Suni umekuwepo kwa siku nyingi, na mapambano ya kugombea maslahi ya kisiasa yalikuwa makali tokea kumalizika kwa vita vya Iraq. Watu wa madhehebu ya Shiah wanalaani watu wa madhehebu ya Suni kufanya mashambulizi ya kigaidi, na watu wa madhehebu ya Suni wanalaani watu wa madhehebu ya Shiah kukandamiza watu wa madhehebu ya Suni kwa kutumia fursa ya kuendesha serikali ya muda. Baada ya uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Desemba mwaka jana watu wa madhehebu ya Shiah na Suni walikuwa na msimamo mkali katika mgawanyo wa madaraka katika serikali.
Wachambuzi wanaona kuwa mashambuzi ya kisilaha ambayo pengine yatasababisha vita wenyewe kwa wenyewe hayatakuwa na mwafaka wowote kwa madhehebu yote, viongozi wa makundi yote wanapaswa kuwa watulivu ili kuzuia hali isiwe mbaya zaidi na waendelee kushughulika na mchakato wa siasa ili kujenga serikali yenye umoja wa kitaifa.
Idhaa ya kiswahili 2006-02-24
|