Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-24 15:52:47    
Jinsi madaktari wa China wanavyowahudumia wagonjwa wa Tanzania kwa moyo mkunjufu

cri
Serikali ya China ilianza kupeleka vikundi vya madaktari nchini Tanzania kuanzia mwaka 1968, na kila mwaka kwa nyakati tofauti inaipatia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Zanzibar dawa na vifaa vya tiba vyenye thamani ya Yuan za Renminbi laki nne. Katika miaka 38 iliyopita, madaktari wa China walipambana na matatizo ya aina mbalimbali ambayo ni pamoja na hali duni ya vifaa vya matibabu na kutoweza kuzoea maisha ya huko, na kufanya kazi kwa bidii katika kuwasaidia wananchi wa Tanzania kuondokana na maumivu ya magonjwa kwa moyo mkunjufu, na wamesifiwa na kupendwa sana na watu wa Tanzania.

Jukumu la kupeleka madaktari Tanzania bara linachukuliwa na mkoa wa Shandong, mkuu wa kikundi cha madaktari wa China Bwana Gan Lianxi alisema:

"Kuanzia mwaka 1968 hadi leo, mkoa wa Shandong umeshapeleka vikundi 19 vya madaktari elfu moja hivi nchini Tanzania. Walifanya kazi katika sehemu mbalimbali za Tanzania bara."

Mkuu Gan Lianxi alisema, ili kutatua tatizo la wanavijiji waishio sehemu za mbali kushindwa kwenda kuonana na madaktari, madaktari wa China wamewahi kutumia njia ya kupanda gari kwenda kuonana na wagonjwa wa vijijini kila siku. Inafahamika kuwa, kikundi cha sasa cha madaktari wa China kinaundwa na madaktari 25, ambao wanafanya kazi katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, hospitali ya Tabora na Dodoma zilizoko katika sehemu ya kati ya Tanzania na hospitali ya Musoma iliyoko katika sehemu ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Bwana Gan Lianxi alisema, ili kutoa huduma bora kwa watu wanaohudumiwa, serikali ya China inatilia maanani sana kazi ya kuwachagua madaktari. Kwanza inawachagua wale wenye ustadi na uzoefu, halafu wanawapa mafunzo ya lugha ya Kiingereza kwa miezi kumi, na kuchaguliwa rasmi baada ya kufaulu mtihani. Japokuwa hali ya maisha ya hivi sasa ya madaktari wa China nchini Tanzania imeboreshwa zaidi kuliko zamani, lakini ikilinganishwa na ile ya nchini China bado kuna tofauti kubwa. Lakini madaktari wa China wanajitahidi kadiri wawezavyo kusaidia kuwatibu wagonjwa wa Tanzania.

Hii ni mara ya nne kwa Bw. Gan Lianxi kufanya kazi nchini Tanzania, anaipenda Tanzania na watu wake na kuifanya kazi ya kuwasaidia watanzania kama jukumu lake muhimu. Kama madaktari wengine wa China nchini Tanzania, Bw. Gan si kama tu anawasaidia wagonjwa wa Tanzania kwa ustadi wake mzuri, bali pia amejifunza jinsi ya kufua nguo na kupika chakula.

Kutokana na kubadilika kwa mazingira ya kazi na hali duni ya matibabu, itachukua muda kwa madaktari wa China kuzoea hali halisi ya hospitali za nchini Tanzania. Bwana Bi Weimin aliyefanya kazi katika hospitali ya Dodoma alisema:

"Tukiwa madaktari, jukumu letu muhimu ni kuwahudumia vizuri watu wa Tanzania. Tofauti na nchini China hali ya tiba ya hapa ni duni, hivyo tunapaswa kuwafanyia wagonjwa upasuaji kutokana na uzoefu tulio nao."

Zaidi ya hayo, magonjwa ya kuambukiza kama vile malaria na Ukimwi ni changamoto nyingine inayowakabili madaktari wa China. Kwa mfano walipotoka kwenda kuonana na wagonjwa nyumbani kwao usiku, hawawezi kuzuia kuumwa na mbu wenye viini vya malaria, wanafahamu vizuri hatari ya ugonjwa wa Ukimwi, lakini walipokutana na wagonjwa wenye virusi vya Ukimwi wanaohitaji operesheni hawana neno lingine ila tu kutekeleza jukumu lao ipasavyo, madaktari wa China ndivyo wanavyowahudumia wagonjwa wa Afrika kwa moyo wa kujitolea.

Hospitali za Tanzania hukabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari, kwa kawaida daktari mmoja anashughulikia vitanda 100 vya wagonjwa, hivyo madaktari wa China wanakuwa na kazi nyingi sana na wakati mwingine kuchelewa kula kwao ni jambo la kawaida.

Bwana Gan Lianxi alisema:

"Kila Madaktari wa China kila wanapofanya operesheni hawana budi kushinda matatizo ya aina mbalimbali, lakini wanajitahidi kuwahudumia wagonjwa kadiri wawezavyo. Ili kutatua upungufu mkubwa wa dawa, madaktari wa China walianza kuwatoza wagonjwa gharama ndogo ya dawa kuanzia mwaka 1994, na kutumia fedha hizo kununua dawa nyingine ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa."

Wagonjwa wa Tanzania kuanzia raia wa kawaida hadi maofisa wa ngazi ya juu waliowahi kuhudumiwa na madaktari wa China hawahesabiki, ambao ni pamoja na baba wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere, katibu mkuu wa zamani wa chama tawala cha mapinduzi CCM Bwana Rashid Kawawa, rais wa zamani Bwana Benjamin Mpaka na waziri mkuu wa zamani Bwana Fredrick Sumaye. Mwaka juzi Bwana Benjamin Mkapa aliumia mfupa wa goti lake, na ilikuwa hata vigumu kutembea, aliwahi kufanyiwa operesheni kwenye hospitali moja ya Zurich nchini Uswisi, lakini maumivu yake bado hayakuweza kuondolewa, lakini baadaye alitibiwa na daktari wa China kwa tiba ya acupuncture, ambayo ilimsaidia sana.

Moyo mkunjufu wa madaktari wa China wa kufanya kazi na ustadi wao mzuri umesifiwa sana na serikali ya Tanzania na watu wake. Mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma Bwana John Mtimba alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari aliisifu sana serikali ya China kwa kuwapeleka madaktari kuwasaidia watu wa Tanzania katika miaka 38 iliyopita. Alisema:

"Kwanza tunaishukuru serikali ya China kwa kutupatia msaada wa madaktari, hapa tunapata madaktari watano kila baada ya miaka miwili, na wameweza kusaidia kutoa huduma za afya, hasa upande wa matibabu. Wametusaidia sana kwa sababu Tanzania haina madaktari bingwa wa kutosha. Wanaokuja ni madaktari bingwa, ambao wanafanya kazi kwa moyo bila malalamiko, na wanafanya kazi kwa kujituma. Tunawashukuru sana kwa kazi wanazofanya. Natumai kuwa, muda wa madaktari wa China wanaofanya kazi hapa ungerefushwa, na tunaomba waendelee kuja Tanzania, na sisi tuko tayari kushirikiana nao katika kutoa huduma, na kuboresha huduma ya afya kwa wananchi."

Idhaa ya kiswahili 2006-02-24