Makamu wa rais wa Iran ambaye pia ni mwenyekiti wa shirika la nishati ya atomiki la taifa Bw. Gholamreza Aghazadeh tarehe 26 baada ya kumaliza mazungumzo na kiongozi wa shirika la nishati ya atomiki la Russia Bw. Sergei Kirienko huko Bushehr nchini Iran alisema, kikanuni, pande mbili zimeafikiana kuhusu pendekezo lililotolewa na Russia la kujenga kiwanda cha pamoja cha usafishaji wa uranium nchini Russia. Wachambuzi wanasema, hatua zilizofikiwa na pande mbili za Iran na Russia zimeleta tumaini jema kwa utatuzi wa amani wa suala la nyukilia la Iran.
Katika mkutano na waandishi uliofanyika siku hiyo, Bw. Kirienko na Bw. Aghazadeh walitangaza pande mbili watakuwa na mazungumzo tena huko Moscow siku chache zijazo. Bw. Kirienko alisema, anaamini kuwa baada ya duru lingine la mazungumzo, Russia na Iran zitakuwa na maendeleo yanayoridhisha pande mbalimbali husika kabla ya kufanyika kwa mkutano wa baraza la uratibu la shirika la nishati ya atomiki duniani tarehe 3 mwezi Machi.
Waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergei Lavrov alitoa tamko siku ile huko Moscow akisema, suala la nyukilia la Iran litaweza kutatuliwa kwa njia ya amani.
Pendekezo la kujenga kiwanda cha pamoja cha kusafisha uranium nchini Russia lilitolewa kwa mara ya kwanza na Russia mwezi Desemba mwaka jana, ambalo linazingatia maslahi na ufuatiliaji wa pande mbalimbali, hivyo Umoja wa Ulaya na Marekani zilisema kuwa zinakubaliana na pendekezo hilo, isipokuwa Iran imekuwa ikisema pendekezo hilo bado halijakamilika na haikukubali pendekezo hilo, kwa kuwa haki ya Iran ya kusafisha uranium nchini mwake isingekataliwa. Tarehe 20 na 21 mwezi huu, Russia na Iran zilikuwa na mazungumzo ya kwanza huko Moscow kuhusu suala la nyukilia la Iran. Baada ya mazungumzo, ofisa wa Iran aliona, pande mbili za Iran na Russia zinaweza kuafikiana kuhusu kuanzisha kwa pamoja kiwanda cha kusafishia uranium. Kisha kiongozi wa shirika la nishati ya atomiki la Russia Bw. Kirienko akiongoza ujumbe wa nchi hiyo aliwasili Iran tarehe 24, na kuanza mazungumzo ya duru la pili, ambapo kikanuni, ziliafikiana kuhusu kujenga kiwanda cha pamoja cha kusafishia uranium.
Lakini wachambuzi wanaona, siku hiyo Iran ilieleza tu kukubali pendekezo lililotolewa na Russia kuhusu kujenga kiwanda cha pamoja cha kusafishia uranium, na haikutoa jibu wazi kuhusu suala linalofuatiliwa zaidi na jumuiya ya kimataifa la Iran kuacha mpango wa uvumbuzi wa nyukilia nchi hiyo yenyewe. Hivyo bado hakuna uhakika kuhusu utatuzi kamili wa suala la nyukilia la Iran.
Bw. Kirineko alipohojiwa na vyombo vya habari vya Russia siku hiyo, alisema, utatuzi wa suala la nyukilia la Iran ungekuwa na vitu viwili; Kitu cha kwanza, haki ya kila nchi ya kuendeleza nishati ya nyukilia kwa njia ya amani ingeheshimiwa, ambapo kanuni za kimataifa za kutoeneza silaha za nyukilia haziruhusiwi kuharibiwa. Kutokana na msimamo wa kanuni hiyo ya Russia, hatua ya kujenga kiwanda cha pamoja cha usafishaji wa uranium inalenga kulinda haki ya Iran ya kuendeleza nyukilia kwa njia ya amani, wala haijaondoa wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa juu ya kuendeleza peke yake nishati ya uranium kwa Iran. Hivyo, Iran inatakiwa kutoa ahadi wazi ya kuacha kuendeleza nyukilia kwenye nchi hiyo yenyewe.
Habari kutoka shirika la habari la Russia zinasema, ofisa mmoja wa ujumbe wa Russia unaoshiriki kwenye mazungumzo na Iran, alisema pande mbili za Russia na Iran zitakuwa na mazungumzo wiki ijayo kuhusu suala la nyukilia la Iran, ambapo Russia itatoa mpango kamili wa utatuzi wa suala la nyukilia la Iran, yaani kutaka Iran kuacha shughuli zote za usafishaji wa uranium na uendelezaji wa nyukilia wakati inaposaini mkataba na Russia wa kujenga kiwanda cha pamoja cha usafishaji wa uranium.
Tarehe 6 mwezi Machi, baraza la uratibu la shirika la atomiki duniani litaitisha mkutano kujadili suala la nyukilia la Iran. Wachambuzi wanaona kuwa suala hilo litaweza kutatuliwa ndani ya shirika la atomiki duniani, na kama itakuwa kwa njia ya amani au la, kwa kiwango kikubwa inategemeana na kama Russia itaweza kuisihi Iran iache shughuli za kusafisha uranium peke yake au la kabla ya kufanyika kwa mkutano huo.
|