Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-27 20:18:40    
Sherehe ya kuzinduliwa rasmi kwa Kituo cha 91.9 FM cha CRI yafanyika huko Nairobi Kenya na hapa Beijing China

cri

Leo tarehe 27 sherehe ya kuzinduliwa rasmi kwa Kituo cha 91.9 FM cha CRI imefanyika huko Nairobi Kenya na hapa Beijing, China, ambapo Mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian na msafara wake walioko Nairobi, Kenya, mkurugenzi wa shirika la utangazaji la Kenya KBC Bwana Waruru pamoja na balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli wamehudhuria sherehe hiyo huko Nairobi, na naibu mkuu wa Idara kuu ya radio, filamu na televisheni ya taifa ya China Bwana Tian Jin na manaibu wakurugenzi wa CRI Bwana Chen Minyi na Xia Jixuan pamoja na maofisa wanaohusika wamehudhuria sherehe iliyofanyika hapa Radio China kimataifa.

 

Kwenye sherehe hiyo kwanza Mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa aliongea kwa simu na Naibu mkuu wa Idara kuu ya radio, filamu na televisheni ya China Bwana Tian Jin, akiwaambia kuwa usikivu wa Kituo cha 91.9 FM cha CRI huko Nairobi Kenya ni mzuri sana, na sherehe ya kuzinduliwa rasmi kwa Kituo cha 91.9 iliyofanyika huko Nairobi iliendelea katika hali ya furaha.

Naibu mkuu wa Idara kuu ya radio, filamu na televisheni Bwana Tian Jin alitoa hotuba kwenye sherehe hiyo akisema, anapongeza kuzinduliwa rasmi kwa kituo cha FM cha Radio China kimataifa, amesema kituo hicho kitakuwa daraja la kuhimiza maingiliano ya kirafiki kati ya China na Kenya na wananchi wao. Aliishukuru serikali ya Kenya kuiunga mkono serikali ya China kujenga kituo hiki cha FM huko Nairobi Kenya, na amewataka wafanyakazi wa Radio China kimataifa wafanye juhudi kubwa za kuandaa vipindi vinavyokidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu walioko Kenya ili kuwavutia wasikilizaji wengi zaidi.

 

Balozi wa Kenya nchini China Bibi Ruth Sereti Solitei pia alitoa hotuba akisema, kama alivyosema Naibu mkuu wa Idara kuu ya radio, filamu na televisheni ya taifa ya China Bwana Tian Jin, historia ya urafiki kati ya China na Kenya ilianza tangu enzi na dahari, ambapo miaka 600 iliyopita, mwanamaji maarufu wa China Zheng He aliwahi kuongoza kikosi cha merikebu cha China kwenda pwani ya Kenya, na miaka 42 imepita tangu China na Kenya ziwekeane uhusiano wa kibalozi, China na Kenya zimefanya ushirikiano wa kirafiki katika sekta mbalimbali. Kenya inaona fahari kuwa sehemu ya kwanza kwa China kujenga kituo chake cha FM katika nchi za nje, anaamini kuwa kuzinduliwa kwa Kituo cha FM cha Radio China kimataifa kutaongeza urafiki na ushirikiano kati ya wananchi wa China na Kenya, matangazo ya kituo hiki yatawasaidia wananchi wa Kenya waifahamu China, pia yatawasaidia wananchi wa China waijue zaidi Kenya. Akisema:

Wiki kadhaa zilizopita nilikuwa Nairobi Kenya, nilipata nafasi ya kusikiliza matangazo ya Radio China kimataifa kwenye wimbi la FM, naweza kusema kuwa, usikivu wa matangazo hayo ni safi sana, watu wa Nairobi wanafurahia sana, hakika matangazo ya CRI kwenye wimbi la FM yatawavutia wasikilizaji wengi, kwani watu wa Kenya wana hamu kubwa ya kuijua China, matangazo hayo hata yatawahimiza wafanyabiashara wengi wa Kenya waje China kuanzisha shughuli kibiashara, ameipongeza tena Radio China kimataifa kufungua kituo hiki cha 91.9FM, na kuishukuru tena serikali ya China kuichukua Kenya kuwa mwenzi wake wa ushirikiano.

Na ofisa wa ubalozi wa Kenya Bwana Fred Ondieki alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari pia anasema:

Mimi napongeza sana kuzinduliwa rasmi kwa kituo cha FM cha Radio China kimataifa huko Nairobi Kenya, ni matumaini yetu kuwa matangazo ya Radio China kimataifa kwenye wimbi la FM huko Nairobi Kenya yatawavutia wasikilizaji wengi.