Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-28 15:18:35    
Uzalishaji wa magari madogo sana wahimizwa nchini China

cri

Serikali ya China inataka serikali za mikoa ziondoe vikwazo vilivyowekwa juu ya magadi madogo, ambayo yanachangia hifadhi ya mazingira, kabla ya mwezi Machi. Licha ya hayo serikali imetoa sera husika za kuhamasisha uzalishaji na ununuzi wa magari madogo. Mtaalamu husika amesema, kitendo hicho kinaonesha kuwa uzalishaji wa magari madogo nchini China utaharakishwa na kutarajiwa kuwa magari mengi madogo yatakayouzwa kwa wingi mwaka huu.

Kwenye soko moja la magari mjini Beijing, Bw. Ou Qing alikuwa akichagua gari dogo. Alimwambia mwandishi wetu wa habari, ameamua kununua gari moja dogo kutokana na serikali kutoa sera za kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya magari madogo na kupanda mfululizo kwa bei ya petroli.

"Bei ya magari makubwa ni ghali, na uwezo wangu bado ni mdogo. Lakini magari madogo yanakumbana na vikwazo vingi vya sheria ya barabarani hivyo nina wasiwasi kununua gari dogo. Baada ya kuondolewa vikwazo kwa magari madogo, magari madogo hayataathirika kutokana vikwazo vilivyowekwa, na bei yake ni nafuu. Tena matumizi ya petroli ya magari madogo ni madogo ikilinganishwa na magari makubwa, hivyo hata kama bei ya petroli itapanda zaidi, haitakuwa mzigo mkubwa kwa mwenye gari dogo."

Nchini China watu wanaotaka kununua magari madogo kama Bw. Ou ni wengi, hivyo magari madogo madogo yatauzwa sana katika soko la China. Takwimu zilizokusanywa na jumuiya ya viwanda vya magari ya China zinaonesha kuwa, idadi ya magari madogo yaliyouzwa katika mwaka 2005 ilichukua asilimia 50 hivi ya jumla ya magari yaliyouzwa nchini. Ingawa magari madogo yatauzwa sana nchini, lakini Bw. Ou bado ana wasiwasi mwingi.

"Nimeamua kununua gari dogo, nitanunua lile dogo zaidi, lakini nina wasiwasi juu ya usalama wake."

Uchunguzi uliofanywa na tovuti moja nchini unaonesha kuwa, baada ya kuondolewa kwa vikwazo husika kwa magari madogo, 39.2% ya wanunuzi wa magari wanataka kununua magari madogo. Uchunguzi huo unasema, wanunuzi wanaona sifa kubwa za magari madogo ni bei rahisi na matumizi madogo ya petroli, lakini upungufu wake ni nguvu ndogo, siyo salama sana na gari kuonekana kuwa la kiwango cha chini.

Watu wa sekta ya uzalishaji magari wana maoni tofauti na maoni ya umma kuwa magari madogo sana yanaonekana kuwa ya kiwango cha chini. Naibu meneja mkuu wa moja ya makampuni ya magari, Bw. Tang Teng alisema,

"Huenda watu wana maoni yasiyo sahihi kuhusu magari madogo, kwani wakizungumzia yale magari madogo, ni rahisi kwao kufikiria ni magari yale rahisi na ya teknolojia ya kiwango cha chini. Ukweli ni kwamba katika masoko ya magari ya kimataifa, magari madogo kabisa si yale ya kizamani."

Tokea muda mrefu uliopita, baadhi ya viwanda vya magari madogo vinafikiri kuwa uzalishaji wa magari madogo hauna faida kubwa, tena ili kupunguza gharama na bei ya magari madogo, viwanda hivyo havikutilia maanani sana teknolojia ya uzalishaji na sifa ya usalama, hivyo wanunuzi wengi wanadhani magari madogo sana ni magari hafifu.

Bw. Tang alisema hali hiyo imebadilika, viwanda vya magari vya China vinazingatia sana ubora wa magari madogo, wanaongeza baadhi ya zana ambazo hapo zamani ziliwekwa tu katika magari ya hali ya juu zikiwemo zana za kutunza gari, taa na viyoyozi vinavyojiendesha vyenyewe, mambo ambayo yamekuwa mwelekeo wa uzalishaji wa magari madogo katika siku za usoni.

Kampuni ya magari ya kwanza ya mji wa Tianjin ni moja ya kampuni za magari madogo. Mwaka uliopita ilizalisha magari madogo aina Xiali laki 2, ambayo yalichukua 30% ya nafasi ya soko la magari. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Wang Gang alisema, hivi sasa serikali imetoa sera za kukuhimiza uzalishaji wa magari madogo, kampuni yao itainua ubora wa magari ili kuvutia wanunuzi wengi. Aliongeza, "tunajitahidi kufanya magari madogo kuwa na sifa za magari ya kiwango cha juu, ili tuweze kutumia fedha kidogo kupata magari yanayoridhisha, kutumia nishati kidogo na kuchangia hifadhi ya mazingira ya asili."

Naibu mkurugenzi wa kamati ya kudumu ya wataalamu ya jumuiya ya viwanda vya magari nchini China, Bw. Rong Huikang alidokeza kuwa, mwaka huu China itarekebisha ukusanyaji wa kodi ya ununuzi wa magari, ambapo kodi ya magari madogo itapunguzwa ili kuvutia wanunuzi. Alisema, "Mwaka huu serikali itatoa sera nyingi za kuhamasisha uzalishaji wa magari madogo. Kwa mfano, kodi za ununuzi wa magari karibu ni sawa kwa hivi sasa. Baadaye kodi za ununuzi zitagawanyika katika ngazi kadhaa, kodi ya ununuzi wa magari madogo itakuwa ndogo zaidi. Habari zinasema, magari yatagawanyika katika ngazi 6 au 7 hivi, ambapo kodi ya ununuzi wa magari madogo itapunguzwa kwa kiasi kikubwa zaidi."

Imefahamika kuwa katika nchi za Ulaya, Japan na Korea ya Kusini, magari madogo yanapendwa zaidi na watu, nchi hizo pia zimetoa sera nafuu husika ili kuhimiza maendeleo ya uzalishaji wa magari madogo. Hapo baadaye, magari madogo si kama tu hayatakumbwa na vikwazo vya sheria za usalama barabarani, bali wateja watapata nafuu katika ulipaji kodi na malipo yanayotozwa kwenye barabara za kasi. Kwa sasa nchini China mauzo ya magari madogo yanachukua 20% hivi ya jumla ya idadi ya magari yanayouzwa, ambayo ni kidogo sana ikilinganishwa na wastani wa 70% kwa nchi za Ulaya. Katika upande huo, maendeleo ya uzalishaji wa magari madogo bado una nafasi kubwa nchini China. Bw. Rong Huikang wa Jumuiya ya viwanda vya magari ya China amesema, mauzo ya magari madogo yatachukua nafasi kubwa zaidi mwaka huu kwenye soko la magari nchini. Alisema, "Kwa mfano, magari aina ya Xiali ambayo yaliuzwa sana mwaka jana. Baada ya marekebisho kwa mara kadhaa, aina kadhaa za magari madogo ya Xiali zimekuwa chini ya cc 1000. Magari mengine madogo kama ya QQ yanayozalishwa na kampuni ya Chery, yale ya chini ya cc 800 na cc 1,100 yaliuzwa sana. Huu utakuwa mwelekeo wa China."

Inakadiriwa kwamba mauzo ya magari ya China yatakuwa na ongezeko la 12% mwaka huu, idadi ya magari yatakayouzwa itaweza kuzidi milioni 6.4. Katika mazingira ambayo China imeondoa vikwazo kwa magari madogo madogo, magari madogo yatachukua nafasi kubwa zaidi kwenye soko la magari nchini.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-28