Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC katika nchi 35 unaonesha kuwa, watu wengi wanaona baada ya vita vya Iraq, tishio la ugaidi dhidi ya dunia sio kama tu halijatokomezwa, bali pia limekuwa kubwa zaidi kuliko hapo zamani.
Miongoni mwa nchi zilizofanyiwa uchunguzi huo, ni nchi mbili tu ambazo zaidi ya nusu ya idadi ya watu waliohojiwa wanaona kuwa dunia imekuwa salama zaidi baada ya vita vya Iraq. Asilimia zaidi ya 60% ya watu waliohojiwa wa nchi nyingine 33 wanaona kuwa vita hivyo vimefanya tishio la ugaidi kuwa kubwa zaidi, ambapo watu wenye maoni tofauti na hayo ni 12% hivi, na 15% ya watu wanaona vita vya Iraq havikuleta mabadiliko yoyote kwa mapambano dhidi ya ugaidi. Katika nchi tatu Marekani, Uingereza na Iraq ambazo zinahusika moja kwa moja na vita vya Iraq, watu wanaoona mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji nguvu zaidi wamefikia 55%, 77% na 75% kwa mbalimbali.
Watu wanafahamu kuwa, Marekani ilitumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kupeleka jeshi lake kuuangusha utawala wa Taliban wa Afghanistan na kupambana na kundi la Al-Qaeda, halafu iliuangusha utawala wa Saddam wa Iraq kwa nguvu ya kijeshi bila idhini ya Umoja wa Mataifa. Jeshi la Marekani pia lilitumia nafasi hiyo kuingia mashariki ya kati, Asia ya kati na kujaribu kurudi Asia ya kusini mashariki. Marekani inasema, "dunia imekuwa salama zaidi" baada ya vita Afghanistan na Iraq, na rais Bush wa Marekani alishinda katika uchaguzi mkuu na kuendelea na wadhifa wa urais kwa kipindi kingine kutokana na harakati za kupambana na ugaidi.
Lakini hivi sasa baada ya miaka zaidi ya 4 tangu kuanzishwa mapambano dhidi ya ugaidi duniani, watu wanaona tishio la ugaidi dhidi ya dunia limekuwa kubwa zaidi. Watu bado wana wasiwasi na hali nchini Iraq. Vita vya Iraq havijatokomeza ugaidi, kundi la Al-Qaeda linapata wafuasi na wanachama wengi kwa kutumia nafasi hiyo na kuifanya Iraq kuwa uwanja wa mafunzo ya shughuli za kigaidi duniani. Kundi la Al-Qaeda na makundi mengine yenye msimamo mkali wa kisiasa yanayohusiana nalo au kufanana nalo, bado yanafanya shughuli zao na kuzusha matukio ya umwagaji damu katika sehemu mbalimbali duniani. Baadhi ya vyombo vya habari vya Ulaya vinafika hadi hata kuona kutokea hali mbali zaidi tangu kuanzishwa mapambano dhidi ya ugaidi.
Ni dhahiri kuwa kuna vyanzo vingi kwa kupamba moto kwa shughuli za ugaidi, lakini ukweli ni kwamba moja ya vyanzo muhimu ni sera ya umwamba wa Marekani katika miaka mingi iliyopita. Marekani imekuwa ikiipendelea Israel katika mashariki ya kati, jambo ambalo limesababisha manug'uniko kutoka kwa nchi za kiarabu. Baada ya kutokea kwa tukio la "tarehe 11 Septemba", Marekani ikitumia kisingizio cha kupambana na ugaidi inaelekeza mkuki wake dhidi ya nchi za kiislamu, ikidai kubadilisha nchi za kiarabu kwa "demokrasia" ya Marekani. Katika mapambano dhidi ya ugaidi Marekani inatumia "vigezo viwili" na kubuni maana ya mapambano dhidi ya ugaidi kwa kufuata upendeleo wake yenyewe, na kuyafanya mapambano hayo kuwa chombo cha kubagua itikadi na taratibu za kisiasa zinazotofautiana na Marekani, ili kuendeleza sera zake za kuwa kiongozi wa dunia.
Kwa upande mwingine gharama ya vita dhidi ya ugaidi imefanya watu wengi zaidi wa Marekani kuona kuwa ni mzigo mzito. Idadi ya vifo na majeruhi ya askari wa Marekani katika nchi za Iraq na Afghanistan kuongezeka kwa mfululizo; Marekani imetumia dola za kimarekani karibu bilioni 400 katika miaka zaidi ya 4 iliyopita; nchi nyingi za Umoja wa Ulaya ambazo ni washirika wa Marekani, zinakuwa na msimamo wa kuishuku vita ya Iraq na kutofanya ushirikiano kuhusu vita vya Iraq. Mambo hayo yameifanya serikali ya Marekani ijiingize katika shida kwenye suala la mapambano dhidi ya ugaidi.
Hivi karibuni Rais George Bush wa Marekani alisema, ushirikiano wa kimataifa ni kitu muhimu cha ushindi katika vita vya kupambana na ugaidi. Tamko lake hilo ni sahihi, lakini kupata ushirikiano wa kimataifa kutategemea vitendo halisi vya Marekani.
Idhaa ya Kiswahili 2006-03-01
|