Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-01 20:29:35    
Wachina watilia maanani mlo kamili kwa ajili ya afya bora

cri

Katika miaka ya karibuni wakazi wa mijini nchini China wanapokula katika mikahawa au nyumbani, vyakula huwa vinono vya aina mbalimbali, lakini licha ya vyakula hivyo pia wameanza kupenda vyakula vingine kama viazi vitamu na mahindi. Hali hiyo inaonesha kuwa mawazo kuhusu uchaguzi wa aina za vyakula yanabadilika, na wanatilia maanani zaidi kula mlo kamili ili wawe na afya bora zaidi.

Bwana Dong Liangji ni mfanyakazi katika shirika moja mjini Beijing, ana umri wa miaka 30 hivi. Katika siku za karibuni kila Jumamosi huwa anakwenda kwenye shule inayotoa mafunzo kuhusu lishe iliyoandaliwa na Shirikisho la Elimu ya Lishe la China, anaona kwamba lishe ni kitu muhimu kwa afya na ni msingi wa mwili wa kufanya kazi vizuri. Alisema,

"Lishe ni kitu muhimu kinachohusiana moja kwa moja na afya zetu, mtu akitaka kuwa na maisha bora na kufanikiwa katika jitihada zake na sharti awe na afya njema, lakini mtu anaweza vipi kuhakikisha afya bora? Naona cha msingi ni kuwa na uwiano wa lishe."

Mwishoni mwa wiki iliyopita, waandishi wetu walifika kwenye shule aliyoelezea Bw. Dong. Ukumbi huo ulikuwa umejaa watu vijana kwa wazee. Mkuu wa shule hiyo alieleza kuwa wakati shule ilipofunguliwa miaka miwili iliyopita watu waliokuwa wanashiriki kwenye masomo walikuwa kumi kadhaa tu, lakini sasa wamekuwa mia kadhaa, kwa jumla watu waliowahi kushiriki kwenye masomo ya shule hiyo wamefikia elfu kumi.

Bi. Jia Nengfang aliyewahi kushiriki kwa mara zaidi ya kumi alisema, lengo lake la kushiriki kwenye masomo hayo ni kwa ajili ya kumsaidia bwana wake aliyenenepa kubadilisha mwenendo wa chakula. Alisema zamani kutokana na kutofahamu elimu ya uwiano wa lishe, chakula kilikuwa cha aina za nyama, hali hiyo ikiwa ni pamoja na kukaa ofisini bila kufanya mazoezi, mafuta yalijaa mwilini haraka. Sasa anamshawishi bwana wake apunguze chakula cha nyama na kula zaidi mboga na chakula kilichopikwa kwa maziwa. Baada ya marekebisho ya aina za chakula bwana wake amepungua uzito, na anajiona mwepesi.

Karo ya shule kwa kila muhula ni yuan 3,900, ambayo ni kiasi cha mshahara wa mfanyakazi wa ngazi ya juu katika mashirika ya miji mikubwa, lakini Bi. Jia Nengfang mwenye umri wa miaka 30 hivi alisema haoni hasara ya kulipa karo hiyo. Alisema,

"Sioni hasara, katika miaka unapokuwa kijana unalipa gharama hiyo kwa kujipatia elimu ya kufahamu namna ya kuishi kiafya, lakini hakika utaokoa malipo mengi ya kulipa matibabu baada ya kuzeeka kwa sababu ya kuwa na afya."

Wataalamu wanasema kuwa, kutokana na maisha bora, watu hupata lishe kupita kiasi kutokana na chakula bora na watu wengi wanapata ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine, kwa hiyo watu wameanza kutilia maanani uwiano wa lishe. Bi. Sun Shuxia anayeshughulikia lishe katika Kamati ya Hifadhi ya Afya ya China alisema,

"Hapo zamani, kutokana na umaskini watu waliokosa chakula cha kutosha hawakuzingatia lishe, lakini sasa kutokana na kuwa na maisha bora, ufahamu wa namna ya kukinga magonjwa umekuwa mkubwa, watu wameanza kutilia maanani namna ya kujipatia afya."

Afya bora kwa lishe imekuwa aina ya kazi mpya katika jamii nchini China. Kati ya kazi mpya za aina kumi zilizotangazwa na serikali, mojawapo ni kazi ya "utaalamu wa lishe", pamoja na kazi hiyo, mikahawa ya lishe na idara za kutoa mashauri ya afya pia zimejitokeza. Katika kituo cha kufanya mazoezi ya afya kuna mkahawa wa lishe. Ndani ya madirisha ya maonesho kuna vyakula vya aina mbalimbali kwa seti, ambavyo vyote vilichanganywa na wataalamu wa lishe, kati ya vyakula hivyo kuna chakula cha Kichina, chakula cha Kijapan na chakula cha Kimagharibi. Mtaalamu wa lishe alionesha seti moja ya chakula akisema,

"Hiki ni chakula cha kuimarisha misuli, jimbini yake inatia joto, hii ni saladi ya mboga, hii ni steki ya nyama ya ng'ombe ambayo inatia protini, na hii ni sandwichi. Seti hiyo ya chakula inasaidia kupunguza uzito na kuimarisha misuli."

Kutokana na shughuli nyingi wafanyakazi wa ngazi ya juu wa mashirika kila wakati wanafanya kwa kutumia kompyuta, wanahitaji zaidi chakula maalumu kilichochanganywa kisayansi virutubisho.

Katika mji wa Taiyuan uliopo kaskazini mwa China kuna shirika moja ambalo linatoa vyakula maalumu kwa ajili ya wafanyakazi wa ngazi ya juu wa mashirika. Shirika hilo linatoa vyakula kwa mujibu wa hali ya afya ya wafanyakazi hao. Mkuu wa shirika hilo alisema,

"Kwanza tunafanya uchunguzi kuhusu hali yao ya chakula, tunaomba wafanyakazi wajaze fomu kuhusu mazoea ya chakula chao, kisha tunafanya utafiti na kurekebisha chakula chao kwa chakula chetu tunachowaandalia."

Hivi leo watu wengi wanazingatia mchanganyiko wa aina za vyakula. Hapo zamani vyakula kama viazi vitamu na mahindi vilipuuzwa, lakini sasa vinafuatiliwa. Kwani watu wamefahamu kuwa vyakula hivi vinatia afya. "Chakula bora asubuhi, chakula cha kutosha mchana na chakula kidogo jioni" umekuwa usemi unaojulikana kwa wote.

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza jinsi Wachina wanavyozingatia uwiano wa lishe katika miaka ya karibuni. Kipindi hiki kinaishia hapa. Kwaherini.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-01