Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-02 17:58:10    
Mapambano dhidi ya mihadarati duniani yakabiliwa na changamoto kubwa

cri

Taarifa iliyotolewa na mamlaka ya udhibiti wa mihadarati duniani tarehe 1 mwezi Machi huko Geneva kuhusu mihadarati duniani mwaka 2005 inasema, ingawa jumuiya ya kimataifa imepata maendeleo katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwasaka wahalifu wanaohusika, lakini mapambano dhidi ya mihadarati duniani bado yanakabiliwa na changamoto kubwa.

Kwenye bara la Asia, Afghanistan ni nchi muhimu inayozalisha kasumba, ambayo ilichukua 87% ya jumla ya zao hilo lililolimwa duniani mwaka 2005. Heroin iliyozalishwa kiharamu nchini Afghanistan iliongezeka kwa mfululizo toka miaka ya 90 ya karne iliyopita. Suala la uzalishaji na matumizi ya mihadarati limekuwa kikwazo kikubwa kwa nchi hiyo kuelekea kwenye hali ya utulivu.

Biashara ya magendo na matumizi ya mihadarati katika sehemu ya Asia ya kusini mashariki vimekuwa suala lenye utata mwingi na kuwahusisha watu wa hali mbalimbali, hususan katika nchi za Bangladesh, India na Nepal ambazo usimamizi mbaya kuhusu dawa za kulevya umechangia watu wa hali mbalimbali kutumia dawa hizo. Aidha, katika miaka ya karibuni watu wanaotumia dawa ya kulevya nchini India wameanza kujidunga sindano ya dawa za kulevya badala ya kuvuta unga wa dawa hizo, njia ambayo imekuwa moja ya vyanzo vya kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Katika bara la Amerika Kusini, kwenye nchi za Colombia, Bolivia na Peru, mashamba yanayolimwa zao la mihadarati yameanza kuongezeka kwa 3% mwaka 2004 kuliko mwaka uliotangulia baada ya kupungua kwa miaka mitatu mfululizo, na kuenea hadi kwenye maeneo mapya. Makadirio yaliyofanywa kutokana na maeneo ya mashamba ya zao la mihadarati, uzalishaji wa cocaine mwaka 2004 ungeweza kufikia tani 687 ikiwa ni ongezeko la 2% kuliko mwaka uliotangulia. Kutokana na kuwa serikali ya Colombia imeimarisha utekelezaji wa sheria dhidi ya mihadarati, kilimo cha mihadarati kinahamia Bolivia na Peru kutoka nchi hiyo. Jambo linalowafanya watu wawe na wasiwasi mkubwa zaidi, ni jitihada ya kupiga marufuku kilimo cha zao la mihadarati imeleta mgogoro katika mambo ya siasa na jamii ya baadhi ya nchi za Amerika ya kusini, na mgogoro huo unapunguza uwezo wa serikali za nchi hizo kupiga marufuku matumizi ya mihadarati.

Kiasi kikubwa cha cocaine inayozalishwa katika nchi za Amerika ya kusini, kinasafirishwa kwenda Marekani na nchi za Ulaya. Serikali za Marekani na nchi za Ulaya zikipitia mikataba ya pande mbili au ya pande nyingi zinatoa misaada ikiwemo fedha kwa nchi hizo katika shughuli husika za utekelezaji wa sheria, uchunguzi wa kesi za jinai na uendeshaji wa mashitaka. Taarifa hiyo inasema, ingawa katika miaka ya karibuni, nchi za Amerika ya kusini zimepiga hatua muhimu katika upigaji marufuku matumizi ya madawa ya kulevya na kuwasaka wahalifu husika, lakini maendeleo hayo bado hayajaweza kupunguza tatizo cocaine duniani.

Taarifa imekadiria kuwa, hivi sasa idadi ya watu wanaotumia cocaine nchini Marekani ni milioni 2 na laki 3, lakini idadi ya vijana wanaotumia cocaine nchini Marekani inaendelea kupungua. Nchini Marekani watu wanaotumia heroin ni kiasi cha 0.1% ya jumla ya idadi ya watu wake.

Kuhusu Ulaya, taarifa hiyo ilisema, bangi na Ecstasy ni aina mbili za dawa za kulevya zinazotumika sana katika nchi za Ulaya. Katika nchi za Umoja wa Ulaya, 15% ya wanafunzi wenye umri wa miaka 15 wanatumia bangi mara 40 kwa wastani kwa mwaka. Ecstasy zinazotumiwa na nchi za Ulaya zinachukua theluthi moja ya jumla ya Ecstasy zinazotumiwa duniani. Aidha, Ulaya ni chanzo cha Ecstasy zinazotumika katika bara la Amerika na bara la Asia.

Taarifa hiyo inasema, kutokana na matumizi ya dawa za kulevya kuwa na uhusiano mkubwa na umaskini, ukosefu wa ajira na vitendo vya uhalifu, hivyo imependekeza idara husika za nchi mbalimbali zifikirie utatuzi wa suala hilo kwa pamoja ili kuongeza ufanisi.