Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-02 18:16:19    
Waziri mstaafu anayejikita katika shughuli za kilimo

cri

Mkoa wa Hainan upo kusini ya China. Katika mkoa huo, yupo mzee mmoja ambaye alistaafu miaka mitatu iliyopita, akaamua kuaga maisha ya mjini na kurudi katika maskani yake kijijini. Kurudi kwake kulileta mabadiliko makubwa katika kijiji hicho maskini, na wanavijiji wenzake wakaanza kuwa na maisha bora. Mzee huyo ni naibu mkuu wa zamani wa mkoa wa Hainan Bw. Chen Suhou.

Kijiji cha Songmei kipo mbali na miji, ni maskani ya Bw. Chen Suhou. Mzee huyo anapenda kutembeatembea kijijini akiwa na mkoba wenye chupa ya maji uliotengenezwa kwa kitambaa. Mbali na kuvaa mavazi safi, Bw. Chen anaonekana hana tofauti na wakulima wenzake. Mbele ya nyumba yake amepanda mboga za aina kadhaa kama wanavyofanya wakulima wengine wa kijiji hicho chenye familia 170.

Mkulima huyo wa kawaida aliwahi kushika wadhifa wa naibu mkuu wa mkoa wa Hainan kwa miaka 7 akishughulikia mambo ya kilimo. Alistaafu mwaka 2003. Bw. Chen Suhou na mke wake walirudi katika maskani yao na wakawa wakulima. Akizungumzia uamuzi huo, Bw. Chen alisema (sauti 1) "Kuishi mjini au kijijini? Huu ni uamuzi mkubwa katika maisha yangu. Nilikuwa nimeshughulikia mambo ya wakulima na kilimo kwa miaka mingi katika kazi yangu, ninawapenda wakulima. Kwa hiyo tunaona ni rahisi kujenga upendo na wakulima tukirudi kijijini."

Hivi sasa nchini China kuna maofisa wa ngazi ya mawaziri wapatao 1,500 ambao wamestaafu. Wengi wanaishi katika miji, wanapewa huduma nzuri ya afya na wanapata manufaa mbalimbali. Lakini Bw. Chen Suhou ni mtu tofauti kidogo na maofisa hao.

Mwanzoni aliamua kurudi maskani na kuwa mkulima akiwa na lengo la kupitisha siku za uzee katika hali ya utulivu. Aliporudi maskani yake, alikuta kijiji cha Songmei chenye hali duni ya kimaendeleo. Wanavijiji walitegemea kilimo cha mpunga na mapato ya wastani yalikuwa Renmnbi Yuan elfu moja tu kwa mwaka, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani 120. Kutokana na maelezo ya wanavijiji wenyewe, kijiji hicho ni maskini kiasi kwamba wasichana wa nje hawakutaka kuolewa na wavulana wenyeji wa kijiji hicho.

(sauti 2) "Umaskini ulikuwa bado haujaondolewa. Nilikuwa naibu mkuu wa mkoa huo wa kushughulikia mambo ya kilimo, na ofisi ya kupambana na umaskini ilikuwa chini ya usimamizi wangu. Kwa hiyo ninawajibika. Ninapaswa kuwasaidia wanavijiji wenzangu kutafuta mbinu za kuondoa umaskini na kupata pesa, na kuwasaidia kutatua matatizo yao."

Mzee Chen aliona chanzo cha umaskini ni wakulima wa kijiji hicho ni kujishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula tu, vikiwemo viazi vitamu na mpunga, mazao hayo yasiyo na thamani kubwa hayaleti pesa nyingi hata kama wakipata mavuno makubwa. Wakati huo huo wakulima wa vijiji jirani wamekuwa wakipata faida kubwa kutokana na kilimo cha mananazi. Ingawa wakulima wa kijiji cha Songmei waliwahi kupanda hekta kadhaa za mananasi, lakini hawakupata mavuno hata kidogo. Nibu mkuu wa kata ya Nanbao ambapo kipo kijiji cha Songmei Bw. Wang Ru alichambua hali hiyo akisema, wakulima walikuwa wanang'ng'ania mtizamo wa kizamani wa kuthamini mazao ya chakula na kupuuza mazao ya biashara.

Bw. Chen Suhou alifanya jitihada kubwa ili kubadilisha mtizamo huo wa wanakijiji wenzake. Hatua ya kwanza ilikuwa kuwapelekea wakulima kutembelea makao makuu ya kupanda mananasi na kujifunza. Mkulima wa kijiji hicho Bw. Lin Maoqing alisema, (sauti 3) "Kutokana na maandalizi ya Mzee Chen, tulitembelea makao makuu ya kupanda minanasi yaliyopo kwenye wilaya na miji mingine na kupewa mafunzo. Baada ya kurudi nyumbani, kamati ya kijiji chetu ilituhamasisha kuanzisha mashamba ya mfano ya kupanda mananasi."

Baadaye mzee Chen aliwatembelea wanakijiji familia moja baada ya nyingine, akiwashawishi kupanda mananasi. Alifanikiwa kuwashirikisha wakulima wa familia 7 kuanzisha Shirika la mananasi, na mzee Chen alikuwa msaidizi wa shirika hilo bila ya malipo. Mbali na hayo, mzee Chen mwenyewe alikwenda katika chombo cha fedha kuomba mikopo. Mkurugenzi wa chombo cha fedha Bw. Chen Fenzhang alikuwa anasitasita akiwa na wasiwasi kuhusu wakulima kushindwa kurudisha mikopo. Ili kupata mikopo Mzee Chen alitoa dhamana kwa sifa yake. Wakulima walikuwa hawana ujuzi, mzee Chen aliwaalika wataalamu wa Taasisi ya sayansi ya kilimo ya mkoa wa Hainan kuwasaidia, na baada ya kupata mavuno alishughulikia kuwasiliana na viwanda vinavyonunua mananasi.

Mwaka mmoja baadaye, wakulima wa familia hizo 7 wa shirika la mananasi walipata jumla ya Renminbi Yuan karibu laki 4, sawa na dola za kimarekani elfu 50. Walilipa mikopo ya Yuan elfu 60 na kuweka akiba ya Yuan zaidi ya laki 3. Mkurugenzi wa chombo cha fedha Bw. Chen Fenzhang alifurahi sana, na yeye mwenyewe aliibandika ubao wa "Kijiji cha Uaminifu" katika mlango wa kamati ya kijiji cha Songmei.

Akizungumzia tukio hilo, mzee Chen Suhou alisema (sauti 4) "Kwa kuwa wakulima wa kijiji hicho waliokopa wote walilipa mikopo kwa wakati, wamejionesha kuwa wao ni waaminifu, kwa hiyo chombo cha fedha kinafurahia kuwapatia mikopo, na ubao huo ni ishara ya uungaji mkono wa chombo cha fedha."

Kutokana na uungaji mkono wa chombo hicho cha fedha, shirika la mananasi lilijiendeleza sana. Hadi mwaka jana, familia zote za kijiji cha Songmei zilipanda mananasi, hali hii ilikifanya kijiji hicho kijulikane kama kijiji cha mananasi. Kwa sababu ya mabadiliko ya mfumo wa kilimo, kijiji hicho ambacho kilikuwa maskini kilianza kupata mapato, wastani wa mapato ya wanakijiji uliongezeka kwa mara moja katika miaka mitatu iliyopita.

Sambamba na kupata faida, mzee Chen Suhou aliwashirikisha wanakijiji wenzake katika kuboresha vifaa vya uzalishaji na mazingira ya kuishi. Walijenga soko, zahanati na kituo cha utamaduni. Wanakijiji wenzake walimsifu sana mzee Chen, wakisema naibu mkuu huyo wa zamani wa mkoa wa Hainan alirudi kijijini na kuwa mkulima, hatua yake hiyo iliwafanya wakulima wenzake waanze kuishi kama wakazi wa mijini.