Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-03 16:52:14    
Nchi za Afrika kuwa sehemu mpya zinazowavutia watalii kutoka China

cri

Kabla ya kuwadia kwa sikukuu ya Spring ya mwaka huu, taarifa zilizotolewa na mashirika ya utalii ya Beijing zilisema kuwa, nafasi zote za vikundi vya watalii wa China waliotaka kwenda kutalii kwenye nchi za Afrika katika kipindi cha kusherehekea sikukuu ya Spring zilikuwa zimejaa.

Mhusika wa shirika la kimataifa la utalii la China Bwana Lin Bo alisema, hivi sasa idadi ya watalii wa China wanaokwenda kutalii kwenye nchi za Afrika bado ni ndogo, yaani haizidi asilimia 5 ya idadi yote ya watalii wa China wanaokwenda nchi za nje kutalii. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, idadi hiyo inaongezeka mwaka hadi mwaka, soko la utalii la Afrika lina uwezo mkubwa wa kuwavutia watalii wa China.

Takwimu zilizotolewa na idara ya usimamizi ya mipaka ya wizara ya usalama wa umma ya China zinaonesha kuwa, katika mwaka 2005 idadi ya watu wa China waliokwenda kwenye nchi za Afrika ilifikia laki moja na elfu 10, ikiwa imeongezeka kwa mara moja na zaidi kuliko mwaka uliotangulia. Hivi sasa idadi ya nchi za Afrika zilizoorodheshwa kuwapokea watalii wa China imefikia 16.

Bi. Liu aliyewahi kutalii katika nchi za Afrika alisema, kutalii kwenye nchi za Afrika kuna umaalum wa kipekee, kwa mfano Kenya ina makabila mengi ambayo hadi leo yamedumisha hali ya kiasili. Katika hoteli ya toptrees ya Kenya, Bi. Liu na watalii wenzake walikaa kwenye miti, na kuwatazama wanyama pori waliokuwa wanazungukazunguka karibuni.

Bi. Liu aliongeza kuwa zamani watu wa China walikuwa wanafahamu kidogo sana kuhusu mambo ya Afrika, wengi wao walipozungumzia nchi za Afrika, huzihusisha nchi za Afrika pamoja na joto, magonjwa na vurugu, lakini baada ya kutembelea Afrika wamegundua kuwa, kama nchi na mabara mengine duniani, nchi za Afrika zina ustaarabu wa kale na wakazi wanaofanya kazi kwa bidii.

Waraka wa sera za China kwa Afrika uliotolewa na serikali ya China tarehe 12 mwezi Januari umesisitiza kuwa, China itaongeza nguvu kuwashawishi raia wake kutalii katika nchi za Afrika, na kuziruhusu nchi nyingi zaidi za Afrika ziweze kuwapokea watalii wa China.

Bw. Lin Bo alisema hivi sasa Misri, Afrika ya kusini na Kenya ni nchi za Afrika zilizowapokea watalii wengi zaidi wa China kuliko nchi nyingine za Afrika, katika siku zijazo mashirika ya utalii ya China yatafungua njia mpya katika nchi nyingine za Afrika. Nchi mbalimbali za Afrika zinafuatilia sana soko la utalii la China, idara za utalii za Kenya na Zimbabwe zimewahi kuwaalika kwa mara nyingi wahusika wa utalii wa China kufanya ukaguzi nchini kwao.

Bw. Lin Bo alifahamisha kuwa, kuomba visa vya utalii katika balozi za nchi za Afrika zilizoko nchini China ni rahisi, kwa kawaida inachukua siku saba.

Waziri wa utalii wa Kenya Bwana Moris Delonzo alipohojiwa na mwandishi wa habari wa China alisema, katika miaka ya karibuni, idadi ya watalii wa China waliokwenda Kenya kutalii imeongezeka mwaka hadi mwaka, kutoka 2000 ya mwaka 2002 hadi 9000 ya mwaka 2004. Baada ya Kenya kuruhusiwa kuwa nchi inayopokea watalii kutoka China mwaka 2004, mwaka 2005 idadi ya watalii wa China kufika nchini Kenya kutalii iliongezeka haraka na kufikia elfu 11.

Utalii unatoa mchango mkubwa katika uchumi wa Kenya, ambao unachukua asilimia 12.65 ya thamani ya jumla ya uzalishaji nchini humo, umetoa ajira za moja kwa moja kwa watu laki moja na elfu 38, na watu wengine laki tatu na elfu 60 wanafanya kazi zinazohusiana na sekta ya utalii. Bw. Delonzo alisema serikali ya China siku sote inawahimiza raia wake kutalii katika nchi za Afrika, na wizara ya utalii ya Kenya imeifanya China kuwa soko jipya la watalii, na imechukua hatua nyingi za kuwavutia watalii wa China. Kwa mfano kuanzisha mtandao wa Internet kuhusu utalii wa Kenya kwa lugha ya kichina, kuandaa shughuli za aina mbalimbali za kuwavutia watalii wa China, shirika la ndege la Kenya mwaka jana lilianza kufanya safari za moja kwa moja hadi mji wa Guangzhou, kusini mwa China ili kuwafanya watalii wa China wafike Kenya kwa urahisi zaidi. Isitoshe serikali ya Kenya imejitahidi kuboresha miundo mbinu ya utalii ili kuwapatia watalii wa China huduma nzuri zaidi.

Naibu meneja wa shirika lingine la utalii la China Bi. Zheng alisema kuwa, miundo mbinu ya utalii ya nchi za Afrika ni mizuri, kuna hoteli nyingi nzuri na huduma bora. Alisema gharama kubwa za kutalii katika nchi za Afrika ni sababu muhimu inayokwamisha kuongezeka haraka kwa watalii wa China wanaokwenda nchi za Afrika. Sasa mashirika ya utalii ya China yameanza kushirikiana na mashirika ya usafiri ya nchi mbalimbali ili kupungua gharama za utalii za kwenda katika nchi za Afrika.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-03