Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-06 16:11:47    
Tamasha kubwa kwenye maskani ya ukuta mkuu wakati wa michezo ya Olimpiki ya Beijing 2008

cri

Mwaka 2008 michezo ya 29 ya Olimpiki itafanyika hapa Beijing, China, katika kipindi hiki cha Safari nchini China, kuanzia sasa kila mwezi tutawaletea maelezo yanayohusika na michezo hiyo. Na leo tunawaletea maelezo kuhusu Tamasha kubwa kwenye maskani ya ukuta mkuu.

Kijana mwenye umri wa miaka 22 anayeitwa Kogaito Yoshiki ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Waseda cha Japan, akibeba mkoba wake wa kupanda mlima na kamera kifuani alikuja Beijing kutalii. Katika shirika moja la utalii la vijana mjini Beijing alizungumzia mpango wake wa mwaka 2008 na mwandishi wetu wa habari akisema:

Nitafanya juhudi kubwa kupata nafasi ya kuja Beijing kutazama michezo ya Olimpiki, ambapo nataka kula bata wa kuokwa, nataka kutazama mchezo wa mpira wa miguu, na pia nataka kupanda ukuta mkuu.

Kama matumaini hayo ya kijana huyo wa Japan yataweza kutimizwa, yeye atakuwa mmoja kati ya watazamaji laki 2.6 wa michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008, ambapo akiwa pamoja na wachezaji wa michezo ya Olimpiki, maofisa na watu wengine kutoka nchi za nje, wakati wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, Beijing itawapokea watalii kutoka nchi za nje wapatao laki 6 hivi.

Kijana huyo wa Japan Kogaito Yoshiki huenda hajafahamishwa kuwa, mashirika ya utalii ya Beijing yameichukua fursa ya michezo ya Olimpiki ya Beijing kuandaa "Tamasha kubwa kwenye maskani ya ukuta mkuu". Ili kuwapokea watalii kutoka nchi mbalimbali na kuwawezesha kujisikia mvuto wa mashariki kwenye maskani ya ukuta mkuu, watu wanaofanya shughuli za utalii wameanza kufanya maandalizi. Hata shirika lile la utalii la vijana la Beijing lililompokea kijana Kogaito hivi sasa linafanyiwa upanuzi na ukarabati. Meneja wa shirika hilo Bwana Li Bin alisema:

Ili kukaribisha michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, tutapanua shughuli zetu ili kukidhi mahitaji ya watalii kutoka nchi za nje. Hivi sasa hoteli yetu ina vitanda 200, tunapanga kuongeza vitanda na kuvifanya vifikie 400 hadi 500 ifikapo mwaka 2008, na tutaboresha zaidi vifaa na zana ili kukidhi mahitaji ya watalii.

Hivi sasa mahoteli kadha wa kadha yenye nyota mjini Beijing pia yameanza kupambwa upya au kukarabatiwa upya, ama kuboresha vifaa na zana za mahoteli. Kwa kuwa watazamaji wa michezo ya Olimpiki wengi wao watakuja peke yao, hivyo Beijing itafuata ahadi yake ya kuomba kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki, itaongeza mahoteli ya kuwapokea watazamaji wa nchi za nje kufikia zaidi ya 800, pia itaongeza mashirika ya utalii ya vijana na mahoteli ya familia ya muda ili kupunguza matumizi ya watalii.

Mbali na kukamilisha ujenzi wa miundo mbinu ya makazi na mawasiliano, na kuondoa hali wasiwasi ya watalii juu ya huduma kadha wa kadha, Beijing pia itawaandalia watalii njia mbalimbali za utalii ili kuwawezesha watazame michezo ya Olimpiki, na wajionee vivutio vya nchi ya kale ya China. Ofisa mkuu wa ofisi ya uhimizaji wa utalii katika idara ya utalii ya Beijing Bwana Wang Qing akifahamisha mpango wanao waandalia watalii akisema:

Mpango wetu ni kuwa, mbali na kutazama sherehe ya ufunguzi na ya ufungaji wa michezo ya Olimpiki pamoja na michezo ya Olimpiki, watalii pia watatembelea sehemu 6 kubwa ambazo ni urithi wa mali ya utamaduni duniani kama vile ukuta mkuu, Jumba la kale la wafalme, Jumba la Tiantan la kutambika mungu wa mbinguni, na makaburi 13 ya wafalme wa zama za kale za China. Wakati huo huo wataweza kupata nafasi za kwenda kutembelea makazi ya zamani ya Beijing, vichochoro vya Beijing, kwenda kwenye mabustani ya Beijing kujiunga pamoja na wakazi wa Beijing katika kuwatembeza ndege wanaofugwa, kufanya mazoezi ya kujenga mwili, ama kwenda sehemu kadha wa kadha zenye vivutio mjini Beijing, adhuhuri na jioni wataweza kwenda kwenye mikahawa kuonja chakula cha Beijing, kutazama opera ya Beijing, hata usiku wataweza kucheza ngoma ya Yangge mitaani pamoja na wakazi wa Beijing.

Beijing ni mji wenye vivutio vingi vya utalii, mbali na ukuta mkuu, makasri ya kale ya wafalme na sehemu nyingine za urithi wa mali duniani, pia kuna majumba zaidi ya 130 ya makumbusho na sehemu zaidi ya 270 zenye vivutio. Wakati wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, mashirika ya utalii ya Beijing pia yataandaa njia mbalimbali za utalii zinazohusiana na michezo ya Olimpiki, ambapo watalii wataweza kutembelea majumba ya michezo ya Olimpiki, sehemu zenye vivutio, kwenda kwenye magulio yanayojulikana nchini na ng'ambo, mitaa maarufu yenye baa na mikahawa mjini Beijing na sehemu zinazoonesha utamaduni wa kisasa na kadhalika, ambapo watalii wa nchini na ng'ambo watashuhudia utamaduni wa zama za kale pia kuvutiwa na utamaduni wa wakazi wa Beijing wa hivi leo.

Idara ya mawasiliano ya Beijing pia itaagiza mabasi yenye ghorofa ya kufanya utalii mjini. Mabasi ya aina hiyo, ngazi ya juu itakuwa wazi, ili kuwapa urahisi watalii watakapotazama mandhari ya Beijing, na mabasi hayo yataegeshwa kwenye sehemu yaliko mahoteli mbalimbali, sehemu muhimu zenye vivutio vya utalii, na sehemu zilizo karibu na maduka makubwa au klabu za burudani. Kwenye mabasi hayo, kutafungwa mitambo inayojiendesha kuhusu uongozaji wa utalii, watalii wataweza kuchagua lugha na kusikiliza ufafanuzi. Tikiti za mabasi ya aina hiyo zitakuwa za Yuan 200 hivi, mtalii akinunua tikiti hiyo anaweza kupanda mabasi kufanya matembezi bila kujali anapanda mara ngapi katika siku mbili.

Mbali na kufanya matembezi mjini Beijing na sehemu zilizoko pembeni mwa Beijing, wakati wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, watalii wa nchi za nje pia wataweza kuchukua nafasi kwenda sehemu nyingine nchini China kutalii. Hivi sasa mashirika ya utalii yanayohusika yameanza kufanya majaribio ya kuandaa mipango. Meneja wa Shirika kuu la utalii wa kimataifa la China Bwana Zhao Xin amesema:

Mwaka huu shirika letu limeanzisha njia za mabasi kufanya utalii nchini China, watalii wanaweza kuagiza tikiti kwenye tovuti yetu, njia hizo ni za kudumu, watalii wanaweza kuchagua njia ya kufunga safari kutoka Beijing na kuelekea Shanghai, au njia ya kutoka Beijing hadi Xian, kutoka Beijing hadi Guilin, ama kutoka Beijing hadi Guangzhou. Njia hizo za utalii pia zitawahudumia watalii wa nchi za nje watakaokuja Beijing wakati wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, ambapo tuna waongozaji wa utalii wanaofahamu lugha za kigeni.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-06