Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-07 14:39:23    
Mpango wa maendeleo ya vijiji vipya wa China

cri

Mkoa wa Guizhou ulioko sehemu ya kusini magharibi ya China ni mkoa mkubwa kwa kilimo wenye idadi kubwa ya wakazi wakulima. Kwenye milima mikubwa ya mkoa wa Guizhou kuna kijiji kimoja kinachojulikana kwa jina la "Qiaodi", katika miaka michache iliyopita mazingira ya maisha ya huko yalikuwa mabaya kutokana na wakulima kuwa na mapato madogo na muundo mbinu hafifu. Mwanakijiji Bw. Zhang Deming alimwambia mwandishi wetu wa habari,

"Hata katika mwaka 2000, mazingira ya maisha ya kwetu Qiaodi yalikuwa mabaya, mvua ikinyesha, ilikuwa ni shida kubwa kutoka nyumbani. Kijijini kwetu kuna vijana wengi, ambao walitaka kubadilisha mazingira ya maisha, lakini hawakufaulu. Chini ya uongozi wa serikali, sisi tumekuwa na azma kubwa ya kuishi maisha mazuri."

Bw. Zhang Deming alitaka sana kubadilisha mazingira ya maisha ya kijijini, kuongeza pato la wakulima ni matarajio ya wakulima wa China. Kutokana na athari ya kihistoria na utaratibu wa utawala, katika zaidi ya nusu karne iliyopita, sehemu ya vijiji ya China ilikuwa nyuma kimaendeleo, pato la wakulima pia ni dogo sana ikilinganishwa na pato la wakazi wa mijini. Hali ya wakulima kushindwa kuonana na madaktari kutokana na matatizo ya kiuchumi na kushindwa kuwasomesha watoto wao, inaonekana mara kwa mara.

Nchini China idadi kubwa sana ya watu ni wakulima, suala la sehemu ya vijiji linahusiana na utulivu wa nchi na maendeleo endelevu ya uchumi. Katika miaka ya karibuni, serikali ya China imekuwa ikijaribu kutatua tatizo hilo, ilibuni mikakati kadha wa kadha ya kuunga mkono maendeleo ya sehemu ya vijiji ikiwemo ya kutoa ruzuku moja kwa moja kwa wakulima na kuondoa kodi ya kilimo. Hatua hizo kwa kiwango fulani zimeinua juhudi za uzalishaji mali kwa wakulima na kuongeza pato la wakulima, lakini tofauti kati ya miji na vijiji inaendelea kupanuka kutokana na kasi ya maendeleo ya miji ya China.

Naibu mkurugenzi wa ofisi ya uongozi ya serikali kuu kuhusu mambo ya fedha na uchumi Bw. Chen Xiwen alisema,

"Hivi sasa, tofauti kati ya miji na vijiji nchini inaendelea kupanuka. Wastani wa pato la mkulima lilikuwa Yuan 3,255 mwaka uliopita, wakati pato la mkazi wa mijini lilikuwa Yuan 10,493, tofauti kati yao ni Yuan 7,238, ambayo inaongezeka na wala haipungui. Kwa upande mwingine tofauti ya manufaa waliyopata wakazi wa mijini na wakulima yakiwemo ya elimu, mambo ya afya na utamaduni yalikuwa makubwa zaidi kuliko yale ya mapato."

Ili kutatua tatizo hilo kimsingi, baada ya majadiliano na majaribio yaliyofanyika katika miaka kadha iliyopita, hivi karibuni serikali ya China ilibuni sera za kujenga vijiji vipya. Kutokana na sera hizo, katika muda wa miongo kadhaa, China itatenga fedha nyingi kwa sehemu ya vijiji ili kuboresha miundo mbinu ya sehemu ya vijiji na kufanya wakulima wanufaike sawa na wakazi wa mijini kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii.

Katika miaka michache iliyopita, sera hizo zilitekelezwa kwa majaribio kwenye kijiji cha Qiaodi kilichoko mkoani Guizhou. Serikali ya huko ilitenga Yuan laki kadhaa, kushirikisha wakulima katika ujenzi wa barabara, nyumba, pamoja na majengo ya mambo ya afya na utamaduni, licha ya hayo serikali itatoa ruzuku ya kuwahimiza wakulima kulima mazao ya biashara. Baada ya ujenzi wa miundo mbinu katika miaka kadhaa iliyopita, hivi sasa kijiji cha Qiaodi kimekuwa kijiji kipya chenye huduma kamili na maisha ya neema. Barabara ya kijiji ni nzuri na safi, ambapo nyumba za wakulima zenye ghorofa zimejengwa na kupangwa kwa utaratibu mzuri.

Mwanakijiji bibi Li Fumei alipozungumzia mabadiliko yaliyotokea katika miaka michache iliyopita alisema, hapo awali kiwango cha maisha cha familia yake kilikuwa chini,

"Zamani tulipika chakula kwa kutumia kuni, ambazo tulipaswa kuzikata milimani na ilikuwa ni kazi ngumu, lakini hivi sasa tunatumia gesi, majiko ya umeme au gesi asilia."

Bibi Li alisema, hapo zamani watu wa familia yake na mifugo yao walitumia choo kimoja, hivi sasa si kama tu kimejengwa choo kinachotumiwa na watu, tena waliweka chombo cha maji-moto, hivyo wanaweza kuoga maji moto kama wakazi wa mijini.

Ni dhahiri kuwa mabadiliko yaliyotokea katika kijiji cha Qiaodi hayako katika nyumba na mazingira ya maisha peke yake, pamoja na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya wakulima, mabadiliko makubwa yametokea katika sifa maadili ya watu. Kiongozi wa kijiji cha Qiaodi Bw. Liu Xin alisema, hapo zamani kijijini kulikuwa na wezi wengi kutokana na umaskini na njaa. Wakazi waliona wasiwasi mkubwa wakisema, "roho inadunda tunapotoka nje mchana kwa kuogopa kuibiwa nyumbani, roho pia inadunda tunapotoka nje usiku kwa kuogopa kuporwa njiani, na roho pia inadunda mchana na usiku kwa kuogopa watoto kupotoka. Lakini sasa mambo yamebadilika, katika miaka minne iliyopita halikutokea hata kesi moja ya usalama."

Mwezi Machi mwaka huu, serikali ya China ilitangaza mpango wa 11 wa maendeleo ya uchumi na jamii ya miaka mitano na kiasi cha fedha zitakazotumika katika ujenzi wa vijiji vipya nchini. Fedha zitakazotengwa na serikali hasa zitatumika katika kuboresha miundo mbinu ya sehemu ya vijiji na kuinua kiwango cha sayansi na teknolojia ya kilimo, huduma za mambo ya afya, utibabu, elimu na utamaduni kwa wakulima.

Serikali ya China imetoa wito wa kutaka mashirika ya fedha, kampuni na watu binafsi kuwekeza katika ujenzi wa vijiji vipya vya China ili kuhimiza haki na mapatano ya jamii.

Naibu mkurugenzi wa ofisi ya uongozi ya serikali kuu kuhusu mambo ya fedha Bw. Chen Xiwen alidokeza kuwa, ili kuunga mkono ujenzi wa vijiji vipya, katika siku za baadaye China itatenga fedha nyingi zaidi kwa sehemu ya vijiji. Alisema baada ya ongezeko la kasi la uchumi kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, China imekuwa na uwezo wa fedha na kuimarisha uungaji mkono kwa maendeleo ya kilimo, hivi sasa serikali inaweza kutoa ruzuku kwa kilimo kwa kutumia mapato ya viwanda; kwa upande mwingine sera za serikali ya China za kujenga aina mpya ya vijiji zitakuza uwezo wa ununuzi wa wakulima milioni 900, hatua ambayo itakuza mahitaji ya nchini na kunufaisha maendeleo ya muda mrefu ya uchumi wa China.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-07