Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-07 14:58:05    
Barua 0307

cri
Mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian alasiri ya tarehe 28 Februari huko Nairobi Kenya alihudhuria Mkutano wa CRI na wasikilizaji wake wa 91.9 FM, ambapo Bwana Wang Gengnian alibadilishana maoni na kuzungumza na wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Balozi wa China nchini Kenya na wajumbe wa sekta mbalimbali wa Kenya na wajumbe wa ujumbe wa Radio China kimataifa walihudhuria mkutano huo.

Kwenye mkutano huo mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian aliwapa zawadi wasikilizaji waliopata ushindi katika kujibu maswali kuhusu matangazo ya Radio China kimataifa kwenye wimbi la 91.9 FM huko Nairobi Kenya, akitoa hotuba yenye uchangamfu. Alisema kituo cha FM cha Radio China kimataifa ni mradi wa ushirikiano kati ya serikali za China na Kenya. Baada ya kujengwa kwa kituo hiki, Radio China kimataifa imepata nafasi ya kutoa huduma zenye sifa bora zaidi za matangazo kwa wasikilizaji na marafiki wa Kenya, ili kukidhi mahitaji ya usikivu ya wasikilizaji wetu wengi.

Mkuu Wang alisema kwa kupitia kituo cha FM cha CRI, wasikilizaji wetu wanaweza kuifahamu China kwa wakati na kwa urahisi zaidi, ambapo wanaweza kupata habari kuhusu mawasiliano ya kirafiki na ushirikiano wa dhati kati ya serikali za China na Kenya na wananchi wao, pia wanaweza kufahamishwa mabadiliko mapya yanayotokea katika dunia ya hivi leo na kuelewa utamaduni wa binadamu wa aina mbalimbali katika dunia hii tunayoishi kwa pamoja.

Mkuu Wang alisema kutoa huduma nzuri za matangazo ya vipindi mbalimbali vya habari na burudani ni nia yetu ya kuanzisha kituo hiki cha FM kwenye wimbi la 91.9. Kuandaa vizuri vipindi vyetu si kama tu kunatubidi tuchape kazi zaidi, bali pia kunahitaji uungaji mkono wa wasikilizaji wetu wa Kenya. Si muda mrefu baada ya kuanzishwa rasmi kwa matangazo yetu kwenye wimbi la FM, tumepata wasikilizaji wengi, hii inatutia moyo sana.

Amesema, "tunakutana hapa Nairobi tukiweza kubadilishana maoni moja kwa moja na kujadili namna ya kuandaa vizuri vipindi vyetu. Tutainua siku hadi siku sifa ya vipindi vyetu kutokana na mahitaji ya wasikilizaji wetu wa Kenya, kuongeza habari, kuboresha mtindo wetu wa kuhariri na kutangaza, na tutafanya juhudi kujenga daraja la urafiki kati ya wananchi wa China na Kenya.

Balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli alitoa hotuba kwenye mkutano huo na wasikilizaji wa Radio China kimataifa uliofanyika huko Nairobi Kenya, alisema:

Mimi ni balozi wa China nchini Kenya, pia ni mkazi wa Nairobi, na ni msikilizaji mmoja mtiifu wa Radio China kimataifa. Nikiwa msikilizaji, mimi pia nafuatilia sana vipindi vya radio hiyo. Kabla ya kuanzishwa kwa Kituo cha 91.9 FM cha CRI, Radio China kimataifa kila siku inarusha matangazo ya vipindi vyake kwa saa mbili kwa kupitia shirika la utangazaji la Kenya KBC, wajibu wangu ni kuelewa mambo yanayotangazwa kwenye vipindi hivyo, pia nimepata vitu vingi hata manufaa mengi.

Balozi Guo alisema, "nikiwa mkazi wa Nairobi, naona furaha kubwa, kwani sasa mjini Nairobi kuongezwa kituo kipya cha FM cha Radio China kimataifa ambacho kila siku kinatangaza kwa saa 19 kwa lugha tatu. Kama wajuavyo wote, mjini Nairobi kumekuwepo radio tatu kutoka nchi za nje, yaani BBC, VOA na RFI. Radio hizo tatu ni za nchi mbalimbali, ambazo zote ni za magharibi na zinawakilisha utamaduni wa magharibi. Kituo kipya cha FM cha Radio China kimataifa, tunaweza kusema ni radio inayotangaza utamaduni wa mashariki au tunasema ni mjumbe mmoja wa utamaduni wa mashariki. Nina imani kuwa, nikiwa mkazi wa Kenya, sisi sote tuna matumaini kuwa mjini hapa kutakuwepo utamaduni na ustaarabu wa aina mbalimbali, ili sisi sote tuweze kupata mengi kutoka kwa maingiliano ya utamaduni wa aina mbalimbali.

Balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli alisema, "nikiwa balozi wa China nchini Kenya, nafurahia sana kuanzishwa kwa Kituo cha FM cha Radio China kimataifa hapa Nairobi Kenya, kwani kituo hiki kimekuwa kama daraja moja kati ya wananchi wa China na Kenya katika kuongeza maelewano na kuweka msingi imara zaidi wa urafiki kati ya wananchi wa nchi hizo mbili."

Balozi Guo ameahidi kuwa, ubalozi wa China nchini Kenya utafanya ushirikiano na Radio China kimataifa kama ulivyofanya siku zote, ili kuandaa vizuri kwa pamoja matangazo ya Radio China kimataifa kwenye wimbi la 91.9 FM. Mafanikio ya Radio China kimataifa yanahitaji kutegemea uungaji mkono wa wasikilizaji wetu wa Kenya, ambao wangetoa maoni na mapendekezo ili kuisaidia Radio China kimataifa iandae vizuri zaidi vipindi vyake.

Wasikilizaji wetu wa Kenya zaidi ya 40 walihudhuria mkutano huo, ambapo walipongeza kwa furaha kuzinduliwa rasmi kwa kituo cha 91.9 FM cha CRI huko Nairobi Kenya. Mjumbe wa wasikilizaji hao Bwana Hassan alisema, "wanazishukuru serikali za China na Kenya, hasa Radio China kimataifa ambayo imewajengea wasikilizaji wake daraja la urafiki. Vipindi vya Radio China kimataifa si kama tu viwaletea wasikilizaji wake wa Kenya habari kutoka mashariki ya dunia, na kuwawezesha wajue mengi zaidi kuhusu China, nchi kubwa ya mashariki inayoendelea kwa haraka, bali pia imetuwezesha kupata mafunzo mengi yenye manufaa, na kutuwezesha kupata habari nyingi zaidi na kwa haraka zaidi kuhusu serikali ya China, uchumi na utamaduni wa China na kadhalika. Urafiki kati ya Kenya na China ulianzia miaka 600 iliyopita, wananchi wa nchi hizo mbili ni kama ndugu, na sasa matangazo ya Radio China kimataifa yametufanya tuwe na urafiki wa karibu zaidi".

Katika mkutano huo, wasikilizaji wetu walitoa maoni na mapendekezo mengi kuhusu vipindi vyetu kwenye wimbi la 91.9 FM huko Nairobi Kenya, ambapo wasikilizaji wengi pia walibadilishana maoni na wajumbe wa ujumbe wa Radio China kimataifa waliokwenda Nairobi kuhudhuria sherehe ya kuzinduliwa rasmi kwa Kituo cha 91.9 FM cha Radio China kimataifa juu ya maendeleo ya CRI ya siku zijazo, mkutano huo ulifanyika katika hali motomoto.

Baada ya kuanzishwa kwa matangazo ya Kituo cha 91.9 FM ya Radio China kimataifa huko Nairobi Kenya, wasikilizaji wetu wengi wametuletea barua, ambao wamesema usikivu wa matangazo yetu ni mzuri, na vipindi vyake vinahusu mambo mengi mbalimbali. Sasa tunawaletea mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari aliyeko Nairobi na wasikilizaji wetu.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-07