Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-09 20:37:09    
Maisha ya ajabu ya mwanamke aliyekuwa mtumwa huko Tibet ya zamani

cri

Mama Tshering Ihamo ana umri wa miaka 79, anaishi kwenye makazi yake yaliyopo katika wilaya ya Nedong, kanda ya Lhoka mkoani Tibet. Maisha yake ya kila siku yanaanza kwa kusafisha nyumba yake, kumwagia maji maua na majani aliyopanda katika ua wake na kumlisha mbwa wake. Mzee huyo anaonekana kuwa na afya nzuri, na anapenda kufanya kazi za nyumbani huku akiimba.

Wasikilizaji wapendwa, mkiambiwa kwamba miaka 40 iliyopita kabla ya ukombozi wa Tibet, mama huyo alikuwa ni mtumwa, je, mnaweza kuamini? Na mkiambiwa kuwa, baadaye mama huyo alishika wadhifa wa naibu spika wa Bunge la umma la mkoa unaojiendesha wa Tibet, je mnaweza kuamini?

Bibi Tshering Ihamo alizaliwa mwaka 1926 kwenye zizi la ng'ombe katika wilaya ya Lhongzi ya Tibet. Wazazi wake walikuwa ni watumwa, kwa hiyo mtoto huyo akawa mtumwa wa kuzaliwa. Mchana mama yake alimbeba huku akifanya kazi na usiku familia hiyo ya watu watatu ilikaa ndani ya zizi la ng'ombe nje ya hekalu. Chakula kibaya walichopewa na bwana wao kilikuwa hakitoshi. Kutokana na kusumbuliwa na utapiamlo utotoni mwake, Tshering Ihamo alikuwa mwembamba kupita kiasi. Alipokuwa na umri wa miaka 6, alilazimishwa kufanya kazi kwa bwana wake. Katika lugha ya Kitibet, watumwa hao wanaitwa "Langsheng", maana yake ni kama wanyama wanaofahamu kuongea. Kila siku alisafisha shamba la bwana wake na kuokota kuni milimani, pia alifanya kazi ya kumbeba mtoto mnene wa kiume wa bwana wake. Alipigwa viboko mara kwa mara hata akifanya kosa dogo sana.

Bwana wake alikufa wakati Bibi Tshering Ihamo alipokuwa na umri wa miaka 12. Mjane wa bwana shamba aliwauza wazazi wa Tshering Ihamo kwa watu wengine, na kuhamia na watumwa vijana akiwemo Tshering Ihamo kwenye shamba lingine lililopo umbali wa kilomita 200. Kuanzia hapo msichana huyo na wazazi wake wakatengana daima.

Kila alipogusia tukio hilo, Bibi Tshering Ihamo hakuweza kujizuia kutokwa na machozi. Alisema "Niliondoka maskani yangu nilipokuwa na umri wa miaka 12, sikupata nafasi hata moja ya kukutana na baba na mama. Katika shamba la bwana wetu, mchana nilichunga ng'ombe, na asubuhi na jioni nilikamua maziwa, kuandaa chakula na kutengeneza nyuzi. Nilikuwa na maisha kama mnyama, nilifanya kazi mpaka usiku wa manane, lakini nilipewa chakula kibaya au kuchapwa viboko. Nilikuwa nafanya ibada kwa dhati ya moyo kwa budhaa kila siku, lakini sikupata mwangaza hata kidogo."

Mwaka 1959, serikali ya China ilianza kutekeleza mageuzi ya kidemokrasia mkoani Tibet. Katika mageuzi hayo, mfumo wa utumwa ambao uliendelea kuwepo kwa miaka minane tokea ukombozi wa amani wa Tibet ulitokomezwa. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Bi. Tshering Ihamo aliyekuwa na umri wa miaka 33 alikuwa mtu huru, alipewa mbuzi watatu, ng'ombe mmoja wa maziwa pamoja na shamba lenye ukubwa wa karibu nusu hekta.

Kutokana na maisha magumu aliyoyapitia, Bibi Tshering Ihamo alithamini sana maisha mapya yenye uhuru. Mwaka 1961 alianzisha shirika la kusaidiana la waliokuwa watumwa, ambalo ni shirika la kwanza la namna hii mkoani Tibet. Walijifunza namna ya kuzalisha mazao ya chakula, walikuwa wa kwanza wa kutumia mbegu bora na walishirikiana kuchimba mifereji na kujenga boma.

Kijiji alichoishi kilipokumbwa na mafuriko makubwa, ili kulinda mazao ya chakula, Bibi Tshering Ihamo alitangulia kuingia kwenye maji. Yeye na wenzake walizuia mafuriko kwa kutumia miili yao, hatua hiyo ilihakikisha boma unakarabatiwa. Baada ya maafa hayo, walipata mavuno makubwa. Na tukio hilo lilifanya shirika lake la kusaidiana la wakulima kuwa maarufu nchini China. Hapo baadaye, Bibi Tshering Ihamo alikuja Beijing na kukutana na viongozi wa taifa akiwemo aliyekuwa rais wa China Marehemu Mao Zedong.

Katika miaka ya 70 na 80 ya karne iliyopita, Bibi Tshering Ihamo alichaguliwa kuwa mbunge wa taifa kwa mara mbili mfululizo, na kuteuliwa kuwa naibu spika wa Bunge la umma la mkoa unaojiendesha wa Tibet. Ingawa alishika wadhifa wa naibu katibu wa kamati ya chama, alikuwa anajikubmusha kuwa aliwahi kuwa mtumwa aliyenyanyaswa. Alikuwa mpole na kufuatilia matatizo ya watu wa kawaida, mbali na hayo alishikilia yeye mwenyewe kufanya kazi za nyumbani.

Bibi Tshering Ihamo alistaafu mwaka 1983 akiitikia ombi la kiongozi wa zamani wa China Marehemu Deng Xiaoping la kuwaingiza vijana wenye elimu madarakani.

Mzee Tshering Pedron alifanya kazi pamoja na Bi. Tshering Ihamo, wao pia ni majirani wa miaka mingi. Kwa mtazamo wake, Bi. Tshering Ihamo ni mzee mwenye heshima na ni rafiki yake wa siku nyingi. Ingawa amestaafu miaka 22 iliyopita, lakini anaendelea na kazi yake.

Wasikilizaji wapendwa, mnaosikia ni wimbo alioimba Mzee Tshering Ihamo. Wimbo huo unaoitwa "Hakuna China mpya bila Chama cha kikomunisti" ni wimbo anaoupenda sana kuliko nyimbo nyingine, pia ni wimbo unaopendwa na wazee wengi wa Tibet. Bibi Tshering Ihamo alieleza kuwa, hatasahau ni Chama cha kikomunisti cha China ambacho kilimwokoa kutoka kwenye maisha ya taabu ya utumwa na kumletea maisha mazuri ya karibu miaka 50. Alisema hana masikitiko katika maisha yake bali anataka kutoa mchango zaidi kwa jamii.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-09