Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-09 20:39:12    
Wafugaji wa China watembelea barani Ulaya

cri

Bw. Ilatu mwenye umri wa miaka 37 ni mfugaji wa kabila la Wamongolia, anaishi katika uwanda wa juu wa Erdos, magharibi ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani wa China. Hivi karibuni, Bw. Ilatu na wafungaji wengine 12 walikwenda barani Ulaya kujifunza jinsi wafugaji wa huko wanavyoendesha shughuli za ufugaji.

Bw. Ilatu anafuga mifugo karibu 500. Baada ya kurudi kutoka Ulaya, aliamua kuongeza idadi ya ng'ombe wa maziwa na kupunguza idadi ya mbuzi. Alimwambia mwandishi wa habari wa Radio China Kimataifa kuwa, "Katika nchi nilizotembelea, sekta ya ufugaji inatiliwa maanani na mazao ya mifugo ni miongoni mwa vyakula muhimu kwa wenyeji wa nchi hizo, vile vile wanazingatia kukuza shughuli za uzalishaji wa nyama. Viwanda vya kuchinja mifugo vina vifaa vya kisasa na hali safi. Kwa mfano machinjio ya ng'ombe, kutoka hatua ya mwanzo mpaka ya mwisho, yanawekwa bayana rekodi kuhusu mahala pa kuzaliwa kwa ng'ombe, mtu aliyemchinja pamoja na wakati wa kumchinja. Hatua hizo zinahakikisha sifa ya nyama. Kwa hiyo nchi hizo zinauza nyama nje ya nchi kwa wingi."

Watu wa kabila la Wamongolia wanategemea ufugaji tangu zamani. Lakini hivi sasa wafugaji hao wanakabiliwa na matatizo. Katika ufugaji wa jadi, mifugo ya ng'ombe na mbuzi inachungwa kwenye mbuga mkubwa. Kwa kuwa idadi ya mifugo inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko kukua kwa majani, umetokea ukosefu mkubwa wa majani katika ukanda wa mbuga. Kuchunga mifugo bila kikomo pia kumeharibu sana malisho katika eneo hilo, kwa mfano mbuzi wanakula nyasi pamoja na mizizi. Mbali na hayo, mifugo inatembeatembea kwa kujitafutia chakula, kwa hiyo inakula hadi inashiba, halafu inaacha inatembea tembea na kuwa na njaa tena, hali ambayo inafanya unene wa mifugo hiyo upotee bure.

Ili kukabiliana na hali hiyo, huko Erdos ambako ni maskani ya Bw. Ilatu serikali ilipendekeza mbinu mpya wa kufuga mifugo zizini. Ili waweze kutekeleza mbinu hiyo, wafugaji wanatakiwa kujenga zizi kwa ajili ya mbuzi na ng'ombe, pia inawabidi wapande majani kwa wingi ili kuweka akiba ya malisho.

Bw. Ilatu alikumbusha kuwa, mwanzoni wakati wa utekelezaji wa mbinu hizo, wafugaji walikuwa hawazifurahii, waliona hatua za kujenga zizi na kupanda majani, zitaongeza gharamu za shughuli za ufugaji. Lakini baadaye waligundua kuwa, mashaka yao si ya kweli.

Bw. Suyabalatu ni jirani wa Bw. Ilatu. Wao waliambatana kwenye safari hiyo barani Ulaya. Bw. Suyabalatu alisema "Baada ya kuchukua hatua ya kufuga mifugo zizini, mbuzi jike walikaa katika maskani yenye ujoto. Zamani kila mbuzi jike alikuwa anazaa mtoto mmoja tu kwa mwaka, lakini sasa anaweza kuzaa watoto wawili hata watatu kwa mwaka. Kiasi cha mbuzi wadogo waliozaliwa wanaokufa kinapungua na mbuzi wananenepa. Naona ng'ombe na mbuzi wa sasa ni wa aina bora kuliko siku zilizopita."

Mbinu ya kufuga mifugo zizini inafanya ufugaji ukue kwa kasi katika mji wa Erdos. Hivi sasa kuna familia za wafugaji zaidi ya laki moja katika mji huo, na idadi ya mifugo inakaribia milioni 14. Kutokana na hatua za kuboresha mazingira ya ukanda wa mbuga, mimea katika eneo hilo imekua sana.

Mabadiliko ya mbinu za ufugaji pia yameleta mabadiliko ya mtizamo wa wafugaji, ambao sasa wanazungumzia sana jinsi kupanda majani, jinsi kuzalisha maziwa kwa wingi, jinsi kutengeneza maziwa na mazao ya maziwa, na jinsi kuongeza unene wa ng'ombe na mbuzi.

Ufugaji ni uti wa mgongo wa uchumi katika eneo la Erdos, ambalo linahitaji wafugaji wengi wenye utaalamu na wenye moyo wa uvumbuzi katika juhudi za kuendeleza ufugaji wa kisasa. Kwa hiyo serikali ya mji wa Erdos ilifanya uamuzi wa kuwapeleka wafugaji 100 wanaofuga mifugo mingi zaidi kuliko wengine kwenda nchi za nje kufanya ukaguzi, ili washuhudie ufugaji wa kigeni ulivyo na kuiga uzoefu wao. Serikali inatoa asilimia 70 ya gharama za shughuli za ukaguzi na wafugaji wenyewe wanatoa asilimia 30. Na shughuli hizo zilianza mwaka 2004.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Bw. Ilatu, Bw. Suyabalatu na wafugaji wengine 11 walishiriki kwenye ukaguzi wa kundi la pili. Walitembelea nchi tano za Ulaya zikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji na Luxemburg kwa siku 13, wakifanya ukaguzi katika mashamba ya kisasa ya kufuga ng'ombe na mbuzi, viwanda vya kutengeneza mazao ya mifugo na matumizi ya mashine za ufugaji. Wataalamu wa Ujerumani pia waliwapatia mafunzo ya ufugaji.

Baada ya kurudi nyumbani, mbali na kufanya marekebisho katika mashamba yao ya mifugo, wafugaji hao pia waliwahamasisha jamaa, marafiki na majirani zao kufanya marekebisho katika mashamba yao.

Bw. Saixiyala alikuwa mmoja wa wafugaji waliofanya ukaguzi barani Ulaya, ambapo amejifunza mengi.

"Nina mpango mpya ambao nitautekeleza baada ya kurudi nyumbani. Hatua ya kwanza ni kuboresha mazingira ya kimaumbile, ambayo itasaidia kuongeza mapato ya wafugaji na idadi ya mbuzi. Hatua ya pili ni katika maeneo yenye upungufu wa maji kueneza mbinu ya kufuga mifugo ndani ya zizi, naona hii ni njia pekee ya kukabiliana na upungufu wa maji. Na hatua ya tatu ni kuendeleza ufugaji wa mbuzi wanaozalisha nyama nyingi. Nilivutiwa na mashamba ya kufuga mbuzi wa nyama barani Ulaya. Naona katika mji wetu wa Erdos, pia kuna wafugaji wengi wanaofuga mbuzi wa nyama. Kwa hiyo nitawashirikisha kuendeleza ufugaji wa ng'ombe wa nyama na mbuzi wa nyama."

Wafugaji wa Erdos wamekuwa na upeo mpana zaidi, hali hii inahimiza maendeleo ya ufugaji katika mji huo. Mkuu wa Idara ya kilimo na ufugaji ya Erdos Bw. Ma Dingsuo alisema, hivi sasa mbuga za Erdos zimejaa majani, idadi ya viwanda vya kutengeneza maziwa na nyama inaongezeka na wafugaji wanapata pesa.

"Manufaa ya ziara hizo ni dhahiri. Wafugaji walijifunza kutoka kwa wafugaji wa kigeni mbinu na wazo la ufugaji. Baada ya kurudi nyumbani, walitoa vielelezo na kueneza mbinu za ufugaji miongoni mwa wafugaji wenzao. Matokeo yake ni kama mfugaji mmoja kuwafundisha wafugaji 10 na wafugaji hao 10 kuwafundisha wenzao 100. Hali hii inachangia maendeleo ya uchumi na shughuli za kilimo na ufugaji katika mji huo."

Bw. Ma aliongeza kusema serikali ya Erdos na nchi kadhaa za Ulaya zinazungumzia ushirikiano wa kupeleka wafugaji barani Ulaya kila baada ya kipindi fulani, ili wapatie mafunzo na elimu ya kisasa. Na hatua hiyo inalenga kuinua kiwango cha kilimo na ufugaji cha mji huo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-09