Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-10 20:06:02    
Umoja wa Afrika waitisha mkutano kuhusu kulinda amani ya Darfur

cri

Baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika tarehe 10 huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, liliitisha mkutano wa mawaziri kujadili suala la kukabidhi au la jukumu la kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur, nchini Sudan la Umoja wa Afrika kwa majeshi mengine ya kimataifa.

Eneo la Darfur liko kwenye sehemu ya magharibi ya Sudan. Tokea mwanzoni mwa mwaka 2003, makundi yaliyoanzishwa na wakazi waafrika wa huko yakiwemo "Harakati za ukombozi za Sudan" na "Harakati za haki na usawa" yalianzisha shughuli za kijeshi za kuipinga serikali, ambazo zilisababisha maelfu ya makumi ya watu kupoteza maisha na wakazi milioni zaidi ya 2 kukimbia makazi yao. Kutokana na usuluhishi wa jumuiya ya kimataifa, hususan Umoja wa Afrika, serikali ya Sudan na makundi ya kisilaha yanayoipinga serikali yaliafikiana kwenye mkataba wa kusimamisha mapigano mwezi Aprili mwaka 2004. Mwezi Agosti mwaka huo, jeshi la kwanza la kulinda amani lililopelekwa na Umoja wa Afrika lilifika huko Darfur na kutekeleza jukumu la kulinda amani. Hadi hivi sasa idadi ya askari wa jeshi la Umoja wa Afrika lililoko kwenye sehemu hiyo imezidi 7,000,

Jeshi la Umoja wa Afrika lilifanya kazi muhimu katika usimamizi wa utekelezaji wa mkataba wa usimamishaji mapigano kati ya pande mbili zilizokuwa zikipambana na kulinda usalama wa huko, lakini pia lilikuwa na matatizo mengi. Moja ya matatizo hayo ni shida ya fedha na utoaji huduma ambayo imekwamisha harakati za kulinda amani. Kutokana na kushambuliwa na watu wenye silaha wa huko, jeshi la Umoja wa Afrika lilishindwa hata kulinda usalama wake lenyewe. Hivyo baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika mwanzoni mwa mwaka huu lilitangaza, kikanuni linaunga mkono kukabidhi jukumu la kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur kwa Umoja wa Mataifa baada ya jeshi hilo kumaliza kipindi chake cha kulinda amani huko mwishoni mwa mwezi Machi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alisema, Umoja wa Mataifa unakubali kukabidhiwa jukumu hilo, na sekretarieti ya Umoja wa Mataifa pia imebuni mpango wa kupanga jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa kwenye sehemu ya Darfur nchini Sudan. Marekani inataka sana kupelekwa kwa majeshi ya NATO na Umoja wa Mataifa kwenye sehemu ya Darfur. Katikati ya mwezi uliopita rais Bush alisema, ni bora kuongeza mara dufu idadi ya askari wa majeshi ya kimataifa kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur, na kuruhusu NATO kuingilia moja kwa moja.

Lakini msimamo huo wa Marekani na Umoja wa Mataifa unapingwa vikali na Sudan. Tarehe 22 mwezi uliopita, bunge la Sudan liliitisha mkutano maalumu kujadili suala la upangaji wa majeshi ya kimataifa ya kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur na kuamua, kukataa jaribio lolote la kukabidhi jukumu la kulinda amani la jeshi la Umoja wa Afrika kwa majeshi ya kimataifa yatakayopelekwa na Umoja wa Mataifa, na kukataa nguvu ya nje kuingilia mambo ya ndani ya Sudan kwa visingizio vyovyote. Rais Omar El Bashir wa Sudan alisema, baadhi ya nchi zinajaribu kutimiza malengo yao maalumu kwa kutumia njia ya kupanga majeshi ya kimataifa kwenye sehemu ya Darfur wakati jeshi la Umoja wa Afrika linapokabiliwa na matatizo ya kiuchumi. Jeshi la Sudan limesema limejiandaa kupambana na washambulizi wa nchi za nje. Kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kulinda amani ya Darfur utakaoitishwa na baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika, maelfu ya wakazi wa Khartoum tarehe 8 walifanya maandamano barabarani wakipinga kukabidhi jukumu la kulinda amani ya Darfur kwa majeshi ya Umoja wa Mataifa na kupinga nguvu ya nchi za nje kuingilia mambo ya ndani ya Sudan. Kutokana na kukabiliwa na upinzani wa serikali na watu wa Sudan pamoja na baadhi ya nchi za Afrika, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya pamoja na baadhi ya nchi husika zimekuwa na majadiliano. Vyombo vya habari vinaona, katika hali ambayo jeshi la Umoja wa Afrika limeshindwa hata kulinda usalama wake lenyewe, halitaweza kutekeleza jukumu la kutuliza mapambano ya kisilaha na kulinda amani na usalama wa wakazi.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-10