Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-10 20:44:41    
Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika atazidisha urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika

cri

Balozi wa Congo Brazzaville nchini China Bwana Pierre Passi tarehe 6 kwenye ofisi ya ubalozi wa nchi hiyo nchini China aliwaandalia tafrija mabalozi wa nchi za Afrika nchini China ili kusherehekea kuteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika kwa rais wa nchi hiyo Bwana Denis Sassou Ngueso. Alipohojiwa na mwandishi wa habari wa China alisema, Bwana Ngueso ataendelea kushughulikia kuhimiza maingiliano ya kirafiki na ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China.

Bw. Passi alisema nchi za Afrika na China zina urafiki mzuri wa jadi, Congo Brazzaville na China ni marafiki wa miongo kadhaa. Nchi hizo mbili si kama tu zina msimamo wa aina moja kuhusu mambo mengi ya kimataifa, bali pia zimeimarisha maingiliano na ushirikiano katika maeneo mbalimbali. Congo Brazzaville ni mshirika muhimu wa kibiashara wa China barani Afrika, miradi mingi ya ujenzi wa miundo mbinu ya Congo Brazzaville inajengwa na mashirika ya China. Katika mawasiliano ya utamaduni, Congo Brazzaville kila mwaka inawatuma wanafunzi wengi kuja kusoma nchini China, wasanii wa nchi hizo mbili pia wanatembeleana mara kwa mara.

Bw. Passi alisema akiwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika, Bwana Ngueso ataendelea kuchukua jukumu la kuhimiza maingiliano na ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China. Yeye pia ametilia maanani mkutano wa kwanza wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika unaotazamiwa kufanyika mwaka huu mjini Beijing, akiona kuwa, mkutano huo bila shaka utaleta fursa nyingi zaidi za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili za China na Congo Brazzaville na nchi nyingine za Afrika.

Zaidi ya hayo, Bw. Passi alisisitiza kuwa, kuhusu suala la Taiwan, serikali ya Congo Brazzaville siku zote inashikilia sera ya kuwepo kwa China moja, na inalaani vikali hatua ya Bw. Chen Shuibian kukomesha kamati ya muungano wa taifa na mwongozo wa muungano wa taifa akiona kuwa, vitendo vya Chen Shuibian vya kuifanya Taiwan ijitenge na China vitaleta vurugu katika sehemu ya Asia na Pasifiki hasa kwa kando mbili za mlango wa bahari Taiwan.

Kwenye risala yake aliyotoa kwenye tafrija hiyo, Bwana Passi alizitaka nchi za Afrika ziungane na kushirikiana ili kuleta amani na maendeleo kwa bara zima la Afrika.

Bw. Passi alisema mgogoro wa Darfur wa Sudan, mgogoro wa Cote d'Ivoire na matukio mengine ya Afrika yameonesha kuwa, nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto tatu za usalama, umaskini na utulivu wa kisiasa. Katika kipindi chake cha uwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Bw. Ngueso atachukua hatua mwafaka kuleta amani na utulivu barani Afrika.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-10