Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-13 15:17:01    
Mwigizaji filamu Tao Hong

cri

Mwigizaji wa filamu Tao Hong alianza kujulikana kwa watazamaji wa filamu wa China kutokana na filamu yake ya "Maisha ya Binti Mfalme".

Filamu ya "Maisha ya Binti Mfalme" inasimulia maisha ya binti mfalme Bao Ling wa Enzi ya Qing ambayo ni enzi ya mwisho ya kifalme nchini China, yalivyobadilika kutoka maisha ya furaha na starehe hadi kuwa na maisha ya kiraia kabisa. Katika filamu hiyo, Tao Hong aliigiza kama binti huyo toka alipokuwa na umri wa miaka 10 hadi zaidi ya miaka 30, uigizaji wake hodari unasifiwa sana na watazamaji.

Tao Hong ana umri wa miaka 35, alizaliwa katika mji wa Chongqing, kusini magharibi mwa China. Katika miaka alipokuwa mtoto alipenda sana kucheza na kuimba, watu walimsifu wakisema kuwa "mtoto huyo hakika baadaye atakuwa mwigizaji hodari." Alipokuwa na umri wa miaka 11 alijiunga na shule ya sanaa na kujifunza kucheza dansi kwa miaka minane, baadaye alijiunga na chuo kikuu cha tamthilia. Mwaka 1998 Tao Hong kwa mara ya kwanza maishani mwake alipata tuzo ya waigizaji wa kike kutokana na mchezo wa televisheni wa "Maisha Yangu kando ya Mto", kisha alikuwa mwigizaji wa mchezo wa televisheni wa "Pango la Wahalifu" akiigiza mke wa kiongozi wa kundi la wahalifu, ambaye ni mwanamke mwenye ujanja na hila. Uigizaji wake katika mchezo huo ulimpatia sifa nyingi. Lakini kama walivyokuwa waigizaji wengine wa kike, kwamba watizamaji walikuwa hawaoni kama uhodari wake wa uigizaji unatokana na ustadi wake bali ni asili yake mwenyewe, mpaka alipocheza filamu ya "Bosi wa Mkahawa Mdogo".

Filamu ya "Bosi wa Mkahawa Mdogo" inaeleza maisha ya bosi huyo jinsi yalivyokuwa magumu na yenye matuko mengi. Katika filamu hiyo, aliigiza vizuri kama mwanamke mmoja aliyekuwa mkali na mwenye juhudi, na kuonesha vilivyo mwanamke huyo alivyopambana na shida nyingi za maisha na kuvumilia kwa ajili ya utiifu wa mapenzi. Alipojikumbusha alivyocheza katika filamu hiyo alisema, "Baada ya kusoma mpangilio wa maonesho ya filamu, nilifahamu kwamba nitacheza katika kila onesho, au kwa maneno mengine, kiasi cha ufanisi wa filamu hiyo kilinitegemea mimi nitakavyocheza na waigizaji wengine wote ni wasaidizi tu wa uigizaji wangu, kwa hiyo nilikabiliwa na changamoto kubwa. Kutokana na hali hiyo, miezi minne kabla ya filamu hiyo kutengenezwa sikufanya kazi yoyote ila kufanya mazoezi ya nafasi niliyoigiza hatua kwa hatua. Baada ya mazoezi ya kutosha, nilipocheza filamu hiyo nilikuwa na uhakika."

Kutokana na uhodari wake katika filamu hiyo mwaka 2002alipata tuzo za aina tatu, uigizaji wake ulimpatia umarufu. Tokea hapo aliombwa kucheza katika filamu nyingi, lakini alikataa kwa sababu alitaka kuigiza watu wa aina nyingine. Alisema, "Niliwahi kuombwa kuigiza watu kama bosi wa kike niliyeigiza katika filamu ya 'Bosi wa Mkahawa Mdogo', lakini nilikataa, kwa sababu nilitaka kuigiza watu wa aina nyingine. Baadaye nilichagua kuigiza mtu ambaye ni tofauti kabisa na bosi niliyeigiza ili nipate ustadi zaidi."

Mwishoni mwa mwaka 2004 Tao Hong alikuwa mwigizaji wa watu wawili katika filamu ya "Mapenzi Yangu katika Sehemu ya Kangding". Katika filamu hiyo aliigiza kama mtoto mmoja wa mama wa makamo wa kabila la Watibet. Kutokana na uigizaji hodari, kila mmoja kati ya hao wawili aliigizwa vizuri.

Ingawa Tao Hong amekuwa mwigizaji wa filamu kwa miaka mingi, lakini filamu alizocheza si nyingi kwa sababu anaona, ni bora kucheza vizuri filamu chache kuliko kucheza ovyo filamu nyingi. Anapopata nafasi anayopenda anacheza kwa makini sana. Katika miaka ya karibuni Tao Hong anasifiwa zaidi kutokana na uigizaji wake bora katika filamu za aina tofauti, lakini watu hawasikii habari zake nyingine kutokana na tabia yake ya kupenda maisha tulivu. Alisema, "Maisha ya zama zetu yamebadilika kuwa na matamasha mengi, lakini tabia ya watu ni tofauti, sitaki kujitokeza katika matamasha, mimi ni mwigizaji, kazi yangu ni namna ya kuigiza vizuri, sitaki mengine."

Hivi sasa Tao Hong anacheza katika mchezo wa televisheni "Mkahawa wa Mama Yangu". Katika mchezo huo Tao Hong mara nyingi alicheza ngoma ya kabila la Wakorea kwa umahiri.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-13