Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-14 19:07:16    
Mkutano wa mwaka wa kamati ya haki za binadamu wafedheheka

cri

Mkutano wa 62 wa kamati ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ulifunguliwa tarehe 13 huko Geneva, na ulitangaza kupumzika kwa wiki moja baada ya kufanyika kwa dakika 15. Kutokana na mpango wa awali, mkutano mkuu wa mwaka huu ni mkutano wa kupokezana kati ya baraza la haki za binadamu na kamati ya haki za binadamu. Lakini kutokana na upinzani wa Marekani, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hadi hivi sasa bado hazijapitisha mswada wa azimio kuhusu kuanzishwa kwa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, hatua ambayo inafanya mkutano wa mwaka wa kamati ya haki za binadamu ufedheheke toka mwanzoni mwake.

Kutokana na maagizo ya "nyaraka za mafanikio" za mkutano wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Mataifa wa mwaka uliopita, kamati ya haki za binadamu iliyoko Geneva itabadilishwa kuwa baraza la haki za binadamu. Mwenyekiti wa baraza kuu la 60 la Umoja wa Mataifa Bw. Jan Eliasson tarehe 23 mwezi Februari alitoa mswada wa azimio kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuanzishwa kwa baraza la haki za binadamu. Mswada huo uliungwa mkono na nchi nyingi wanachama, lakini ulipingwa na Marekani. Mswada huo unataka baraza la haki za binadamu liundwe na nchi 47, ambazo ziwe zimepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa. Lakini Marekani inataka kupunguza ukubwa wa baraza la haki za binadamu, na nchi wajumbe wa baraza hilo sharti ziwe zinaungwa mkono na zaidi ya theluthi mbili za kura zilizopigwa. Tofauti ya maoni kati ya Marekani na nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa bado haijaondolewa hadi hivi sasa, na mazungumzo husika bado yanafanyika.

Kwa vyovyote vile, mkutano mkuu wa 62 wa kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa utakuwa wa mwisho tangu ilipoundwa mwaka 1946. Katika miaka zaidi ya 60 iliyopita, ingawa kamati hiyo ilidhibitiwa mara kwa mara na nchi za magharibi na kuwa mahali pa nchi za magharibi kushutumu na kusingizia nchi zinazoendelea, lakini ilikuwa na mafanikio ya kihistoria katika utatuzi wa masuala ya haki za binadamu, kutoa na kubuni nyaraka kuhusu haki za binadamu na kutekeleza haki za binadamu duniani. Habari zinasema, kutokana na mswada wa Bw. Eliasson, tarehe 16 mwezi Juni mwaka huu itakuwa siku ya kumaliza majukumu yake ya kihistoria kwa kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kuhusu hali mpya itakayotokea hapo baadaye kwenye mkutano wa mwaka wa haki za binadamu mwaka huu, kuna uwezekano wa aina tatu: wa Kwanza, utakuwa mkutano wa haki za binadamu kama ule wa zamani, ambao utashughulikia mambo halisi, kufanyika kwa wiki 6 na kujadili ajenda zote 21 za mkutano zilizopangwa hapo awali. Lakini uwezekano wa huo ni mdogo.

Wa pili, utakuwa wa kimchakato kuhusu ajenda 4 muhimu: Kusikiliza taarifa kuhusu hali ya haki za binadamu duniani katika mwaka uliopita; kusikiliza taarifa ya mwenyekiti wa awamu iliyopita; nchi wanachama kutathmini kazi za kamati ya haki za binadamu na kutoa azimio la mkutano, pamoja na kukabidhi kazi zote za kamati ya haki za binadamu kwa baraza la haki za binadamu.

Wa tatu, utakuwa mkutano wa mchanganyiko wa shughuli za kimchakato na kihalisi. Lakini hivi sasa nchi mbalimbali zina maoni na tofauti kubwa kuhusu masuala yanayojadiliwa katika kipindi cha mambo halisi cha mkutano.

Kiongozi wa ujumbe wa kudumu wa China katika Geneva Bw. Sha Zukang amesema, nchi mbalimbali zinataka kuwa na mashauriano zaidi kuhusu uendeshaji wa mkutano na masuala halisi yatakayojadiliwa katika mkutano huo wa mwisho wa kamati ya haki za binadamu. Alisema ujumbe wa China ukiwa na lengo la kuhimiza shughuli za haki za binadamu, unatarajia mkutano wa mwaka huu utajenga moyo wa ushirikiano kati ya nchi mbalimbali ili kuweka msingi mzuri kwa uendeshaji wa shughuli wa baraza la haki za binadamu.

Aliongeza kuwa hivi sasa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan na baadhi ya jumuiya zisizo za kiserikali wanafanya mazungumzo na Marekani kuhusu mswada wa azimio wa kuanzishwa kwa baraza la haki za binadamu. Anatarajia pande zote zitachukua msimamo wenye unyumbufu ili kuuwezesha rasimu ya mswada wa azimio hilo ipitishwe.