Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-16 20:32:10    
China na Russia zitaanzisha shughuli za "mwaka wa taifa" ili kuzidisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili

cri

Rais Vladimir Putin wa Russia atafanya ziara ya kiserikali nchini China kuanzia tarehe 21 hadi 22 Machi. Wakati wa ziara hiyo nchini China, marais wa China na Russia watahudhuria sherehe ya kuanzishwa kwa shughuli za "Mwaka wa Russia".

China na Russia zimekuwa nchi majirani na wenzi muhimu wa kimkakati, shughuli za "Mwaka wa taifa" zimeandaliwa kutokana na maoni ya pamoja yaliyofikiwa kati ya marais wa nchi hizo mbili. Mwezi Julai mwaka 2005, rais Hu Jintao wa China alipofanya ziara nchini Russia, marais wa China na Russia walitangaza kuwa, ili kusukuma mbele maendeleo ya ushirikiano wa kiwenzi na kimkakati kati ya China na Russia, nchi hizo mbili zimeamua kuanzisha shughuli za "Mwaka wa Russia" mwaka 2006 nchini China, na kuanzisha shughuli za "Mwaka wa China" mwaka 2007 nchini Russia.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 16 hapa Beijing, msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China ambaye pia katibu mkuu wa kamati ya maandalizi ya China ya shughuli za "mwaka wa taifa" wa China na Russia Bwana Li Hui amesema, hii ni mara ya kwanza kwa China na Russia kuandaa shughuli za "mwaka wa taifa" kwa kila upande katika historia ya uhusiano kati ya China na Russia, hii ni hatua kubwa ya kutekeleza "Mkataba wa ujirani mwema, urafiki na ushirikiano wa China na Russia". Alisema:

Kuandaa shughuli za "Mwaka wa taifa" wa China na Russia ni uamuzi mkubwa wa kisiasa uliotolewa na marais wa nchi hizo mbili, madhumuni yake ni kuongeza urafiki wa jadi na uaminifu, kusukuma mbele ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye sekta mbalimbali za siasa, uchumi, sayansi na teknolojia na utamaduni, kuhimiza ushirikiano wa kimkakati na kiwenzi kati ya China na Russia ili uendelee kwenye kiwango kipya na kutoa mchango mpya kwa ajili ya amani na maendeleo ya dunia.

Bwana Li Hui amedokeza kuwa, mwaka huu China na Russia zinafanya shughuli zaidi ya 20 zinazohusu sekta za siasa, uchumi na biashara, utamaduni, elimu, afya, michezo, vyombo vya habari, sayansi na teknolojia na mambo ya kijeshi, ambapo utafanyika pia mkutano wa wakuu wa sekta za uchumi na biashara, mkutano wa viongozi wa vyombo vya utungaji wa sheria wa China na Russia, maonesho ya picha, maonesho ya michezo ya sanaa na maingiliano kati ya vijana wa China na Russia.

Balozi wa Russia nchini China Bwana Razov Sergey ametoa matarajio yake juu ya ushirikiano kati ya China na Russia kwenye sekta muhimu. Alisema pande mbili zote zinataka kutekeleza miradi mikubwa ya ushirikiano, hasa kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya nishati. Alisema:

Russia imeona uchumi wa China unaendelea kwa haraka, ambapo mahitaji ya nishati yanapanuka siku hadi siku, hivyo kipaumbele kingetolewa kwa ushirikiano katika sekta ya mafua na gesi asilia. Natumai kuwa wakati wa ziara ya rais Putin nchini China, pande mbili zitafikia makubaliano kuhusu ushirikiano kwenye sekta ya nishati.

Bwana Razov anaona kuwa, shughuli za "mwaka wa taifa" ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya Russia na China kwenye jukwaa la dunia, hatua za usawazishaji kati ya Russia na China katika ushirikiano wa pande nyingi na kuhusu masuala makubwa ya kimataifa zinastahili kusifiwa. Alisema:

Russia na China zina msimamo wa pamoja au misimamo inayofanana kuhusu utatuzi wa masuala makubwa yenye utatanishi duniani kwa hivi sasa, na pia zinashirikiana, juhudi hizo hakika zinasaidia kulinda amani na utulivu wa kanda mbalimbali na dunia nzima.