Tokea tarehe 8 mwezi Machi, siku ambapo shirika la atomiki duniani liliwasilisha suala la Nyuklia la Iran kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, baraza la usalama likakabidhiwa rasmi suala la nyuklia la Iran. Hivi sasa mwelekeo wa suala la nyuklia la Iran bado haujafahamika kutokana na kuwa Iran haijaonesha dalili ya kurudi nyuma kutoka kwenye msimamo wake, wakati nchi tano wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama zina mgongano kwenye misimamo yao.
Habari zinasema Uingereza na Ufaransa zimetoa mswada wa taarifa ya mwenyekiti wa baraza la usalama ukitaka Iran "kuendelea kusimamisha upya na kabisa shughuli zote zinazohusika na usafishaji wa nyuklia zikiwemo shughuli za utafiti wake", na kutaka Iran ifikirie upya mpango wake wa kujenga kinu cha nyuklia cha aina ya maji mazito (heavy water). Mswada huo unataka mratibu mkuu wa shirika la atomiki duniani atoe taarifa tena ndani ya siku 14 kwa baraza la usalama kuhusu maendeleo mapya ya suala la nyuklia la Iran, ili baraza la usalama liweze kuchukua hatua zaidi kuhusu suala hilo. Lakini baada ya kushauriana kwa mara kadhaa, nchi tano wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama hazikufikia makubaliano kwenye mswada huo. Hivyo mbali na nchi hizo tano kuendelea kujadiliana, majadiliano hayo yatapanuka na kuzishirikisha nchi 10 zisizo za wajumbe wa kudumu wa baraza hilo tarehe 17 mwezi huu.
Vyombo vya habari vya Ulaya vimefanya uchambuzi na kuona kuwa, utatuzi wa suala la nyuklia la Iran umekuwa na matatizo mengi zaidi hivi sasa, nafasi ya mazungumzo ya kidiplomasia bado ipo, lakini fursa zinaonekana zikipungua kila siku inayopita. Hali hiyo inahusiana na kuongoza upya kwa Marekani kuhusu suala la nyuklia la Iran. Endapo hapo nyuma yalikuwa mazungumzo yaliyofanyika kati ya Umoja wa Ulaya na Iran, basi hivi sasa yamekuwa mazungumzo yanayofanyika kati ya Marekani na Iran. Ingawa hapo nyuma, Marekani ilieleza kuunga mkono jitihada ya amani ya nchi tatu za Umoja wa Ulaya kuhusu suala la nyuklia la Iran, lakini kwa undani Marekani ilikuwa na mashaka, na kusemasema maneno mara kwa mara, ikitishia kuwasilishwa kwa suala la nyuklia la Iran kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Hivi sasa Marekani inaona kuwa utatuzi wa suala hilo unaelekea upande inaotarajia, hivyo ni dhahiri kwake kutumia fursa hiyo ya uongozi katika utatuzi wa suala la nyuklia la Iran.
Ukweli ni kuwa suala la nyuklia la Iran ni chanzo cha utatuzi kamili wa suala la Iran kwa Marekani. Vyombo vya habari nchini Marekani vinasema, mpango wa Marekani ni kuwa kama kuna uwezekano, Marekani inataka wakaguzi wa kimataifa warudi nchini Iran ili kufahamu vizuri zaidi suala hilo; endapo kutakuwa na uwezekano huo, itapaleka suala hilo kwa baraza usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo itafanya kwa hatua kadhaa: Kwanza, kupitisha taarifa yenye msimamo thabiti ya mwenyekiti, kisha kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi ili kudhoofisha nguvu yake na kusaidia makundi yanayoipinga Iran na kuyasaidia makundi ya upinzani kunyakua madaraka ya utawala wa Iran; kitakachofuata ni hatua ya Kijeshi dhidi ya Iran kwa kisingizio kuwa vikwazo havikufanikiwa, na kunyakua madaraka ya utawala wa Iran pamoja na kuleta "demokrasia" nchini humo ili kutatua kabisa suala la Iran.
Ndani ya baraza la usalama, Russia na China zinataka suala la nyuklia la Iran litatuliwe kwa njia ya mazungumzo na kuchukua msimamo wa uangalifu mkubwa kuhusu uingiliaji wa baraza la usalama. Nchi hizo mbili zinaona, mswada wa Uingereza na Ufaransa haukutoa nafasi nyingi ya kutosha kwa shughuli za kidiplomasia, na wala haukutoa muda wa kutosha kwa Iran, hususan katika hali ambayo Russia na Iran zilikuwa zinaendelea na mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran, haifai kuacha jitihada ya utatuzi wa kisiasa kuhusu suala hilo. Katika kipindi cha hivi sasa, Russia na China bado zinasisitiza umuhimu wa shirika la atomiki duniani kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran.
Iran ni nchi mhusika muhimu zaidi katika suala la nyuklia, hivyo chaguo la Iran litaamua mwelekeo wa maendeleo ya suala hilo. Hadi hivi sasa bado hakuna dalili yoyote ya mabadiliko ya msimamo wa nchi hiyo.
|