Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-17 18:10:23    
Kampuni ya China kujenga barabara nchini Tanzania

cri

Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na kampuni ya ujenzi wa barabara na madaraja ya China , wametia saini makubaliano ya ujenzi wa barabara kutoka Kagoma kwenda Lusahanga mkoani Kagera,Tanzania. Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 154 utagharimu Sh . bilioni 48.9.

Makubaliano hayo yalisainiwa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa TANROADS Dk. Fredrick Addo-Abeid na Mhandisi Mkuu wa kampuni ya China Construction engineering Profesa Wang Xiang Ming.

Akizungumza baada ya utiaji saini makubaliano hayo, Dk. Addo-Abeid alisema, mradi huo wa ujenzi wa barabara kutoka Kagoma kwenda Lusabanga ni sehemu ya mradi mzima kuanzia Mutukula-Bukoba kupitia Biharamulo na kuishia Lusahanga.

Dk. Addo-Abeid alisema Sehemu ya kwanza na ya pili ya barabara hizo zimeshajengwa. 'Sehemu ya kwanza ilijumuisha barabara itokayo Mutukula hadi Bukoba Muhutwe yenye urefu wa kilomita 112 iliyotengenezwa na kampuni ya China Henan International Co-operation Group' alisema.

Aidha, alisema kuwa sehemu ya pili ilijumuisha barabara itokayo Muhutwe hadi Kagoma yenye urefu wa kilomita 24 na ujenzi wake ulifanywa na kampuni ya China and Bridge Corporation.

Aliongeza kuwa kazi ya ujenzi wa barabara hizo ilianza mwaka 2002 na kumalizika mwaka 2004. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa miradi wa TANROADS Bw.Boniface Nyitti alisema sehemu ya tatu ya mradi huo uliosainiwa jana inajumuisha barabara ya Kagoma hadi Lusahanga.

Bw. Nyitti alisema fedha za mradi huo ni msaada kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa Tanzania.

Aidha alisema mradi huo utachukua miezi 39 na kwamba unatarajiwa kumalizika Juni 2009.

Aliongeza kuwa Mhandisi mshauri wa mradi huo anatokea nchini India na gharama ya usimamizi itakuwa Sh. 540, 533, 750. Naye Mhandisi Mkuu wa kampuni hiyo Profesa Wang Xiang Ming alisema atahakikisha kazi hiyo inafanyika vizuri na kukamilika kwa wakati muafaka.

Aidha mhandisi huyo aliahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-17