
Wakati miaka mitatu tangu Marekani kuanzisha vita vya Iraq bila kibali cha Umoja wa Mataifa inapokaribia kutimia, watu wanaopinga vita hiyo wa sehemu mbalimbali duniani hivi karibuni walifanya maandamano ya kutoa malalamiko. Katika miji ya New York na Washington nchini Marekani, pia kulikuwa na maandamano ya kutoa malalamiko. Upigaji kura za maoni ulioandaliwa hivi karibuni na mfumo wa habari za televisheni za cable unaonesha kuwa, watu wanaounga mkono sera za rais Bush kuhusu Iraq ni kiasi cha 28% tu, na ni wa kiwango cha chini kabisa. Ingawa serikali ya Bush inajitahidi kuwasihi watu waendelee kuunga mkono vita vya Iraq, lakini sauti ya kukosoa vita vya Iraq imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.
Muda si mrefu baada ya jeshi la muungano la Marekani na Uingereza kuuangusha utawala wa Saddam Hussein, rais Bush alitangaza shughuli muhimu za kivita za jeshi la Marekani nchini Iraq zimeisha. Lakini miaka mitatu imeshapita, shughuli za kimabavu nchini Iraq si kama tu hazijapungua, bali ni kinyume chake idadi ya vifo inaongezeka kwa mfululizo. Takwimu zilizotolewa na jumuiya inayochunguza idadi ya watu waliokufa katika mapigano nchini Iraq zinaonesha kuwa, tokea mwezi Mei mwaka 2003 hadi mwaka 2004, wairaq 6,331 walikufa katika matukio ya kimabavu, mwaka 2005 idadi hiyo inaongezeka kwa haraka hadi kufikia 11,312. Wakati vita ya Iraq ilipotimia mwaka mmoja, kila siku kulikuwa na wastani wa watu 20 wanaouawa, lakini ilipotimia miaka mitatu hesabu hiyo ilizidi 36 kwa siku.
Ili kupata uungaji mkono wa vyombo vya habari rais George Bush tarehe 18 alipotoa hotuba kwa njia ya redio kama kawaida yake kila wiki. Alisema Marekani itamaliza vita hiyo kwa ushindi kamili, lakini alisisitiza kuwa Marekani inatakiwa kujiweka tayari kujitoa mhanga mkubwa zaidi. Tarehe 19 Bw Bush alitoa taarifa katika Ikulu ikizungmzia jinsi Marekani ilivyoisaidia Iraq kupata maendeleo katika kujenga demokrasia nchini mwake, lakini hakutaja mapambano ya kimabavu yanayotokea kila siku nchini Iraq. Jambo linalotatanisha watu zaidi ni kuwa, katika taarifa yake hiyo Bush hakutumia hata neno moja la vita. Katika siku hiyo waziri wa ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld alitoa makala kwenye gazeti la "Washington Post" ikisema, Marekani haiwezi kuondoa jeshi lake mapema kutoka Iraq. Endapo Marekani itaondoa jeshi lake haraka kutoka Iraq, huenda Iraq ikaingia mkononi mwa magaidi.
Ingawa serikali ya Bush inajitahidi kuwaeleza watu wake umuhimu wa kushikilia vita ya Iraq na kujaribu kuwasihi waendelee kuunga mkono sera za serikali kuhusu Iraq, lakini sauti ya kukosoa vita ya Iraq imekuwa ikizidi kuongezeka siku hadi siku. Tarehe 19 Gazeti la New York Times lilitoa makala ya mhariri ikisema, endapo lengo la Marekani ni kuanzisha nchi moja yenye utulivu na demokrasia katika sehemu ya katikati ya mashariki ya kati na kuhimiza sehemu nzima ya mashariki ya kati kukuza demokrasia, basi ukweli wa mambo umethibitisha kuwa lengo la Marekani limeshindwa kabisa.
Mjumbe wa barza la juu la bunge la Marekani anayetoka chama cha Demokrasia Bw Joe Lieberman alisema, katika Iraq vifo na shughuli za kimabavu zinaongezeka kila siku inayopita, serikali haina nguvu, na iko mbali na lengo la kujenga serikali ya umoja. Alilaani kuwa kuangalia kutoka upande wowote, hali ya Iraq imekuwa mbaya zaidi kuliko ile ya mwaka mmoja uliopita.
Kutathmini vita ya Iraq, hata watu wale waliounga mkono vita ya Iraq hapo awali, hivi sasa wanakiri kuwa vita ya Iraq haina mafanikio. Msomi William F. Buckley Jr aliyeunga mkono Marekani kushambulia Iraq, hivi sasa anaona kuwa kushambulia Iraq ni kuanzisha vita kimakosa, kwenye mahali pa makosa na wakati wa makosa.
Kura mpya za maoni zinaonesha kuwa, watu wa Marekani wamekuwa na malalamiko mengi zaidi kuhusu hali mpya ya vita ya Iraq, theluthi mbili ya watu waliohojiwa walisema, rais Bush hakufanya vizuri kuhusu suala la Iraq, na 75% ya watu wanaona kuwa Iraq itakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. 60% ya watu waliohojiwa walisema vita ya Iraq imeleta athari mbaya kwa Marekani, kuna chombo cha habari kinachosema, vita ya Iraq imekuwa "tundu jeusi" katika bajeti ya Marekani, na itakuwa mzigo mzito kwa chama cha Republican katika uchaguzi wa kati mwaka huu.
Idhaa ya Kiswahili 2006-03-20
|