Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-21 16:57:07    
Mbunge wa taifa aliyeshiriki mkutano akiwa na mahindi

cri

Wasikilizaji wapendwa mkutano wa bunge la umma la taifa la China, ambalo ni chombo chenye madaraka kubwa zaidi nchini, ulifungwa tarehe 14 hapa Beijing. Kati ya washiriki zaidi ya 2,900 wa mkutano huo, kulikuwa na mbunge mmoja aliyeshiriki kwenye mkutano akiwa na mahindi, Bw. Li Denghai, mbunge huyo mkulima amevunja rekodi ya dunia ya uzalishaji mahindi kwa kutumia mbegu za mahindi chotara.

Bw. Li Denghai ana umri wa miaka 57, yeye ni mpole na mwaminifu. Mwandishi wetu wa habari alipoingia kwenye chumba chake, aliona mahindi na mbegu za mahindi zilizowekwa ndani ya mifuko midogo. Bw. Li Denghai alisema mbegu hizo za mahindi alizileta kutoka kwenye shamba la majaribio lililoko kwenye kisiwa cha Hainan, umbali wa kilomita zaidi ya 2,300 kutoka kwenye hoteli aliyofikia. Aliongeza kusema atapeleka mbegu hizo hadi kwao, mkoa wa Shangdong, sehemu ya mashariki ya China ili kuotesha mbegu nyingi za aina hiyo.

Lakini ni kitu gani kilimchofanya Bw. Li Denghai asisahau mahindi yake katika sehemu yoyote anakokwenda? Bw. Li alisema, yeye alikuwa mkulima, sasa amekuwa shabiki mkubwa sana kuhusu utafiti wa mahindi. Katika miaka 30 iliyopita alilima zao la mahindi, kufanya utafiti kuhusu mahindi na hatimaye alivunja rekodi ya uzalishaji wa mahindi. Hapo mwanzoni kabisa, Bw. Li Denghai alikuwa na wazo la kufanya watu wengi zaidi waondokane na njaa, kwani alipokuwa mtoto alikuwa na upungufu mkubwa wa chakula.

"Mwaka 1972, China ilianza kuhimiza kilimo cha mahindi chotara, aina ya mahindi waliyopanda wakulima haikuwa na uzalishaji mwingi na uzalishaji ulikuwa kilo 1,500 hivi kwa hekta, lakini uzalishaji wa mahindi chotara unaweza kufikia kiasi cha kilo 3,000 kwa hekta, hali ambayo ilitufanya tuone uwezo mkubwa wa uzalishaji wa mahindi chotara."

Ili kuotesha mbegu bora za mahindi, Bw. Li Denghai na baadhi ya wataalamu wa kilimo walipanda kwa majaribio mbegu bora walizokusanya kutoka sehemu mbalimbali nchini China. Ili kupata mahindi yanayofaa kwa uoteshaji wa mbegu chotara na kuchunguza hali ya ukuaji wa mahindi chotara, Bw. Li alifanya kazi shambani mara kwa mara kwa saa 5 au 6 mfululizo. Bw. Li Denghai alizaliwa mkoani Shandong, ambapo zao la mahindi linaweza kupandwa mara mbili kwa mwaka, lakini mkoa wa Hainan wenye joto kali ni mahali pekee ambapo zao la mahindi linaweza kupandwa katika majira yote manne. Mwaka 1978, Bw. Li Denghai na wenzake walianzisha kituo cha majaribio kwenye sehemu ya milima mkoani Hainan. Hivi sasa wamefyeka mashamba ya majaribio za hekta zaidi ya 10 na kufanya majaribio ya kuotesha mbegu za mahindi kwa miaka 28 mfululizo.

Jitihada za akina Li Denghai hazikupotea bure. Hivi sasa Bw. Li ameotesha mbegu mpya za mahindi karibu aina 100. Mwezi Oktoba mwaka 2005, mbegu mpya alizootesha ziliweka rekodi mpya ya dunia kwa uzalishaji wa tani 2.1 kwa hekta. Hatua za Bw. Li Denghai hazikuishia kwenye mashamba ya mahindi tu, bali pia zinaelekea hadi masokoni. Mwaka 1992 alianzisha kampuni binafsi inayoshughulikia utafiti wa kisayansi, uenezaji wa teknolojia, uzalishaji na uuzaji. Mwaka 2005 hisa za kampuni yake zilianza kuuzwa sokoni, kampuni yake imekuwa ikipata maendeleo mazuri mwaka hadi mwaka, hivi sasa mashamba yanayopandwa mbegu za kampuni hiyo yamefikia theluthi moja ya jumla ya mashamba yote ya mahindi.

Kampuni ya Li Denghai ina nguvu kubwa ya utafiti wa kisayansi, lakini katika maendeleo yao hawana budi kupambana na tatizo moja la hifadhi ya haki-miliki ya kielimu. Alipozungumzia uhusiano kati ya hifadhi ya haki-miliki ya kielimu na kampuni binafsi za utafiti, mkurugenzi Zhang Shihuang, ambaye ni profesa wa kituo cha zao la mahindi cha taasisi ya utafiti wa sayansi ya kilimo ya China, alisema,

"Uzalishaji wa kilimo unaenea kwenye maeneo makubwa, hivyo siri ya teknolojia yake siyo rahisi kuzuiliwa. Katika mazingira ya namna hiyo, mitaji binafsi haiwezi kuingia katika sekta hiyo endapo haki-miliki za kielimu hazilindwi barabara. Lakini ikiwa fedha haziwekezwi kwenye sekta hiyo, basi maendeleo ya teknolojia ya kisasa ya China yatakumbwa na matatizo makubwa."

Mbegu chotara za mahindi alizootesha Bw. Li Denghai zilipewa tuzo la ngazi ya kwanza ya uvumbuzi wa teknolojia ya sayansi mwaka 2004 na kupata hataza ya ngazi ya taifa, tena haki-miliki yake inalindwa na sheria. Alipozungumzia dhamana ya kisheria katika utafiti wa sayansi ya kuotesha mbegu chotara nchini katika miaka ya karibuni Bw. Li Denghai alisema,

"China imepiga hatua kubwa kuliko zamani katika hifadhi ya haki-miliki ya kielimu, baraza la serikali lilibuni na kuanza kutekeleza 'kanuni za hifadhi ya mbegu mpya za mimea' mwezi Aprili mwaka 1997, na ilijiunga na 'mkataba wa hifadhi ya mbegu mpya za mimea duniani' mwezi Aprili mwaka 1999, licha ya hayo China imebuni 'sheria mpya ya mbegu' na kuimarisha hifadhi ya haki-miliki ya kielimu kwa kufuata sheria."

Baada ya kupata mafanikio katika shughuli zake, Bw. Li Denghai aliyekulia kijijini anafuatilia sana suala la ongezeko la uzalishaji la wakulima wa China. Alipozungumzia manufaa wanayopata wakulima kutokana na zao la mahindi Bw. Li anaona, kuongezwa kwa shughuli za uzalishaji wa mahindi ni kitu muhimu sana, wazo la kupata utajiri haliwi kufikiria kilimo peke yake. Alisema, "Shughuli za ufugaji wa nguruwe, kuku, ng'ombe wa maziwa na chakula cha mifugo mingine zina uhusiano mkubwa sana na mahindi. Mahindi ni zao zuri sana, licha ya kuwa ni chakula pia ni mali-ghafi ya viwanda na nishati. Kuna nchi nyingi ambazo kutokana na upungufu wa nishati, zinazalisha spiriti kwa mahindi ikiwa ni nyongeza ya nishati ya petroli."

Bw. Li Denghai ni mwanasayansi, mfanyabiashara na pia ni mbunge wa taifa aliyetoka sehemu ya vijiji, hivyo ana uchungu na wakulima. Kila anapokuta utungaji na usimamizi wa sheria kuhusu manufaa ya wakulima kilimo na maendeleo ya sehemu ya vijiji, anakuwa uchangamfu sana. Katika mkutano wa majadiliano wa vikundi vidogo wa kamati ya kudumu ya bunge la taifa uliofanyika hivi karibuni kuhusu "mswada wa sheria ya ubora na usalama wa mazao ya kilimo", Bw. Li Denghai alitoa pendekezo akitaka ufuatwe utaratibu wa ufuatiliaji wa kisheria kuhusu uzalishaji na uuzaji wa mazao ya kilimo ili kulinda maslahi ya wakulima.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-21