Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-22 19:45:02    
China inafanya utafiti wa chanjo ya homa ya mafua ya ndege kwa binadamu

cri

Hivi sasa homa ya mafua ya ndege inaenea kote duniani. Ugonjwa huo si kama tu unatishia maisha ya ndege, bali pia unatishia afya ya binadamu. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani, hivi sasa watu zaidi ya 160 kote duniani wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo, na nusu kati ya wagonjwa hao wamekufa. Hivi sasa bado hakuna mbinu wala madawa nzuri ya kutibu ugonjwa huo, chanjo ni njia ya pekee ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo mkali. China inajitahidi kufanya utafiti wa chanjo ya homa ya mafua ya ndege kwa binadamu.

Katika miaka miwili iliyopita, sehemu nyingi duniani ziliathiriwa na homa ya mafua ya ndege, na matukio mengi ya binadamu kuambukizwa ugonjwa huo yalitokea kwenye sehemu kadhaa za Asia ya Kusini Magharibi. Wakati huo maambukizi ya ugonjwa huo pia yalitokea nchini China lakini maaambukizi ya ugonjwa huo hayakutokea kwa binadamu. Kutokana na hali hiyo, serikali ya China na idara husika zilitambua tishio la homa ya mafua ya ndege kwa afya ya binadamu na kuanza mara moja kufanya utafiti wa chanjo ya homa ya mafua ya ndege kwa binadamu.

Kuanzia wakati huo yaani mwanzoni mwa mwaka 2004, kampuni ya bidhaa za viumbe ya Sinovac ya China ilikuwa ni kampuni ya kwanza ya China kufanya utafiti wa chanjo ya ugonjwa huo kwa binadamu. Kampuni hiyo maarufu ya teknolojia ya juu ina uwezo mkubwa wa utafiti na uvumbuzi, hasa katika eneo la utafiti wa chanjo, iliwahi kufanikiwa kutengeneza chanjo ya homa ya manjaro A na wakati huo ilikuwa inashirik kwenye kazi ya utafiti wa chanjo ya ugonjwa wa SARS.

Chanjo ya homa ya mafua ya ndege kwa binadamu iliyotengenezwa na kampuni hiyo ni chanjo ya virusi dhaifu. Kutokana na msaada wa shirika la afya duniani WHO, kampuni hiyo ilipata sampuli za virusi vya homa ya mafua ya ndege vinavyoweza kutumika kutengeneza chanjo, na kuanza kazi ya kuzalisha virusi. Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Yin Weidong alieleza kuwa, hatua hiyo ni tatizo kubwa katika kutengeneza chanjo ya ugonjwa huo, kwani ni lazima watafiti waweke virusi ndani ya mayai ili sampuli za virusi hivyo ziweze kuzaliana. Baada ya siku tatu, virusi vinakusanyika.

"watafiti wetu walikuwa na kazi ngumu katika maabara isiyotakiwa kuwa na vijidudu, walitumia mbinu tofauti za utafiti na kupata data nyingi za majaribio. Kwa jumla walitumia mayai milioni moja kukusanya virusi vya kutosha."

Baada ya kupata maendeleo ya mwanzo, watafiti wa kampuni hiyo walifanya majaribio kwa wanyama wadogo. Katika muda wa miezi kadhaa, watafiti walifanya majaribio kuhusu uwezo wa kinga na usalama wa chanjo kwa kutumia panya weupe zaidi ya elfu mbili. Majaribio ya wanyama yameonesha, chanjo hiyo imefanikiwa kuongeza kwa usalama kinga ya panya weupe dhidi ya homa ya mafua ya ndege. Halafu, kampuni hiyo ilifanya utafiti zaidi kuhusu uwezo wa kuzaliana kwa virusi, utulivu wa gene, ufanisi na ustadi wa kudhoofisha virusi, kuthibitisha utaratibu husika na mbinu za upimaji, kujenga ghala za sampuli za virusi na wakamaliza kusanifu na kutengeneza chanjo ya majaribio.

Hadi kufikia mwezi Novemba mwaka jana, kazi zote za utafiti wa chanjo hiyo kabla kutumika kwa binadamu zilikamilika. Tarehe 16 mwezi Novemba, chanjo hiyo iliidhinishwa na kamati ya usimamizi ya chakula na dawa ya taifa la China na kuanza kufanyiwa majaribio kwa binadamu. Siku hiyo hiyo, wizara ya afya ya China ilitangaza tukio la kwanza la binadamu kuambukizwa homa ya mafua ya ndege nchini China.

Baada ya kupata habari hiyo, kampuni ya Sinovac ilirekebisha mpango wa majaribio ya chanjo hiyo na kuongeza idadi ya watafiti na vifaa katika mradi huo, ili chanjo hiyo iweze kufanyiwa majaribio kwa binadamu. Baada ya muda mfupi, kikundi cha majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu kilichoundwa na kampuni hiyo na hospitali ya urafiki wa China na Japan walitoa tangazo la kuwaomba watu wanaojitolea kufanyiwa majaribo. Baada ya siku mbili tu, watu wengi walipigia simu hospitali hiyo kutaka kushiriki kwenye majaribio. Mkurugenzi mkuu wa idara ya matibabu ya magonjwa ya mfumo wa kupumua ya hospitali hiyo Bw. Lin Jiangtao alisema,

"watu wanaojitolea wanatoka sekta mbalimbali, wakiwemo watumishi wa matibabu, makada, wafanyakazi wa kampuni na wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini. Kitendo cha watu hao kuweza kujitolea kushiriki kwenye majaribio hayo ni cha kijasiri."

Hospitali ya urafiki wa China na Japan ilichagua watu sita wanaojitolea kushiriki kwenye majaribio ya kikundi cha kwanza."

Bi. Zhang mwenye umri wa miaka 20 ni mwuguzi, ingawa ana ujuzi wa udaktari lakini baada ya kupigwa chanjo hiyo, bado alikuwa na wasiwasi. Alisema,

"nilikuwa na wasiwasi baada ya kudungwa chanjo, nilidhani nitakuwa na homa lakini sikuwa na dalili mbaya."

Kama ilivyokuwa kwa Bi. Zhang, watu wengine watano waliojitolea wote hawakuwa na dalili mbaya baada ya kudungwa chanjo hiyo. Baada ya siku 56, watu hao wamekuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huo. Baada ya mafanikio hayo, majaribio bado yaliendelea. Mpaka sasa watu zaidi ya 120 wamejitolea kushiriki kwenye majaribio ya chanjo hiyo. Hakuna hata mtu mmoja aliyekuwa na dalili mbaya baada ya kudungwa chanjo hiyo.

Mkurugenzi wa mradi wa utafiti wa chanjo ya homa ya mafua ya ndege wa wizara ya sayansi na teknolojia ya China Bw. Jia Jingdun alisema, ingawa hadi kufikia mwezi Mei na Juni majaribio ya kikundi cha kwanza yatakuwa yamekamilika, na majaribio hayo yataendelea kuwa na vikundi vya pili, tatu na hata nne, lakini ana imani kubwa na utafiti wa chanjo hiyo.

"hivi sasa chanjo hiyo inaweza kuongeza kwa ufanisi kingamwili dhidi ya ugonjwa huo. Lakini bado inahitajika kuthibitishwa kwa majaribio na utafiti. Lakini nina imani kwamba chanjo hiyo inaweza kukinga ugonjwa huo kwa usalama."

Bw. Jia alisema, ingawa bado ni mapema kwa binadamu kuanza kutumia chanjo ya homa ya mafua ya ndege, lakini China imefanya maandalizi kwa ajili ya lengo hilo. Hivi sasa mstari wa kuzalisha chanjo hiyo umekamilika. Baada ya majaribio yote kukamilika au katika hali ya dharura, ikiidhinishwa na idara husika, mstari huo unaweza kuanza kufanya kazi mara moja.