Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-23 16:34:50    
Vita vya watu wawili dhidi ya jangwa vilivyodumu kwa miongo kadhaa

cri

Miaka 73 iliyopita Wang Daqing alipokuwa mtoto, alifuatana na baba yake kuhamia huko Alxa, mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ulioko kaskazini ya China, ambapo walikuwa na lengo moja pekee la kujitafutia mahala pa kuishi. Hata hivyo Alxa ilibadilika kuwa mahali ambapo Bw. Wang alianza vita dhidi ya jangwa, na vita hivyo vimedumu kwa miongo kadhaa.

Bw. Wang Daqing na mke wake Bibi Meng Xiuying, sasa ni wazee wenye umri wa miaka 80. Wanaishi katika eneo linalojulikana kwa kuwa na msitu ndani ya eneo la jangwa, msitu huo una miti zaidi ya elfu 10 ambayo inakua katika mazingira yenye upungufu wa maji na hali ya hewa mbaya, kutokana na kuwa unapakana na Jangwa la Tengger kwa upande wa mashariki.

Bw. Wang na mke wake ni watu shupavu kama miti waliyopanda, wanapendelea kukaa katika kitongoji cha Haosiburdu, wilaya ya Alxa kutunza oasisi hiyo waliyojenga ndani ya jangwa katika miongo iliyopita.

Wang Daqing alizaliwa mwaka 1926katika familia ya wakulima mkoani Gansu. Utotoni mwake alikuwa na maisha magumu. Ili kupata maisha mazuri zaidi, akifuatana na baba yake walipita Jangwa la Tengger na kufikia Alxa, wakati ambapo mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka 8.

Mwaka 1960 Bw. Wang Daqing alihamia na kukaa kwenye kijiji cha Bayanbur, kitongoji cha Haosiburdu mara baada ya kijiji hicho kujengwa.

Wakati huo huo, kazi kuu ya wakazi wa huko ilikuwa kupanda miti na kulishughulikia jangwa ili liweze kulimika. Bw. Wang alikumbusha kuwa, "Kila mtu alikuwa anaitikia mwito wa serikali wa kubadilisha ardhi ya taifa iwe ya kijani."

Mwaka 1983 China ilitekeleza sera ya wakulima binafsi kusaini mkataba na serikali wa kupewa haki ya kulima mashamba. Kutokana na sera hiyo, ardhi ya hekta kadhaa zenye miti waliyopanda wanakijiji iligawanywa. Miti hiyo ilikatwa kwa haraka, na kijiji hicho cha Bayanbur kwa mara nyingine kilibadilika na kuwa ardhi kame. Bw. Wang alikuwa na wasiwasi mkubwa, lakini hakuacha ndoto ya kugeuza ardhi kame kuwa msitu.

Alianza kupanda miti kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 3 ambalo alijenga wigo na kutumia kisima kilichoachwa na kikosi cha kujenga taifa. Aliweka lengo la kupanda miti katika ardhi isiyopungua hekta 0.06 kwa mwaka.

Ni vigumu sana kwa mti kuweza kukua katika eneo la Jangwa la Tengger ambapo kiasi cha wastani wa milimita 100 tu za mvua hunyesha kwa mwaka.

Watu wengi hawakuamini uwezo wa Bw. Wang na wengine walimshauri aache mpango huo. Hata hivyo Bw. Wang alipuuza mapendekezo hayo. Alimshawishi mke wake kufuga peke yake mbuzi wa makumi kadhaa wa familia hiyo, ambapo yeye mwenyewe kuanzia hapo alijitia kabisa katika shughuli za kupanda miti.

Ilimchukua siku kadhaa kununua miche ya miti kutoka kwa kitongoji cha Haosburdu, na aliiwekea miti yake mbolea. Siku nyingine ilimbidi afanye kazi kwa saa 24 kwa siku kadhaa mfululizo ili kumwagilia miti. Hata hivyo Bw. Wang alifurahia kuona ardhi ya kijani inaongezeka siku moja baada ya nyingine.

Ili waweze kupanda na kutunza miti, Bw. Wang na mke wake walikataa mwaliko wa binti yao wa kuishi maisha rahisi mjini. Mke wake Bibi Meng Xiuying hakuondoka wilaya ya Alxa kwa miaka 15 na wazee hao hawakuhudhuria kwenye harusi ya mjukuu wao miaka mitatu iliyopita.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imewahamisha wakazi wengi kutoka kwenye maeneo yenye mazingira magumu mpaka na kuwapeleka kwenye maeneo yenye mashamba au mijini katika juhudi za kuinua kiwango cha maisha yao. Wakazi wengi wameondoka kutoka kitongoji cha Haosiburdu katika miaka ya karibuni, ambapo katika ardhi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 7,814, sasa wamebaki watu 1,500 tu wakiwemo Bw. Wang na mke wake, ambao wanaendelea na shughuli za kutunza miti yao.

Bw. Wang na mke wake walipewa hati ya kumiliki msitu huo mwaka 2003. Hivi sasa wao wamezeeka sana kiasi kwamba wanashindwa kupanda miti wao wenyewe, kwa hivyo wana hamu ya kuwapata watu watakaoweza kuendelea na shughuli za kutunza miti na kuongeza ukubwa wa msitu.

Baadhi ya watu walikwenda kutazama miti lakini walikuwa na wasiwasi na mazingira magumu ya huko. Mwaka huu Mzee Wang aliamua kuikabidhia serikali umiliki wa miti hiyo, na yeye na mke wake wataendelea kuitunza hadi watakapofariki dunia.

Mwaka 1979 China ilianza kuadhimisha tarehe 12 Machi siku ya kupanda miti ili kuwahamasisha wananchi kupanda miti kwa hiari kote nchini. Wanasayansi wanasema katika miongo mitatu iliyopita juhudi za wananchi za kupanda miti kwa hiari zimebadilisha ardhi yenye ukubwa wa kilomita 219,000 za mraba kuwa misitu. Hivi sasa misitu ya China inahifadhi mbao mita za ujazo bilioni 12.456, na kati yao mbao zaidi ya mita za ujazo bilioni moja zilipandwa baada ya mwaka 1949 wakati China mpya ilipoasisiwa.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-23