Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-23 20:07:48    
Athari mbaya ya maafa ya kimaumbile kwa maendeleo endelevu

cri

Sasa imetimia miaka 46 tangu shirika la hali ya hewa duniani liitangaze tarehe 23 mwezi Machi kuwa "siku ya hali ya hewa duniani". Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku hiyo mwaka huu ni "kuchukua tahadhari na kupunguza athari ya maafa ya kimaumbile. Sababu ya kuchagua kauli-mbiu hiyo kwa shirika la hali ya hewa duniani ni kufikiria kuhusika kwa 90% ya maafa ya maumbile pamoja na hali ya hewa na maji; tukiangalia katika miaka ya karibuni, athari mbaya inayoletwa na maafa ya kimaumbile imekuwa kubwa mwaka hadi mwaka kwa maendeleo endelevu ya nchi mbalimbali.

Mwaka 2005, ukame ulitokea kwenye pembe ya Afrika, baadhi ya sehemu za Ulaya, Asia, Australia na Brazil, ambapo ukame uliotokea nchini Malawi ni mkali zaidi katika miaka 10 iliyopita. Walakini, baadhi ya sehemu za dunia ziliathiriwa vibaya na mafuriko. Kimbunga chenye uharibifu mkubwa kilichotokea kwenye bahari ya Atlantic kiliweka rekodi mpya ya kihistoria. Tundu la hewa ya ozone kwenye anga la ncha ya kaskazini ya dunia linaendelea kupanuka, wakati tundu la hewa ya ozone kwenye anga la ncha ya kusini ya dunia lilichukua nafasi ya tatu kati ya takwimu zilizopatikana katika miaka ya nyuma. Tsunami iliyotokea mwishoni mwa mwaka 2004 ilikuwa na uharibifu mkubwa zaidi katika historia. Katika miaka 10 kati ya mwaka 1992 na mwaka 2001, watu bilioni 2 walikumbwa na maafa ya kimaumbile ya aina mbalimbali, ambapo watu zaidi ya laki 6 na elfu 22 walipoteza maisha yao. Hasara iliyosababishwa na maafa mafuriko na kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ilifikia dola za kimarekani bilioni 226 ikiwa ni 65% ya hasara iliyoletwa na maafa ya maumbile duniani.

Takwimu husika za shirika la hali ya hewa duniani zinaonesha kuwa, katika miongo kadhaa iliyopita, athari mbalimbali zilizoletwa na maafa ya kimaumbile kwa uchumi wa nchi mbalimbali ziliongezeka kwa udhahiri, hasa katika nchi zinazoendelea, hususan nchi zilizoko nyuma kimaendeleo. Maendeleo ya jamii na uchumi ya baadhi ya nchi hizo yalirudi nyuma kwa miaka miongo kadhaa kutokana na maafa hayo. Kutokana na kukabiliwa na changamoto hiyo, shirika la hali ya hewa duniani linaona kuwa, kuchukua tahadhari juu ya maafa ya kimaumbile na kupunguza athari ya maafa ni dhamana muhimu kwa maendeleo endelevu.

Shirika la hali ya hewa duniani linaona kuwa ingawa ni vigumu kujiepusha na maafa ya kimaumbile, lakini binadamu wanaweza kupunguza idadi ya vifo, majeruhi na uharibifu wa kiuchumi kwa kuchukua hatua ya kutoa onyo kabla ya kutokea maafa na kuweka mipango ya kupambana na maafa. Mbinu muhimu zaidi kati ya hatua hizo zinazoweza kuchukuliwa ni kujenga mfumo wa tahadhari kabla ya kutokea kwa maafa ili kuwapa habari za uhakika watu wanaokabiliwa na hatari.

Katika upande wa kimataifa, vituo vitatu vya ngazi ya kimataifa na vituo 40 maalumu vya kikanda vya shirika la hali ya hewa duniani vinatoa huduma ya miundo mbinu ya kazi hiyo kwa nchi mbalimbali, ili kutoa utabiri kuhusu maafa ya aina mbalimbali yakiwa ni pamoja na tufani, mvua kubwa kupita kiasi na ukame. Aidha, shirika hilo limejenga mfumo wa kupima mzunguko wa hewa wa sehemu ya tropiki wa dunia nzima, ambao unafanya kazi zenye ufanisi mkubwa kwa kutoa utabiri kuhusu kimbunga. Idara za hali ya hewa na maji za nchi mbalimbali zinaweza kutoa utabiri na maonyo kuhusu mzunguko wa hewa ya sehemu ya joto katika nchi yake kwa mujibu wa utabiri uliotolewa na mfumo wa upimaji wa kimataifa na kuwafahamisha viongozi wa nchi, vyombo vya habari na umma kwa wakati.

Mbali na hayo shirika la hali ya hewa duniani linapeleka teknolojia kwa nchi zinazoendelea na kuzisaidia kukuza uwezo wao na mfumo wa usimamizi wa data, ili kuhakikisha kwamba nchi zote hususan nchi maskini zinaweza kupata kwa usawa habari na data muhimu kuhusu maafa ya kimaumbile.

Mratibu mkuu wa shirika la hali ya hewa duniani Bw. Michel Jarraud amesema, shirika hilo lina imani ya kupunguza nusu ya idadi ya watu wanaokufa kutokana na maafa ya mafuriko na mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya miaka 15 ijayo kwa kufanya ushirikiano na serikali na washiriki mbalimbali.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-23