Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-27 15:03:47    
Liuyang mkoani Hunan China

cri

Mliosikia ni wimbo uitwao Mto Liuyang, wimbo huu unaimba hivi, tukipita vipengele kadha wa kadha vya Mto Liuyang tukafika Mto Xiangjiang, sehemu hiyo kuna mandhari nzuri ya kupendeza. Mji mdogo Liuyang ulioko kusini ya kati ya China una mandhari nzuri, mjini humo milima na mito inaegemeana, na mji huo pia unajulikana kwa fashifashi zilizotengenezwa huko.

Tukipanda basi kufunga safari kutoka Changsha, mji mkuu wa mkoa wa Hunan, baada ya saa moja na zaidi tutafika Mji mdogo wa Liuyang. Mto Liuyang unaopita mji mzima ni maarufu zaidi, kwani jina la mji pia lilitokana na mto huo.

Mto Liuyang una vipengele vingi, kando ya mto ni sehemu zenye mandhari nzuri. Kila ukipita kipengele kimoja cha mto huo, utaona eneo moja la ardhi yenye rutuba kutokana na mtiririko wa maji ya mto, miti mingi ya mianzi inafunika vijiji vingi vidogo vilivyoonesha umaalum wa sehemu ya kusini ya Mto Changjiang wa China. Ukipanda jahazi mtoni, kwenye sehemu ya mto yenye maji kidogo, hata unaweza kutembea mtoni na kuiwezesha miguu yako ipapase na mawe madogo ya mviringo yaliyo chini ya mto huo. Kama ukipata bahati unaweza kuokota mawe ya maua ya chrysanthemum. Mawe hayo ni pekee ambayo yanaweza kuokotwa tu chini ya Mto Liuyang. Bibi Du Xinqi anayeishi kando ya Mto Liuyang kwa miaka mingi alituambia:

Mawe ya maua ya chrysanthemum ni mawe maalum yaliyopo kwenye maskani yetu Liuyang, mawe hayo yanakuwa chini ya mto, ambayo ni mawe yaliyotanuka yakionekana kama maua ya chrysanthemum, mawe ya aina hiyo yakitengenezwa na fundi wetu yanakuwa ni vitu vya sanaa. Mawe ya aina hiyo yanajulikana duniani, na bei kubwa za baadhi ya mawe hayo ni ghali sana, hata zinafikia Yuan zaidi ya laki moja au laki mbili.

Mawe ya aina hiyo yaliumbika miaka milioni 200 iliyopita, hivyo yanaonekana kama ni mawe yenye vipande vya maua ya chrysanthemum vinavyonyooka na kupendeza. Miaka mia 4 iliyopita, wasanii wa Liuyang walianza kutafuta mawe hayo, kuyachonga kuwa vinyago vya mawe vya aina mbalimbali kwa kufuata maumbo yake ya kiasili. Mwaka 1915, kwenye maonesho ya makumbusho ya vitu vya nchi mbalimbali duniani yaliyofanyika nchini Panama, pazia la kinga ya upepo lililochongwa kwa mawe ya chrysanthemum na msanii mzee Dai Qingsheng lilipewa tuzo la dhahabu. Mwandishi wetu wa habari aliwahi kuona kinyago kimoja cha mawe ya chrysanthemum chenye mita 8 za mraba, chini yake ni kinyago cha dragon anayejizungusha, na mwilini mwa dragon huyo kuna maua meupe ya chrysanthemum ya mawe zaidi ya kumi ambayo yanaonekana kama ni maua mabichi ya kweli yanayopendeza sana.

Tukitembea kwa umbali wa zaidi ya kilomita 20 kwa kufuata Mto Liuyang tutafika kwenye chanzo cha mto huo Mlima Daweishan. Mlima Daweishan ni bustani ya misitu ya ngazi ya taifa. Kwenye bustani hiyo kuna miti ya aina zaidi ya 2000 na wanyama wa aina zaidi ya 50. Bustani hiyo ni nadra kupatikana katika mkoa wa Hunan wenye hali ya hewa ya nusu tropiki. Katika sehemu ya Mlima Daweishan kuna vivutio vingi, ambapo kuna maziwa na chemchem nyingi, na maporomoko makubwa ya maji ya Xiling yako huko. Katika majira ya siku za mchipuko, maua mengi yanachanua mlimani, huko pia kuna miti inayopendeza, ukiigusa kidogo itaweza kutikisika kama inaogopa

Mji Liuyang pia unajulikana kwa fashifashi za huko. Fashifashi zinazotengenezwa mjini humo zinajulikana duniani, kwenye jumba la ukumbusho wa fashifashi, watalii wanaweza kufahamishwa historia ya fashifashi ya Liuyang. Mwongozaji wa utalii Bi.Yuan Huijuan alituambia:

Fashifashi na fataki za Liuyang zimekuwa na historia ya zaidi ya miaka 1400, kwenye jumba la makumbusho ya Liuyang kumewekwa kumbukumbu nyingi kuhusu ufundi wa kutengeneza fataki na fashifashi, ambao baadhi yao sasa hazitumiki tena, hivi sasa fataki na fashifashi nyingi zinatengenezwa kwa mashine badala ya mikono. Hivyo wakazi wa Liuyang walikusanya kumbukumbu hizo za ufundi wa kutengeneza fataki na fashifashi, wanajivunia na kumbukumbu hizo.

Kwenye jumba hilo, fundi mzee aliwaonesha watazamaji mchakato rahisi wa kutengeneza fataki na fashifashi, mwandishi wetu wa habari alivutiwa na utaratibu mmoja baada ya mwingine wa kutengeneza fataki na fashifashi, alisema zamani alijua tu kuangalia fashifashi zilizopigwa ambazo mvuto wake huwafurahisha sana watu, baada ya kutazama kazi waliyooneshwa na fundi, akajua kuwa kumbe kutengeneza fataki na fashifashi ni kazi ngumu. Hivi sasa viwanda vya kutengeneza fataki na fashifashi vimetengeneza fataki na fashifashi kwa teknolojia ya tarakimu ya hali ya juu, kazi hiyo imekuwa rahisi. Na fataki na fashifashi zilizotengenezwa na viwanda vya Liuyang zimekuwa za aina zaidi ya elfu 3, ambazo zinauzwa katika nchi na sehemu zaidi ya mia moja duniani. Kila ifikapo sikukuu, fashifashi zinazopigwa kote nchini China takriban zote ni bidhaa zilizozalishwa huko Liuyang.

Mjini Liuyang kuna nyumba nyingi za kale zilizopangwa vizuri kando ya njia ya kutembea mjini humo. Mwongozaji watalii Dong Cai-e alituambia:

Njia ya utamaduni wa jadi mjini Liuyang ilijengwa kwa kufuata mtindo wa utamaduni wa jadi wa wakazi wa Liuyang, kwenye njia hiyo kuna minara 12 midogo ya mawe iliyochongwa kwa wanyama 12 ambao kila mmoja ni mwakilishi wa mwaka wa jadi wa China. Kando ya njia hiyo kuna maduka mengi ya kuuza vitu maalum vya kienyeji, kama vile mawe ya maua ya chrysanthemum, fataki na fashifashi za Liuyang pamoja na vyakula mbalimbali.

Na siku ile usiku mwandishi wetu wa habari alipata bahati ya kutazama tamasha la fashifashi, ambapo aliona fashifashi nyingi za aina mbalimbali zilipigwa na kurushwa angani, baadhi yake zilikuwa kama maua yaliyochanua mbinguni, nyingine kama nyota zinazometameta angani, nyingine zilikuwa kama maporomoko ya maji kutoka angani, na nyingine zilikuwa kama tausi waliochanua mkia, hata nyingine kama milima na misitu iliyoyumbayumba, na kama maji ya mto yanayotiririka. Yote hayo yalimshangaza sana, kweli hawezi kufikiri jinsi fashifashi hizo zilivyotengenezwa. Mwandishi wetu habari alisema, baada ya kuondoka huko, hata mvuto wa fashifashi hizo uliendelea kukaa akilini mwake kwa siku kadhaa.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-27