Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-28 18:34:33    
Barua 0326

cri

Msikilizaji wetu Bi. Sheale Charles ambaye barua zake huhifadhiwa na T.S. Amooti wa sanduku la posta 114 Kasese Uganda, ametuletea barua akituomba tumsaidie kutafuta rafiki wa kalamu, mwenye roho ya utu na anayeweza kumsaidia kwenye masomo yake, anataka rafiki huyo awe mwanamke mwenye umri wa miaka 18 hadi 22 au mvulana mwenye umri wowote.

Kwanza tunashukuru sana kwa kupata barua hiyo kutoka kwa msikilizaji wetu huko Uganda, kwa kutuandikia barua hii. Kwa kweli huwa ni nadra kwetu kupata barua kutoka Uganda, kwa hiyo tumeifurahia sana barua yake, tunaisoma hapa tukitumai kuwa wasikilizaji wetu wanaweza kumsaidia.

Msikilizaji wetu Godfrey Kahemela wa sanduku la posta 992 Dodoma Tanzania ametuletea barua akisema, anapenda kutushukuru sana kwa huduma ya utangazaji tunayowapatia. Anasema wamejifunza mengi na wamefaidika nayo. Pia anaomba kama itawezekana tumtumie kadi za salaam na pia nakala za jarida zuri la daraja la Urafiki. Na bila kusahau kitabu cha kujifunza kichina. Anasema yeye ni mwanafunzi aliye kidato cha sita na anatarajia kuhitimu masomo yake hivi karibuni mwaka 2006. Anasoma masomo ya Bailojia, kemia na fizikia. Hivyo anapenda kuulizia kama kuna shirika au chuo chochote kinachotoa ufadhili kwa elimu ya chuo anaomba tumtumie anuani yao au jinsi ya kuwapata.

Na msikilizaji wetu Isack Kulwa wa sanduku la Posta 69041 Dar es Salaam ametuletea barua akianza kwa kutusalimu, na kusema yeye anaendelea vizuri na shughuli zake za kawaida. Anasema amefurahishwa sana na shughuli zetu nzuri tunazofanya za kuwashughulikia wasikilizaji wetu bila upendeleo wowote, anasema ni kazi nzuri na anatuomba tuendelee hivyo hivyo.

Pia anasema anatumia nafasi hii kutufahamisha kuwa hivi sasa amehamia sehemu fulani hapo hapo Dar es Salaam ambapo kusema kweli ni amekuwa akitupata kwa shida sana, mwanzoni alikuwa eneo la chuo kikuu cha Dar es Salaam ambako alikuwa anatupata vizuri tu, hivi sasa yuko eneo la mtoni kijichi hapo hapo Dar es Salaam, huko sasa amekuwa hawezi kutupa vizuri, anashindwa kuelewa tatizo ni nini, hata hivyo anasema jarida la daraja la urafiki linaendelea kufanya kazi yake ya kutuunganisha, hivyo urafiki wetu utadumu milele.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Isack Kulwa kwa barua yake, na shukrani zake kwetu, kweli ingawa tumefanya juhudi za kuwahudumia wasikilizaji wetu, lakini bado hazitoshi na tunasikitishwa na usikivu usio mzuri wa sehemu aliko. Kusema kweli siku hizi barua kutoka kwa wasikilizaji wetu wa Tanzania zimepungua, labda ni kutokana na hali ya usikivu ikilinganishwa na usikivu wa kituo chetu cha FM huko Nairobi Kenya, kweli tunapaswa kufanya juhudi zaidi ili kuwawezesha wasikilizaji wetu walioko Tanzania wasikilize vizuri zaidi matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Nicholas Mokaya Magasi wa sanduku la posta 12105 Nairobi Kenya ametuletea barua akisema angependa kutuma pongezi zake kwa wote wanaohusika na matangazo ya Radio China kimataifa. Anasema tangu wakutane na ujumbe wetu mjini Kisii ameona maendeleo na juhudi kubwa ambazo tunafanya ili kuboresha matangazo yetu. Hivi karibuni wameshuhudia kufunguliwa kwa kituo cha FM cha Radio China kimataifa jijini Nairobi. Akiwa mmoja wa wale waliokisikiliza kwanza, anatoa pongezi tena kwa vile matangazo ni masafi na anaomba tujaribu kupanua ili wengine waweze kusikiliza kwa urahisi.

Anasema juhudi zetu wanaziunga mkono na ana hakika kuwa maoni yao ni ya manufaa kwa utayarishaji wa vipindi vyetu, kwa hakika amejionea na kujifunza mengi kuhusu China kwa kupitia kituo chetu cha FM huko Nairobi Kenya. Lakini pia anatoa ombi, anasema angependa kutoa mchango wake ikiwa unahitajika katika kituo hiki kwa kujitolea. Yeye amesomea kuhusu ukusanyaji wa habari na uhariri, maktaba, uchapishaji na makavazi. Mchango wake anadhani utatufaa katika shughuli zetu za kila siku.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu huyo kwa barua zake za pongezi kwa kuanzishwa kwa kituo chetu cha FM cha Nairobi Kenya. Kweli hatua ya mwanzo tumepiga, tunaendelea na juhudi za kuboresha vipindi vyetu, hivi sasa tunahitaji zaidi kusikiliza maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wetu, tunataka kujua kihalisi, wasikilizaji wetu wa Nairobi Kenya wanapenda zaidi vipindi gani na kutaka kuelewa nini kuhusu China. Mpaka sasa tumepata barua kadha wa kadha kutoka kwa wasikilizaji wetu ambao wanataka kutusaidia katika shughuli za kituo hiki huko Nairobi, hapa tunapenda kuwaambia kuwa, ikiwezekana labda tunaweza kuwaambia wahusika ili wakuchague, lakini kwa kweli tuko hapa China, si rahisi sisi shughuli zetu ni kuandaa vipindi, kutafsiri na kutangaza, nyingine zinashughulikiwa na watu wa ofisi nyingine. Tunaomba wasikilizaji wetu mtuelewe na kuendelea kuunga mkono kazi yetu, kutoa maoni na mapendekezo kutusaidia kuboresha matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Geoffrey Wandera Namachi wa sanduku la posta 57333, Nairobi Kenya anasema katika barua yake kuwa, huu ni mwaka wake wa tatu kusikiliza matangazo ya CRI kwa mfululizo, na kutoa maoni mbalimbali mara kwa mara. Kwa ufupi anatoa pongezi kwa CRI kwa huduma zetu mwafaka. Ukweli ulio wazi kama mchana wa jua, ni kwamba China imeleta nyota ya maendeleo barani Afrika hasa Kenya.

Anasema anaipongeza CRI kwa kumtunuku kalenda ya mwaka 2006 pamoja na kumkumbuka mara kwa mara. Anashukuru Radio China kimataifa kwa kumtumia bahasha na kadi za salamu kila mwezi, kutokana na shindano la chemsha bongo hii ndio mara yake ya kwanza kulifanya kwa hivyo penye nia pana njia. Baada ya shindano hilo kukamilika ni bora tuwaandalie historia hiyo kwa gazeti dogo kuhusu chanzo cha kuwepo kwa hali ya sasa kati ya China bara na Taiwan. Anasema kutokana na ujenzi wa kituo kipya cha FM huko Nairobi Kenya hakika ni hatua ya kujivunia na kupongezwa kwa dhati. Kituo hiki kilichofunguliwa rasmi mwishoni mwa mwezi wa Januari mwaka huu, ni ishara ya maendeleo yenye matunda mema.

Anasema vipindi wanavyosikiliza huko Nairobi wanavipenda sana. Lakini anasema itakuwa ni jambo la busara kama tutaongeza kipindi cha mahubiri na nyimbo za dini kwa upande wa Kiswahili kwa nusu saa. Anasema

China na Kenya zimekuwa na urafiki wa kiwenzi wa muda mrefu. Kuna uhusiano wa kibiashara, mawasiliano, kuinuana kiuchumi na ushirikiano mbalimbali kwenye sekta tofauti pamoja na mashirika mbalimbali. China imeisisimua Kenya na maendeleo ya historia ambayo itakuwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Anasema Mungu aibariki Radio China Kimataifa iweze kunawiri zaidi na kupanuka. Anafahamu kwamba Radio China Kimataifa itaendelea kuwakumbuka wasikilizaji wake mara kwa mara. Na kwa udhahiri mkubwa ni kwamba Radio China Kimataifa ni nguzo imara katika kuboresha lugha ya Kiswahili nchini China.

Anamaliza barua yake kwa kusema anapenda kuwakumbuka kupitia CRI, Bernard Namachi, Corronelia Namachi, Melisa Ochieno, Mary Ivelia Namachi, Rose Awino, Sande Linus Ogutu, Mourice Ochieno, Sarah Awino Odongo, na John Odaba. Anasema watafurahi kusikia barua hii ikisomwa kwenye kipindi cha sanduku la barua Jumapili yoyote.

Mutanda Ayub Shariff, Box 172, Bungoma anasema katika barua yake kuwa, Shukurani kwa kazi njema tunayoendelea kufanya tangu mwanzo wa mwaka huu. Ana uhakika haijawa kazi rahisi na imegharimu pesa nyingi na bidii, kuhakikisha wasikilizaji wanapata habari kwenye mtandao au tovuti ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Kwa hivyo wasikilizaji wanapata fursa ya kusoma makala za Radio China Kimataifa kila mara.

Anasema kwa kipindi cha sanduku la barua, anatoa maoni yake tena. Anatushauri kuwa tungejitahidi kadiri tuwezavyo kutilia maanani kusoma barua kwa wakati. Kwani sio jambo zuri ikiwa barua inasomwa na huku ujumbe wake ukiwa umechelewa kwa muda kama miezi miwili au mitatu. Kutokana na sababu hii hata maana ya barua yenyewe inakuwa imepotea.

Tunamshukuru sana Bw Mutanda kwa maoni yake, lakini tunaomba wasikilizaji wetu waweze kutuelewa, kuna wakati barua kutoka kwa wasikilizaji wetu huwa zinachelewa kufika, na ni kweli baadhi zinachukua hata miwili au mitatu kutufikia. Hata sisi hatujui ni kwanini barua hizo zinachelewa na hatujui huwa zinachelewa wapi. Tunajitahidi sana kila barua ya msikilizaji inapofika tunahakikisha kuwa tunaisoma kwa wakati na kuijibu. Pia tunafanya juhudi kusoma kwa wakati kila barua zilizoandikwa vizuri na wasikilizaji wetu, hata hivyo katika siku za baadaye tutatilia maanani zaidi kazi hiyo.

Kuhusu salamu zenu wasikilizaji wetu wana maoni tofauti, na sisi tutafuata utaratibu tuliyowekewa, labda siku za baadaye tutaongeza muda wa salamu zenu, lakini hivi sasa kutokana na hali halisi ya idhaa yetu, hatuna nguvu za kutosha, tunaomba wasikilizaji watuelewe.

Na kwa upande wa salamu zenu Bwana Mutanda anasema, anatoa pongezi sana kwa nyimbo ambazo zinawavutia mashabiki wengi, anasema nyimbo hizo ni nzuri kabisa. Hata hivyo anasema kadi ambazo zinasomwa bado ni chache. Ingekuwa vyema kama kila siku zisomwe kadi kumi za salamu. Na tena ziwe zikisomwa mara mbili au tatu. Pia anasema ni vizuri kama salamu zenu hazitarudiwa mara nyingi, ili wasikilizaji waweze kupata fursa ya kusikiliza salamu nyingi zaidi.

Pia anasema angependa kutufahamisha kuwa jarida la urafiki bado linaendelea kufanya kazi. Siku chache zilizopita alikutana na Bw. Maxwell Mulongo Fwamba, ambaye alikuwa na hamu kubwa kufahamu mengi kuhusu Radio China Kimataifa. Jambo la kushangaza ni kwamba walipokuwa akitembelea Bw. Kenneta, walikuta jarida la urafiki ambalo alisoma kimoyomoyo. Alipoona picha ya Bw. Mutanda Ayubu Shariff ambaye alimfahamu vizuri sana, kwanza kabisa hakuwaamini. Alichukua juhudi ya kumtafuta ili amfahamishe mengi kuhusu Radio China Kimataifa. Na kwa kweli alivyompata hakukawia kumpasha habari hii kwa urefu.

Baada ya Bw. Maxwell kumuulizia kwa undani habari kuhusu Radio China Kimataifa, rafiki yake mwingine Bw. Chrispin Wafula naye kutoka Webuye alipenda kujua mengi. Walikuwa wakishangaa, kwani mwanzo walidhani Radio China Kimataifa ni kwa ajili ya wachina tu, lakini walishangaa sana kusikia wasikilizaji wa Kenya wakisalimiana na kutakiana heri kwa kupitia matangazo ya Radio China Kimataifa, pia alishangaa kusikia kuwa kila mara wasikilizaji wengi wakimsalimia Bw. Mutanda Ayubu.

Hii ilimfanya kusafiri kutoka mjini Webuye hadi kwa Bw. Ayub ili kupata habari kamili kuhusu Radio China Kimataifa. Naye vilevile angalau apate kujihusisha na hali ambayo kwa kweli inafurahisha watu wengi sana. Bwana Mutanda naye pia hutumia fursa hiyo kuwakabidhi wasikilizaji hao kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ili iweze kuwahusisha nayo