Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-30 16:55:05    
Kampeni dhidi ya matumizi ya ovyo ya chakula katika mikahawa mjini Shanghai

cri

Kwenye mkahawa mmoja huko Shanghai, mji wa mashariki ya China, mhudumu alimshauri mteja akisema, "Chakula ulichoagiza ni kingi mno kwa watu watano, bwana. Kwa nini usiache sahani ya mwisho ya chakula ulichoagiza?" Mteja huyo alikubali kwa kuitikia kwa kichwa chake. Kando ya meza nyingine, mhudumu aliwaletea wateja visanduku viwili vya chakula, ili waweze kwenda nyumbani na chakula kilichobaki. Hiyo ndiyo kampeni ya kupunguza matumizi ya ovyo ya chakula inayotekelezwa katika mikahawa mjini Shanghai.

Meneja wa mkahawa uitwao "Familia ya Shanghai" Bw. Liu Dafeng alieleza kuwa, "Kila siku tunakusanya chakula kisichopungua kilo 30 ambacho kinaachwa na wateja. Na kati ya asilimia 30 ya chakula hicho kinakuwa hakijaonjwa na wateja."

Mkahawa huo unashirikiana na kampuni moja ya Korea ya Kusini, kuwahudumia wateja visanduku vya chakula visivyoharibu mazingira bila malipo, ili wateja waweze kwenda nyumbani na chakula ambacho wanashindwa kukimaliza.

Hata hivyo, Bw. Liu alisema si rahisi kuwashawishi baadhi ya wateja wasiagize chakula kinachozidi uwezo wao wa kula, kutokana na mtizamo wa jadi wa Wachina, aibu kwa anayelipia chakula iwapo watu aliowaalika kula wanamaliza chakula bila kuacha chakula kidogo mezani.

Uchunguzi uliofanyika hivi karibuni unaonesha kuwa, asilimia 81 ya Wachina wanaokula mihakawani hawawezi kumaliza chakula wanachoagiza, ambapo asilimia 28 kati yao hawachukui chakula kinachobaki na kwenda nacho nyumbani hata mara moja, na asilimia 53 ya watu wanajitetea kuwa hawataki kuchukua chakula na kwenda nacho nyumbani chakula, kwani chakula kinachobaki si kingi sana.

Uchunguzi huo pia unaonesha kuwa, Wachina wanaume wenye umri kati ya miaka 30 na 40 ni wabadhirifu kuliko wengine kwenye mikahawa, wao wanaagiza chakula kingi na kutochukua chakula kinachobaki kwenda nacho nyumbani.

Kwa kawaida wafanyabiashara wanapenda kuonesha ukarimu mkubwa wanapowakirimu marafiki zao, na wanafamilia wanapokula chakula kwa pamoja mikahawani kuwa wanazingatia kuokoa pesa.

Katika mwaka mpya wa Kichina ambao ilikuwa tarehe 29, Januari mwaka huu, asilimia kati ya 80 na 90 ya watu wa familia mbalimbali waliosherehekea sikukuu hiyo kwenye mkahawa wa Bw. Liu, walichukua chakula walichoshindwa kumaliza na kwenda nacho nyumbani.

Takwimu kutoka kwa mikahawa ya China zinaonesha kuwa, mwaka 2005 thamani ya mauzo ya rejareja ya chakula na vinywaji ilikuwa Renminbi Yuan bilioni 748.6, kiasi ambacho ni asilimia 7 ya pato la taifa. Na mwaka huu kiasi hicho kinatarajiwa kufikia Yuan trilioni 1, ambacho ni sawa na dola za kimarekani bilioni 125.

Ingawa hakuna takwimu za kiserikali, wadau wa sekta ya chakula wanasema Wachina huenda wanapoteza bure Renminbi Yuan bilioni 60, sawa na dola za kimarekani bilioni 7.5 kwa mwaka katika mahoteli na mikahawa mbalimbali kote nchini.

Katika mji wa Shanghai pekee, mikahawa inatoa chakula kinachoachwa kiasi cha tani 1,100 kila siku, na hali hii inaikwamisha China kujenga jamii yenye mazingira mazuri.

Ofisa mmoja wa Ofisi ya ulinzi wa mazingira ya mji wa Shanghai Bw. Shen Yonglin alisema, "Tunaona mikahawa ingefanya kazi kubwa, kwamba inaweza kuwashauri wateja wasiagize chakula zaidi ya uwezo wao wa kula na kuwashawishi waondoke na chakula wanachoshindwa kumaliza."

Kuanzia mwaka 2002, ofisi hiyo ilianzisha kampeni iitwayo "matumizi ya rangi ya kijani" katika mikahawa, kuhamasisha mikahawa isitumie vijiti vya kutumia na kutupa na visanduku vya chakula vyenye vitu vinavyoharibu mazingira.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005, katika mji wa Shanghai kulikuwa na mikahawa ipatayo 43 ambayo inapendelea kuwapendekeza wateja wao wasipoteze chakula na kutumia tu visanduku vya chakula visivyoharibu mazingira, ingawa visanduku hivyo ni vya bei ya juu kwa mara kadhaa kuliko vile vinavyotengenezwa kwa vitu vinavyoharibu mazingira.