Mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone Bwana Desmond de Silva alisema, rais wa zamani wa Liberia Bwana Charles Taylor huenda atasomewa mashitaka kwa mara ya kwanza kwenye mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone tarehe 31, atakuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kufikishwa kwenye mahakama ya kimataifa kutokana na makosa ya kivita.
Bw. Silva alisema katika siku ya kwanza ya kesi yake, Bw. Taylor atasomewa mashitaka dhidi yake, na kuchagua kama anakiri hatia zake au kujitetea. Baadaye kundi la majaji litaanza kushughulikia kesi ya Taylor. Kutokana na utaratibu uliowekwa kwenye sheria ya kimataifa ya makosa ya jinai, kama Bw. Taylor atathibitishwa kuwa na makosa ya kivita, huenda atahukumiwa kifungo cha maisha.
Tangu ashike madaraka ya urais wa Liberia mwaka 1997, Bw. Taylor alikiunga mkono chama cha muungano cha mapinduzi kinachoipinga serikali ya Sierra Leone. Chama hicho kilitumia silaha zilizotolewa na serikali ya Taylor kuzusha vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone, na kusababisha vifo vya watu mia kadhaa. Mwezi Juni mwaka 2003, mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone ilitoa amri ya kumkamata Bw Taylor kutokana na makosa 17, ambayo ni pamoja na hatia ya kivita na hatia ya kupinga ubinadamu katika kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone, na kuomba msaada wa jumuiya ya kimataifa ya polisi wa makosa ya jinai. Mwezi Agosti mwaka 2003, ili kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14 nchini Liberia, jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS ilimtaka Bw. Taylor aende uhamishoni nchini Nigeria. Baadaye mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone iliwahi kuiomba serikali ya Nigeria mara nyingi imfikishe Bw Taylor mahakamani, lakini serikali ya Nigeria ilieleza kuwa haitamrejesha Taylor nchini Liberia hadi Liberia itakapounda serikali iliyochaguliwa na raia na kutoa ombi husika.
Mwezi Januari mwaka huu, rais wa kwanza aliyechaguliwa na wananchi wa Liberia Bi. Ellen Johnson-Sirleaf aliapishwa kushika madaraka. Mwanzoni mwa mwezi March, serikali mpya ya Liberia ilitoa ombi rasmi kwa Nigeria la kumrejesha Taylor, ili ahukumiwe kwenye mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone. Baada ya Nigeria kukubali ombi la serikali ya Liberia, tarehe 27 usiku Bw. Taylor alitoweka katika makazi yake nchini Nigeria. Siku ya pili, jeshi la usalama la Nigeria lilimkamata katika sehemu ya mpaka kati yake na Cameroon na kumkabidhi kwenye mahakama maalum.
Wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi tarehe 30 ilithibitisha kuwa, mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone imetoa ombi kwa mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague ili Bwana Taylor ahukumiwe kwenye mahakama hiyo. Rais Johnson-Sirleaf wa Liberia tarehe 30 pia aliliomba baraza la usalama libadilishe mahali pa kumhukumu Taylor, ili kuhakikisha maslahi ya kudumu ya watu wa Liberia na utulivu na ustawi wa kiuchumi wa nchi hiyo. Kabla ya hapo, Bw. Taylor mwenyewe pia alieleza kupenda kuhukumiwa The Hague kwa kuogopa kulipizwa kisasi na watu wa Sierra Leone.
Wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi ilisema, mahakama ya Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone lazima ipate kibali cha baraza la usalama kuhusu Bw Taylor kuhukumiwa The Hague, na kuhakikisha anaondoka nchini Uholanzi baada ya kuhukumiwa.
Wachambuzi wameona kuwa, sehemu ya Afrika magharibi ilikumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kirefu, sababu moja muhimu ni kuwa baadhi ya mabwana vita walichochea vita hiyo. Kuhukumiwa kwa Bw. Taylor kutakuwa pigo kubwa kwa mabwana vita hao. Kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan alivyosema, jambo hilo litatoa onyo kwa watu watakaokuwa mabwana vita, adhabu ya haki haiwezi kuepukika.
|