Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-03 15:00:22    
Hekalu la Confucius, mnara wa ngoma na ukumbi wa shirikisho la wafanyabiashara wa Guangdong mjini Tianjin

cri

Mji wa Tianjin uko kusini ya Beijing kwa umbali wa muda wa saa mbili hivi kwa safari ya gari, mji huo umekuwa na historia ya miaka mia sita. Tianjin ni mji wa kale wenye kumbukumbu nyingi za utamaduni, kwa sababu mjini humo watu wanaweza kuona michezo ya aina mbalimbali ya jadi, vitu na majengo mengi ya kale.

Mahekalu ya Confucius yako katika sehemu nyingi nchini China, kwa sababu katika siku za kale mahekalu hayo yalikuwa ni mahali pa watu kumfanyia tambiko Confucius ambaye ni mwanafikra na mwanaelimu wa China ya kale, na pia ni mahali pa kuandaa wasomi katika zama za kale. Kwa mujibu wa takwimu, hapa duniani kuna mahekalu ya Confucius zaidi ya 2,000, lakini yaliyohifadhiwa vizuri hadi leo ni kiasi cha 300, hekalu la mjini Tianjin ni moja kati ya mahekalu hayo.

Helalu la Confucius ni kundi la majengo ya kale mjini Tianjin, jengo muhimu katika kundi hilo ni ukumbi wenye paa la vigae vya rangi ya njano. Mkuu wa makumbusho ya hekalu hilo la Confucius Bi. Chen Tong alieleza kuwa, watu wakitembelea hekalu hilo watafahamu jinsi watu wa kale walivyojipatia nyadhifa za serikali. Anasema,

"Katika zama za kale, ni watu waliosoma tu katika hekalu hilo yaani shule ya kiserikali, ndio walioweza kuwa na nafasi ya kuendelea zaidi na masomo yao na kushiriki katika mtihani wa taifa, mtu aliyekuwa wa kwanza katika mtihani wa taifa ndiye aliyepata wadhifa."

Bila shaka, hivi sasa hekalu hilo sio tena shule bali limekuwa mahali pa watu kumfanyia Comfucius tambiko na sehemu ya utalii. Kila mwaka katika majira ya Spring na Autumn watu hufanya tambiko kubwa huko, kwa sababu katika nyakati hizo ni siku za maadhimisho ya Confucius ya kuzaliwa au kufariki. Shughuli za tambiko zinafanyika kwa utaratibu maalumu, kwamba kiongozi wa shughuli hizo anavaa nguo rasmi ya kiofisa, anasoma risala ya tambiko na kuiwasha moto na katika kila hatua ya shughuli hizo kabla ya hatua nyingine watu lazima wapige magoti. Watalii wakitaka kufahamu jinsi utamaduni wa kale unavyokuwa, ni afadhali waende wenyewe kushuhudia shughuli hizo.

Karibu na hekalu hilo kuna mnara mmoja wa ngoma uliojengwa katika karne ya 14, mwanzoni mwa Enzi ya Ming. Ingawa mnara huo unaitwa mnara wa ngoma lakini kwa kweli ni mnara wa kengele. Historia ya mnara huo ilikuwa na matuko mengi. Naibu mkuu wa makumbusho ya mnara huo Bi. Yin Hua alieleza kuwa, mnara huo uliwahi kujengwa mara mbili na kubomolewa mara mbili. Anasema,

"Mwaka 1900 baada ya jeshi la muungano wa nchi nane za Magharibi kuukalia mji wa Tianjin, walibomoa kuta za mji huo katika mwaka wa pili. Wakati huo, ingawa mnara wa ngoma haukubomolewa, lakini uliharibiwa vibaya hata msingi wake ulididimia. Mwaka 1921 mnara huo ulifanyiwa ukarabati, sura yake ikaonekana nzuri zaidi kuliko mnara wa zamani na paa lale liliezekwa kwa vigae vya rangi ya kijani, na ilikuwa na urefu mkubwa zaidi. Baada ya ukombozi, kutokana na ujenzi wa mji, barabara iliyokuwa nyembamba ilipanuliwa, mnara huo ulibomolewa mwaka 1952, kisha mwaka 2000 ulijengwa tena mahali ulipokuwepo zamani ili kuenzi utamaduni wa taifa mjini Tianjin."

Mnara wa sasa sio wa awali bali ni mnara uliojengwa mwaka 2000 kwa mujibu wa ule wa zamani, lakini umejengwa kwenye msingi imara na umeongezwa urefu kutoka ghorofa tatu hadi ghorofa tano, na kengele imebadilishwa kuwa kengele ya shaba nyeusi yenye uzito wa tani tatu, watalii wanaweza kugonga, na sauti yake kubwa ikasikika kote mjini.

Baada ya kuwaeleza kuhusu hekalu la Confucius na mnara wa ngoma, sasa tuwafahamisheni mahali pa kutazama opera ya Kibeijing mjini Tianjin, hapo ndio ukumbi wa zamani wa shirikisho la wafanyabiashara wa Guangdong lilipokuwa.

Ukumbi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Guangdong ni kundi la nyumba za chini, pembezoni kuna kuta ndefu. Nyumba hizo zimeonesha mtindo wa nyumba za Kiguangdong na pia zimeonesha juhudi kubwa za wafanyabiashara wa Guangdong wanaoishi mjini Tianjin. Kiasi cha miaka 300 iliyopita, wafanyabiashara wa mikoa ya Guangdong na Fujian walikuja mjini Tianjin kwa meli kutoka kusini mwa China, baada ya miaka mingi wafanyabiashara hao walijichangia fedha na kujenga ukumbi huo, ambapo huko walikuwa wakiwasiliana, kuwekeana urafiki, kusaidiana na kutatuliana migogoro kati yao.

Jengo linalostahili kutajwa ni jumba la opera. Hilo ni jumba kati ya majumba machache ya kale yaliyopo nchini China. Ndani yake kuna nafasi za watazamaji kiasi cha mia nane, ghorofani kuna boksi kama chumba, na chini hakuna nafasi maalumu, dari lake lilijengwa kwa magogo matatu makubwa na papi nene zisizohesabika. Naibu mkuu wa makumbusho ya ukumbi huo Bi. Xu Meimei anaeleza,

"Inasemekana kwamba magogo hayo matatu yalitoka kutoka sehemu ya kusini ya China, magogo kama hayo ya kunyooka hayapatikani mpaka miti yenyewe iwe na urefu wa mita arobaini hadi hamsini, hili ni ajabu."

Bi. Xu aliongeza kuwa jukwaa lake lilijengwa kwa ustadi mkubwa, ambalo pande tatu zake ni wazi, watazamaji wanaweza kuangalia michezo kutoka pande zote hizo. Mtalii mmoja wa Ufaransa aliusifu sana usanifu wa jukwaa hilo.

kusikia si kuona, ukiwa na nafasi karibuni Tianjin, uangalie hekalu la Confucius, ugonge kengele kubwa ya mnara na utazame opera ya Kibeijing katika ukumbi huo, uhisi mwenyewe utamaduni mkubwa wenye historia ya miaka mia sita mjini Tianjin.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-03