Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-04 15:01:50    
China na Russia zaimarisha ushirikiano kuhusu nishati

cri

Katika miaka ya karibuni, China na Russia zimeimarisha maingiliano na ushirikiano katika sekta za uchumi na biashara, ambapo kitu kinachofuatiliwa sana katika ushirikiano huo ni ushirikiano kuhusu nishati kati ya nchi hizo mbili. Wiki iliyopita wakati rais Vladimir Putin wa Russia alipofanya ziara China, nchi mbili zilisaini mikataba kadhaa muhimu kuhusu nishati, hatua ambayo ilitoa dhamana muhimu katika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati kati ya China na Russia.

Kwenye mkutano wa kwanza wa viongozi wa sekta za uchumi, viwanda na biashara wa China na Russia uliofanyika hapa Beijing, rais Putin alidokeza mambo muhimu yaliyoko kwenye mkataba wa nishati wa pande hizo mbili.

"Shirikisho la Russia limeamua kujenga mabomba ya kupelekea mafuta ghafi kutoka sehemu ya mashariki ya Siberia hadi bahari ya Pasifiki. Hivi sasa kampuni ya kusafirisha mafuta kwa mabomba ya Russia na kampuni ya mafuta na gesi ya asili ya China zimesaini makubaliano husika, na zitafanya utafiti kuhusu uwezekano wa kujenga tawi la njia ya China ya mabomba ya kusafirisha mafuta. Endapo mradi huo utaweza kutekelezwa, itachangia usafirishaji mafuta ya asili ya petroli kwa China. Sekta nyingine yenye mustakabali mzuri wa maendeleo ni ushirikiano wa gesi ya asili. Kampuni ya gesi ya asili ya Russia na kampuni ya mafuta ghafi ya China zimesaini nyaraka husika. Hivi sasa tunafanya uchunguzi kuhusu mipango kadhaa ya kutandika mabomba ya gesi ya asili yanayounganisha nchi hizi mbili. Moja ya njia hizo ni ile inayotoka sehemu ya magharibi na Siberia na nyingine ni ile inayotoka sehemu ya mashariki ya Siberia."

Mwaka 2005, Russia ilitoa tani zaidi ya milioni 8 za mafuta ghafi kwa China kwa njia ya reli, kiasi hicho ni kidogo sana ikilinganishwa na jumla ya mafuta inayonunua China kutoka nchi za nje. Hivi sasa sehemu kubwa ya nishati ya Russia inasafirishwa kwa soko la Ulaya, na usafirishaji wake wa mafuta kwa soko la Asia ulikuwa mdogo. Katika miaka ya karibuni, China na Russia zilijitahidi kuwa na ushirikiano mkubwa katika sekta ya nishati, na kujadili kujenga njia moja ya mabomba ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Russia hadi China.

Kutokana na kusainiwa kwa mkataba wa ushirikiano wa nishati wakati rais Putin alipoitembelea China hivi karibiun, mtaalamu wa suala la Russia wa taasisi ya sayansi ya jamii ya China bibi Li Jianmin alisema,

"Uchumi wa China umepata maendeleo ya kasi, sisi tunahitaji mafuta mengi mwaka hadi mwaka, mafuta yetu siyo mengi, hivyo tunahitaji kununua kutoka nchi za nje. Russia ina nishati nyingi, pande hizo mbili zinaweza kunufaika katika eneo hilo. Kusainiwa kwa mikataba ya safari hii, kumeonesha mwelekeo wa ushirikiano kwenye sekta ya nishati katika siku za baadaye, tena ni kupiga hatua halisi."

Mtaalamu huyo alisema kutokana na mikataba iliyosainiwa, baada ya ujenzi wa mabomba ya gesi ya asili kukamilika, Russia itaweza kusafirisha mita za ujazo za bilioni 80 za gesi kwa China kwa mwaka, kiasi hicho ni zaidi ya nusu ya gesi ya Russia inayosafirishwa kwa Ulaya.

Aidha, kumbukumbu ya majadiliano kati ya kampuni ya mafuta ghafi ya China na kampuni ya mafuta ghafi ya Russia kuhusu ujenzi wa tawi la njia ya kusafirisha mafuta ghafi kwa China kutoka Russia, inafuatiliwa sana na kuungwa mkono na serikali za nchi mbili za China na Russia. Meneja mkuu wa kampuni ya mafuta gjafi ya China Bw. Chen Geng ana imani kubwa kuhusu ujenzi wa njia hiyo ya mabomba, na anataka kushauriana na upande wa Russia na kuhimiza kwa pamoja ujenzi wa tawi la njia ya mabomba ya kusafirisha mafuta kwa China.

"Hivi karibuni, serikali ya Russia imeidhinisha mpango wa ujenzi wa mabomba ya mafuta kutoka sehemu ya mashariki ya Siberia hadi bahari ya Pasifiki, jambo ambalo limeweka msingi wa ujenzi wa mabomba ya mafuta kwa China. Tunapenda kushauriana na Russia na kuhimiza ujenzi wa tawi la njia ya mabomba ya mafuta linalokwenda China."

Mbali na kusainiwa kwa mikataba kuhusu ujenzi wa mabomba ya kusafirisha mafuta na gesi ya asili, China na Russia pia zilisaini makubaliano ya ushirikiano, ambayo nchi hizo mbili zinajenga viwanda vya ubia katika nchi hizo mbili, kufanya ushirikiano wa kutafuta rasilimali ya mafuta nchini Russia, na kusafisha na kuuza mafuta nchini China. Russia imekubali kampuni ya mafuta ya China na kampuni ya mafuta ya Russia kuchimba kwa pamoja mafuta na gesi ya asili nchini Russia. Aidha kampuni za mafuta za nchi hizi mbili zitajenga viwanda vya ubia nchini China na kushughulikia usafishaji wa mafuta na uuzaji wa petroli na bidhaa nyingine za mafuta nchini China.

Mkurugenzi wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya China Bw. Ma Kai amesema, kusainiwa kwa mkataba huo kumekuza sana ushirikiano wa nishati kati ya China na Russia. Alisema, "Tumeona kwa furaha kuwa katika sekta za mafuta na gesi, ushirikiano wa viwanda vya nchi hizo mbili umepanuka kwa kazi za mwanzo za kutafuta mafuta na gesi, na kwa kazi za mwisho za uuzaji. Mwelekeo huo unaonesha kuwa, ushirikiano kwenye sekta ya nishati kati ya China na Russia umekuzwa kwa pande mbalimbali. Kwa mtazamo wa muda mrefu, ushirikiano kwenye sekta ya nishati kati ya China na Russia ungepanuliwa katika maeneo mengi na kwa mitindo mbalimbali, na kujenga uhusiano imara na tulivu wa ushirikiano. Pande mbili zinaweza kukuza ushirikiano wa pande mbalimbali, hususan katika maeneo muhimu ya mafuta, gesi na nguvu ya umeme, pia zinaweza kuwa na ushirikiano katika maeneo ya makaa ya mawe, uendelezaji na matumizi ya nishati mpya pamoja na uokoaji wa nishati."

Wakati wa ziara ya rais Putin nchini China, China na Russia pia zilichunguza kufanya ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia katika maeneo mengi zaidi, si kama tu pande mbili zilisaini mikataba ya ushirikiano kuhusu nishati, uwekezaji, mambo ya fedha na mawasiliano, bali pia zilikuwa na ushirikiano katika kuitisha mkutano wa kwanza wa baraza la viongozi wa sekta za uchumi, viwanda na biashara la China na Russia. Majadiliano hayo yalihusu sera za uwekezaji, ushirikiano wa mambo ya fedha, ushirikiano wa mawasiliano, usafirishaji wa mitambo na zana za umeme kwa nchi za nje na uwekezaji kwa miradi mikubwa.

Rais Hu Jintao wa China alipotoa hotuba kwenye baraza hilo alidokeza kuwa, China na Russia zimethibitisha maeneo muhimu ya ushirikiano wa pande mbili katika siku za baadaye. Alisema, "China na Russia zinatakiwa kuongeza nafasi ya mitambo na zana za umeme katika biashara ya pande mbili na kukuza biashara ya bidhaa za nishati na rasilimali; Kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa vyombo vya umeme vya nyumbani, mawasiliano ya habari, ujenzi wa miundo mbinu na sekta za mafuta na gesi ya asili, misitu, madini na kazi za usindikaji; Kuanzisha ushirikiano na maingiliano katika sekta za safari za anga ya juu, utengenezaji wa mitambo, nishati ya nyukilia, vifaa vipya vya ujenzi, na teknolojia ya viumbe."

Thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili katika mwaka 2005 ilifikia dola za kimarekani bilioni 29.1, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya 30%, pande mbili zimeamua kuongeza thamani hiyo hadi kati ya dola za kimarekani bilioni 60 na 80 mwaka 2010.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-04