
Mkutano wa kwanza wa mawaziri wa baraza la ushirikiano wa maendeleo ya uchumi la China na nchi zilizoko kwenye visiwa vya bahari ya Pasifiki ulifunguliwa tarehe 5 huko Nadi, mji mkuu wa Fiji. Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano, alieleza kwa kirefu sera za China kuhusu nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki pamoja na hatua zinazochukuliwa na China kuhimiza maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki.
China na nchi za bahari ya Pasifiki ziko kwenye sehemu ya Asia na Pasifiki na ni nchi zinazoendelea, hivi sasa zinajitahidi kustawisha uchumi na kukuza maendeleo ya jamii. Mwaka 2005, serikali ya China ilitoa wito wa kuanzisha baraza la ushirikiano wa maendeleo ya uchumi kati ya China na nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki, ili kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na kuleta maendeleo kwa pamoja. Baraza hilo linatoa nafasi muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na nchi hizo. Katika hotuba yake Bw. Wen Jiabao alisema, baraza hilo la ushirikiano wa maendeleo ya uchumi ni muhimu sana katika kuendeleza uhusiano kati ya China na nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki na litakuwa mfano mpya wa kuigwa kwa ushirikiano wa nchi za kusini na kusini.
Alisema China inafuata kwa uthabiti njia ya amani na maendeleo, na inashikilia sera za amani, maendeleo na ushirikiano, inajitahidi kuhimiza amani na maendeleo kwa ushirikiano, na kukuza uhusiano wa urafiki na ushirikiano na nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki kwa msingi wa kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani.
"Kisiasa tunaheshimu utaratibu wa jamii na njia ya maendeleo zinazochagua nchi za visiwa vya Pasifiki kutokana na hali halisi ya nchi hizo, pia tunaheshimu jitihada za nchi hizo katika kulinda mamlaka na uhuru wa kitaifa na kulinda amani na utulivu wa sehemu yao; kiuchumi tunajitahidi kutekeleza lengo la maendeleo ya milenia la Umoja wa Mataifa na kuzisaidia nchi hizo kuimarisha uwezo wao wa kujiendeleza. China siyo nchi tajiri, lakini itaendelea kutoa misaada isiyo na masharti yoyote kwa nchi za visiwa vya Pasifiki. Bw. Wen Jiabao alisema katika mambo ya kimataifa, China inashikilia kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea zikiwemo nchi za visiwa vya Pasifiki, na kuunga mkono madai yao ya haki ya kutumia na kulinda rasilimali za bahari na haki zao za kushiriki kwa usawa mambo ya kikanda na kimataifa.
Bw. Wen Jiabao alisisitiza, kukuza uhusiano wa urafiki na ushirikiano na nchi za visiwa vya Pasifiki siyo sera ya kidiplomasia za muda za China, bali ni sera ya kudumu na ya kimkakati ya serikali ya China. Historia imedhihirisha na itaendelea kuthibitisha kuwa China ni rafiki na mwenzi wa kudumu na kuaminika wa nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki. Aidha alitoa mapendekezo ya kukuza uhusiano kati ya China na visiwa vya bahari ya Pasifiki katika siku za baadaye:
"Kukuza urafiki na ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki ni matarajio ya pamoja ya watu wa pande hizo mbili, na kunaambatana na maslahi ya kimsingi na ya muda mrefu ya pande mbili, na pia kunanufaisha amani na ustawi wa kikanda. Hivyo nashauri China na nchi za visiwa vya bahari ya Pasifiki ziimarishe maingiliano kati ya serikali, mabunge, vyama vya kisiasa na maingiliano ya umma, maelewano na kuaminiana kati yao, kuimarisha mashauriano na ushirikiano katika masuala makubwa ya kimataifa na kikanda, kuunga mkono mambo yanayofuatiliwa na upande mwingine, kuimarisha uungaji mkono kati yao, kushughulikia mahitaji halisi ya nchi za visiwa vya Pasifiki na kuanzisha uhusiano wa aina mpya wa kunufaishana kibiashara na kiuchumi."
Idhaa ya Kiswahili 2006-04-05
|