Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-07 18:16:44    
Suala la uhaba wa wahudumu wa afya lazingatiwa katika siku ya afya duniani

cri

Tarehe 7 Aprili ni siku ya afya duniani. Katika siku hiyo shirika la afya duniani, WHO, limetoa ripoti kuhusu "hali ya huduma ya afya duniani kwa mwaka 2006", ikisema hivi sasa kuna upungufu wa wahudumu wa afya zaidi ya milioni nne duniani. Na upungufu huo unaonekana zaidi katika nchi 57 za kusini mwa jangwa Sahara, Asia na Latin Amerika. Ili kutatua tatizo hilo ripoti imetoa "mpango wa utekelezaji wa miaka 10".

Shirika la Afya Duniani linatoa ripoti kuhusu "hali ya huduma ya afya duniani" kila mwaka. Mada ya siku ya afya duniani mwaka huu ni "nyenzo za wahudumu wa afya" na wito ni "ushirikiano wa pamoja na kuimarisha hali ya afya" ukizitaka nchi zote zilitie maanani utatuzi wa nyenzo za wahudumu afya na kuthamini na kuwaheshimu watu hao. Ripoti hiyo inasema, wahudumu afya ni msingi wa matibabu. Hivi sasa kuna wahudumu milioni 59.2 tu duniani, na kati ya hao theluthi mbili tu wanafanya kazi katika mstari wa mbele, bado kuna upungufu wa wahudumu milioni nne. Watu wasiopungua bilioni 1.3 duniani hawapati matibabu, na kila mwaka watu milioni 10 wanakufa kutokana na maambukizi ya magonjwa na matatizo ya uzazi, kama kungekuwa na wahudumu wengi zaidi, baadhi ya watu hao wangeokolewa.

Ripoti inasema katika nchi zinazoendelea na hasa sehemu za vijijini hali ya upungufu wa wahudumu afya ni mbaya zaidi. Hali hiyo inaonekana mbaya zaidi katika nchi 36 za kusini mwa jangwa la Sahara, nchi 16 za Asia na nchi 5 za Latin Amerika. Kwa kuwa nchi zilizoendelea pia zina upungufu wa wahdumu afya, mathalan, Marekani ambayo ina upungufu wa wauguzi kiasi cha laki 1.25, kwa hiyo wahudumu afya wa nchi zinazoendelea wanakimbilia kwenye nchi zilizoendelea. Kwa mujibu wa takwimu, wahudumu afya wa nchi za Afrika kiasi cha robo wanakimbilia kwenye nchi zilizoendelea.

Ripoti inapendekeza kuwa kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2015 "mpango wa utekelezaji wa miaka 10" utekelezwe, ili kuandaa wahudumu afya wengi zaidi. Na serikali za nchi zote zinapaswa kutilia maanani kuandaa wahudumu afya na kuboresha mfumo wa usimamizi na kuongeza fedha na kupanua wigo wa kukusanya fedha. Nchi 57 zinazoendelea ambazo zina upungufu mkubwa wa wahudumu wa afya zinapaswa kuongeza dola za Kimarekani 10 kwa kila mkazi na kila mwaka.

Kadhalika ripoti imesema kuwa, ushirikiano mkubwa wa nchi zote ni wa lazima ili kutatua tatizo la upungufu wa wahudumu afya. Na nchi zilizoendelea zinapaswa kutunga sheria za kutowaajiri wahudumu afya kutoka nchi zinazoendelea, na kupendekeza kuwa msaada wa kimataifa ni wa lazima katika kusaidia nchi zinazoendelea kwenye juhudi za kuandaa wahudumu afya.

Idhaa ya Kiswahili 2006-04-07