Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-07 19:53:37    
Shirikisho la wafanyabiashara wa China na Afrika

cri

China ni nchi kubwa kabisa inayoendelea duniani, Afrika ni bara lenye nchi nyingi zaidi zinazoendelea duniani, China na nchi za Afrika zote zinakabiliwa na majukumu ya kuendeleza uchumi, na kuboresha maisha ya watu wao. Hivyo kutokana na msingi wa urafiki mkubwa wa jadi uliopo kati ya watu wa China na nchi za Afrika, kuimarisha ushirikiano ili kupata maendeleo kwa pamoja, si kama tu ni matokeo ya lazima ya kihistoria, bali pia ni matakwa ya pamoja ya watu wa China na nchi za Afrika katika zama mpya.

Katika miaka ya karibuni, thamani ya biashara kati ya China na Afrika imeongezeka kwa haraka, na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, thamani hiyo iliongezeka mara 15. Lakini hata hivyo hivi sasa kiasi cha jumla ya biashara kati ya China na Afrika bado kinachukua asilimia 2-3 tu ya thamani yote ya biashara ya China, na jambo hilo limeonesha kuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika bado una uwezo mkubwa na nafasi nyingi za kuendelezwa.

Kwa hali hiyo ilivyo Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Kituo cha Mawasiliano ya Uchumi na tekinolojia cha Kimataifa cha China na Shirikisho la Kuhimiza Shughuli za hisani ya China zilianzisha Shirikisho la Wafanyabiashara wa China na Afrika tarehe 17 Machi mwaka 2005, na ofisi ya sekretarieti ya shirikisho hilo ilianza kufanya kazi rasmi tarehe 25 Agosti mwaka jana.

Hadi leo Shirikisho la Wafanyabiashara wa China na Afrika limeanzisha ofisi katika Nigeria, Ghana, Tanzania, Msumbiji, Cameroon, Kenya na nchi nyingine. Ofisi hizo zitajitahidi kuanzisha ushirikiano na wafanyabiashara wa nchi hizo, kuhimiza serikali za nchi hizo kuunga mkono uwekezaji wa makampuni ya China, na kuyasaidia makampuni ya China kuchagua sekta mwafaka za kuwekeza, ili kuweka mazingira mazuri kwa makampuni ya China kufanya biashara na kuwekeza huko Afrika.

Licha ya ofisi za makao makuu yake hapa Beijing, Shirikisho la Wafanyabiashara wa China na Afrika pia litaanzisha ofisi katika mji wa Shanghai, na mikoa mingine nchini China.

Kauli mbiu ya Shirikisho la wafanyabiashara wa China na Afrika ni kuyaongoza makampuni binafsi ya China kuendeleza raslimali za Afrika, kufungua soko la Afrika, kuanzisha mtandao mzuri wa mawasiliano kati ya washirika wa China na nchi mbalimbali duniani, kuweka hali nzuri ya kuhimiza mawasiliano na ushirikiano wa uchumi na teknolojia kati ya China na Afrika, na kuhimiza ushirikiano kati ya China na Afrika, na ushirikiano kati ya kusini na kusini kwa njia ya kufuata ufanisi mzuri.

Shughuli muhimu zitakazofanywa na Shirikisho la Wafanyabiashara wa China na Afrika ni kama zifuatazo:

Ya kwanza ni kutoa huduma za upashanaji habari. Yaani kutoa huduma za upashanaji habari kwa makampuni ya China kwenda nchi za Afrika na makampuni ya Afrika kuja China kuanzisha shughuli, kuwaandalia mafundi na kufanya shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa njia za kisasa za mtandao wa Internet na tarakimu.

Ya pili ni kuhimiza mawasiliano ya kibiashara. Kutoa mafunzo kwa wanachama wa shirikisho hilo kufanya ukaguzi wa kibiashara katika nchi za Afrika, kuwapokea ujumbe husika kutoka nchi za Afrika na mashirika ya kimataifa kutembelea China, kuanzisha na kukuza njia za mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika.

Ya tatu ni kufanya shughuli za aina mbalimbali kama vile kuandaa semina na makongamano husika, ili kuwapa wanachama fursa za kujifunza na kubadilishana uzoefu na kuinua uwezo wa wanachama wa kutatua matatizo.

Ya nne ni kulinda haki na maslahi halali ya wanachama, kuimarisha kusuluhisha migongano na migogoro kati ya wanachama.

Kuanzia kati kati ya mwezi March hadi mwanzoni mwa mwezi Aprili, Shirikisho la wafanyabiashara wa China na Afrika limeunda ujumbe kufanya ukaguzi wa kibiashara katika nchi nne za Kenya, Uganda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kukagua hali ya uwekezaji na ya kijamii, miundo mbinu na soko la nchi hizo nne, kufanya mazungumzo na mashirika husika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko katika nchi hizo nne, mashirikisho ya wafanyabiashara, idara za uhimizaji uwekezaji za nchi hizo nne ili kutafuta miradi mizuri ya kuwekezwa au kufanyiwa ushirikiano. Ujumbe huo pia umeanzisha uhusiano mzuri na balozi za China zilizoko katika nchi hizo nne, jumuiya za wachina wanaoishi nchini humo na mashirika yaliyowekezwa na wachina wanaoishi humo, na kufanya maandalizi ya kuanzisha ofisi zake katika nchi hizo nne.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-07