Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-07 19:53:08    
Jinsi waandishi habari wa Kenya waionavyo China

cri

Tarehe 5 mwezi Aprili, mwandishi habari wa Kenya Times Bwana Wyclefe Asalwa Salano na mwandishi habari wa East African Standard Bwana Martin Mutua walitembelea jengo la Radio China Kimataifa, na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Baada ya kutembelea ofisi za idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kufahamiana na wafanyakazi wa idhaa ya Kiswahili na kuona utendaji wao wa kazi, pia walipata nafasi ya kwenda studio na kutoa maoni yao kuhusu wanavyoiona China kwa macho yao wenyewe, kuanzishwa kwa kituo cha CRI FM huko Nairobi, Kenya na kuhusu ziara ya rais Hu Jintao wa China anayotarajia kuifanya huko nchini Kenya.

Bw. Wyclife Asalwa Salano alisema, "mambo mengi kuhusu China tuliyapata kupitia vyombo vya habari vya nchi za magharibi, na picha ambayo tumekuwa nayo kuhusu China ni tofauti na ile tunayoiona tulivyofika hapa nchini China. Kwa mfano tunafahamu mgogoro kuhusu Taiwan kutoka vyombo vya habari vya nchi za magharibi, lakini baada ya kufika China, tumeelezewa na maofisa wa serikali wa nchi hii, tumeona kuwa siyo mambo kabisa ya mgogoro kama tunavyosikia, bali kama ni mambo ya ndugu waliokorofishana, ni na picha ambayo tunaelezewa tukiwa kule Afrika kupitia vyombo vya habari vya nchi nyingine.

Kuna mambo mengi tuliyokuwa tunadhani tunafahamu kuhusu China tukiwa huko Afrika, lakini tulipokuja hapa China tumeona kuwa mambo hayo hayapo, habari tulizosikia kutoka kwenye vyombo vingine vinavyosikika huko Afrika siyo habari mwafaka. Nimefurahi kuona kazi inayofanywa na serikali ya China ya kuwapanua mawazo waafrika ili waendelee kujua mengi kuhusu nchi ya china."

Bw. Martin Mutua alisema: "Kwa kweli picha tunayopokea kutoka kwenye vyombo vingine vya habari huko kwetu Kenya kwa kweli ni tofauti kabisa na hali ambayo tumejionea wenyewe hapa China. Ni vizuri kwa kuwa sisi wenyewe tumefika hapa, tumeona kuwa wachina ni watu wazuri, na wametupokea kwa ukarimu."

"Leo mchana tumezungumza na wanafunzi wa nchi za nje wanaosoma katika chuo kikuu cha Beijing, nao pia wametuelezea hali kuhusu maisha yao hapa China, na tumeona kuwa wanaendelea vizuri na masomo, ingawa wanapata shida kidogo kutokana na lugha ya Kichina, kwa hiyo wanajaribu sana kujifunza kichina, tumeona kuwa mambo mengine yote yanaendelea vizuri."

"Kabla ya kufika hapa, mimi nilijua kuwa katika China nzima kuna tatizo kubwa kabisa la homa ya mafua ya ndege, na kwa kweli hayo yote mpaka sasa bado sijaona. Wakati wa mchana tulikula kuku, na hakukuwa na tatizo lolote. Kwa kweli ni makosa kutegemea vyombo vingine vya habari vinavyotueleza mambo ya China. Ni vizuri kwamba sasa kumeanzisha kituo cha kurusha matangazo nchini Kenya, ambacho kitaweza kutoa habari sahihi, na ni vyema tuachane na kasumba ya mambo kutoka vyombo vingine."

Waandishi hao wawili walisema ingawa hawana muda mwingi wa kusikiliza radio kutokana na wao kuwa ni wafanyakazi wa magazeti, lakini wakifika nyumbani watajaribu kusikiliza vipindi vya Radio China Kimataifa ili kupata habari sahihi kuhusu China.

Kuhusu uhusiano kati ya China na Kenya na ziara ya rais Hu Jintao ya hivi karibuni nchini Kenya, waandishi habari hao walisema, wananchi wa Kenya sasa wamechoshwa na sera za nchi za magharibi, na wanaangalia na kufuatilia hii ziara ya rais Hu kwa umakini kabisa, na matarajio yao ni kwamba kutokana na ziara hiyo wanaweza kupata mwelekeo mpya ambao utawaletea nafuu, ili angalau wananchi wa Kenya wapate sera mpya za kuwanufaisha wananchi wengi, kwa hivyo hii ziara ya rais inasubiriwa kwa hamu na wana matumaini kuwa itakuwa na matokeo mazuri.

Pia wanatumai kuwa, ziara hii ya Rais Hu Jintao nchini Kenya itaimarisha uhusiano uliokuwepo kati ya Kenya na China, na kuwatia motisha watu wa Kenya na China kuwa wanapaswa kufanya kazi pamoja na kuelewana kwa sababu wanapaswa kuishi kwa pamoja.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-07