Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-10 14:58:05    
Mwimbaji mashuhuri Li Shuangjiang

cri

Bw. Li Shuangjiang alizaliwa mwaka 1939 mjini Harbin, kaskazini mashariki mwa China. Alipokuwa katika shule ya msingi mara nyingi alipata tuzo katika maonesho ya michezo ya sanaa ya miji na mikoa. Alipohitimu sekondari, alijiunga na chuo kikuu cha matibabu bila kufanyiwa mtihani kutokana na matokeo mazuri ya masomo yake mazuri ya sekondari, hilo alilokuwa nalo baba yake kwa miaka mingi. Lakini Li Shuangjiang alitaka kuacha nafasi hiyo na kutaka kujiunga na chuo kikuu cha muziki kutokana na kupenda sana muziki. Nia yake ilipingwa sana na baba yake, lakini kutokana na kuungwa mkono na mama yake alijiandikisha kisirisiri kwenye mtihani wa kujiunga na chuo kikuu cha muziki na alipokelewa kutokana na matokeo yake mazuri.

Katika muda wa miaka minne wa masomo yake katika chuo kikuu cha muziki, Li Shuangjiang alimaliza masomo yake ya nadharia ya uimbaji na ustadi wa kuimba, licha ya kuwa alijifunza uimbaji wa Kimagharibi, pia alijifunza uimbaji wa Kichina, alidhamiria kuzifanya nyimbo za China zipendwe zaidi na Wachina. Mwaka 1963 Li Shuangjiang alihitimu masomo yake na kupewa kazi katika Kundi la Kijeshi la Michezo ya Sanaa mkoani Xinjiang, akaanza maisha yake ya sanaa jeshini. Katika miaka kumi alipokuwa mkoani Xinjiang alijiendeleza zaidi kwa kujifunza kutoka kwa utamaduni na sanaa za makabila madogo madogo mkoni humo. Alisema, "Nilifurahi sana nilipokuwa mkoani Xinjiang. Kwa sababu, kwanza napenda maisha ya jeshini, pili napenda utamaduni na sanaa za makabila madogo madogo. Katika miaka kumi nilipokuwa huko Xinjiang nilikuwa kama nasoma katika chuo kikuu cha makabila madogo madogo. Kwa kuunganisha pamoja sanaa niliyojifunza kwa watu wa makabila madogo madogo na niliyopata katika chuo kikuu, uimbaji wangu ulikuwa umeinuka sana."

Mwaka 1970 Bw. Li Shuangjiang alishiriki kwenye maonesho ya michezo ya sanaa ya kijeshi, kwa wimbo wake "Sifa kwa Beijing" alipata tuzo ya kwanza, na baadaye aliimba nyimbo nyingi ambazo zilijulikana sana kutokana na kuimbwa naye. Mwaka 1973 Li Shuangjiang alipata uhamisho wa kuja mjini Beijing kwenye Kundi la Opera la Jeshi akiwa mwimbaji.

Baada ya kuja Beijing, Li Shuangjiang alipata ufanisi mkubwa zaidi, kwamba alitoa santuri nyingi za nyimbo zake, nakala zaidi ya milioni tatu za wimbo wake alioimba katika filamu ya "Nyota Nyekundu Inayomelemeta" ziliuzwa, na nyimbo zake nyingine za "Kwaheri Mama" na "Namkumbuka Askari Mwenzangu" zinavutia na zinafahamika sana miongoni mwa watu. Lakini wakati huo ambapo alipokuwa kileleni katika uimbaji wake, maisha yake ya sanaa yakabadilika, kwamba mwaka 1994 alihamishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Sanaa mjini Beijing akiwa mkurugenzi wa idara ya muziki. Bw. Li Shuangjiang anasema, "Mwaka 1994 nilipata uhamisho na kuja kwenye Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Sanaa nikiwa mkurugenzi wa idara ya muziki, jukumu langu lilikuwa jipya, ambalo nitatumia elimu na uzoefu nilioupata kwa miaka mingi kuwafundisha wanafunzi wangu na kuwafanya wawe waimbaji waliopata mafanikio makubwa kwa njia ya mkato."

Li Shuangjiang alipoanza tu kazi yake katika idara ya muziki mara alifanya mageuzi ya ufundishaji. Alianzisha "Jukwaa la Muziki" kwa kufanya maonesho ya muziki mara kwa mara na kufundisha uimbaji hadharani. Kwa kufanya hivyo aliwaletea wanafunzi wake nafasi nyingi za kufanya mazoezi, kiwango chao kiliinuka haraka. Wanafunzi wake wengi walipata tuzo katika mashindano ya waimbaji nchini China na nchi za nje, na ufanisi wake wa ufundishaji ulipata tuzo ya taifa. Hivi sasa, Li Shuangjiang mwenye umri wa miaka 67 amekuwa na wanafunzi waliotapakaa kote nchini na wengi wamekuwa mashuhuri katika nyanja za uimbaji.

Mwanafunzi wake ambaye kwa sasa ni mwalimu wa uimbaji Bw. Li Shuangsong anaona kuwa Li Shuangjiang sio tu anaimba vizuri bali pia ana utaalamu mkubwa wa kufundisha, na ameridhishwa na jinsi alivyo makini katika ufundishaji wake. Anasema, "Wakati tulipowatahini wanafunzi au tunapofanya maonesho ya muziki, maneno aliyosema kwa mara nyingi ni kuwa: Unapokuwa jukwaani lazima uwe umewaka kwa hisia zako. Maneno hayo yanamaanisha kuwa tunapoimba lazima tuimbe kwa hisia za kweli."

Bw. Li Shuangjiang mbali na kujizamisha katika shughuli zake za ufundishaji, naye pia anashughulika kuhariri historia ya muziki wa kijeshi na mara kwa mara alialikwa kuwa mwamuzi katika mashindano ya waimbaji na kufanya juhudi za kugundua waimbaji hodari. Alipokumbuka miaka zaidi ya arobaini ya maisha yake ya sanaa, Li Shuangjiang alisema, anatumai kupanda mbegu nyingi zaidi katika ardhi ya usanii na kuvuna mavuno mazuri ya matunda.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-10