Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-11 16:58:39    
Barua 0409

cri

Msikilizaji wetu Makoye Mazoya wa sanduku la posta 200, MAGU Mwanza Tanzania ametuletea barua akisema, anapenda kutoa pongezi nyingi kwetu kwa mafanikio tuliyoyafikia katika kujenga kituo cha FM huko Nairobi Kenya. Madhumuni ya barua hii ni kutujulisha kuwa yeye ni mwanachama wa Redio China kimataifa, na kwa sasa huko Magu hawawezi kusikiliza vizuri matangazao ya Radio China kimataifa, hali hii imemfanya akose kusikia vipindi vingi sana.

Anasema anatushukuru sana kwa kalenda na bahasha tuliyomtumia, pia na anatupongeza kwa kuboresha huduma zetu za kuimarisha uhusiano kati ya Afrika na China kwa mawasiliano ya kiufundi, Miundo mbinu na Misaada isiyo kuwa na masharti ya kisiasa. Yeye msikilizaji wetu anaposikia yote haya, anapata furaha sana na anatuomba tunawaajiri kufanya kazi, kwani mafanikio hayaji bila kufanya kazi kwa bidii.

Tunamshukuru sana Bwana Makoye Mazoya kwa barua yake, ingawa hawezi kusikiliza vizuri matangazo yetu, lakini anaendelea kutufuatilia na kutuhimiza tufanye bidii ili kuboresha matangazo yetu. Tunaahidi kuwa tutafanya juhudi za kuwawezesha wasikilizaji wetu wapate usikivu mzuri zaidi wa matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Maluha Martin Eagi wa Kitunda Relini sanduku la posta 2203 Dar es Salaam Tanzania ametuletea barua akisema, Jamani mambo ni moto moto hapo nchini. Anaamini kuwa tunaendelea vizuri na kuzidi kuwaandalia vipindi vizuri na vilivyopangika, wasikilizaji wanaoipenda Radio China kimataifa. Anasema lengo kuu la barua hii ni kutoa pongezi kwa uongozi wote wa Radio China kimataifa. Jambo kubwa ambalo angependa kuipongeza Radio China kimataifa ni kuhusu kuzidi kutafuta mbinu mbalimbali na jitihada zote kuwawezesha wasikilizaji watupate vizuri katika matangazo yetu.

Anasema amefurahishwa sana na barua tuliyomwandikia ikimwarifu kuwa tunafanya mikakati ili matangazo ya idhaa ya kiswahili ya redio China Kimataifa yaanze kusikika kupitia redio Tanzania na sauti ya Tanzania Zanzibar, kwa kweli kwa upande wake amefurahishwa na taarifa hiyo, kwa sababu wamekuwa wakishindwa kuyapata matangazo yetu vizuri, wanayasikia kwa taabu redioni, anasema kutokana na sababu hiyo wanachama wake wamekuwa wakimfuata na kumwuliza, mbona matangazo yetu hayasikiki vizuri? kwa kweli amekuwa akishindwa kuwajibu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawasaidia sana.

Pia anapenda kutupongeza kwa kufungua kituo cha kurushia matangazo yetu huko Nairobi Kenya, anatuombea tuzidi kuifanikisha mipango yetu yote ambayo tunaipanga kwa ajili ya wasikilizaji wetu. Anasema kwa kweli tumeonesha ni jinsi gani tunavyowajali wasikilizaji wetu, hivyo wanatushukuru sana.

Tunamshukuru kwa dhati Maluha Martin Eagi kwa barua yake. Kweli kila mara tumepata barua za wasikilizaji wetu wa Tanzania ambao wanalalamika juu ya usikivu mbaya wa matangazo yetu. Tumetoa ripoti kwa ofisi husika ya CRI, wahusika wametuambia kwamba wanajitahidi kuboresha usikivu, na pia tunatafuta njia ya ushirikiano na Radio Tanzania au Radio ya Zanzibar ili kusaidia kuboresha usikivu wa matangazo yetu, tunaahidi tutafanya chini juu ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff wa sanduku la posta 172, Bungoma Kenya anasema katika barua yake kuwa, anafurahi kutuandikia barua hii, kutokana na jinsi alivyoshuhudia uzinduzi rasmi wa kituo cha FM cha Radio China kimataifa sehemu ya Limuru, Nairobi Kenya. Furaha yake kubwa ni kubahatika kukutana na marafiki ambao ni Mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian, wahariri mbalimbali wa idhaa ya CRI, balozi China hapo Kenya Bw. Guo Chongli, na wengineo. Kwa kinaga ubaga hii ni jambo halisi kati ya uhusiano mzuri uliopo kati ya China na Kenya.

Anasema hana budi kumpongeza Bi. Du Shunfang kwa roho nzuri kuweza kumshughulikia, haswa kumfahamisha kwa mkuu wa Radio China kimataifa, balozi na wahariri wengine we China, kulingana naye hii itakuwa historia katika maisha yake. Alifurahia pia kwa vile alipewa nafasi ya kuhojiwa na waandishi wa habari wa Radio China kimataifa pamoja na wahariri wa kituo cha utangazaji na wale wa Televisheni.

Akiweza kuleza kwa ufupi jinsi sherehe ilivyokuwa, kwa kweli mambo hufanyika hapa duniani mabaya au mazuri, lakini kwa jambo ambalo Radio China Kimataifa imelifanya kwa wakenya, ni jambo la maana na la sifa nzuri kupita kiasi. Anasema hivyo kwa sababu, kutokana na alivyotazama aina ya mitambo ambayo iliyokabidhiwa kwa idhaa ya KBC ni ya hali ya juu, yenye nguvu na yenye gharama ya mabilioni ya pesa.

Haya yote anasema kwani ameyaona kwa macho yake na ana haja ya kuyasema kama aliyoyaona. Kwa hivyo anasema ni lazima atoe pongezi kwa serikali ya China pamoja na idhaa kiswahili ya Radio China kimataifa, na kwa mkuu wa radio China kimataifa kwa kupata nafasi ya kuzuru Kenya. Hii imemfanya azidi kuamini kuwa China ni nchi ya kujenga wala sio ya kubomoa. Kwa ishara ya kukata utepe mwekundu uliokuwa na maandishi ya CRI na KBC, inalingana na ishara ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya China na Kenya. Anasema ana uhakika wakenya na wachina pia wataunga mkono jambo hili na kuanza kufunga pingu za maisha kwenye uhusiano wa watu wa nchi hizo. Na tena ni jambo la busara iwapo tutaitikia mwito wa shairi la kichina lisemalo "hata kama majirani wanaweza kuishi mbali, hawawezi kutenganisha urafiki wa kweli"

Kwa kufanya hivyo watakuwa na uhusiano usioweza kutenganishwa, kwa vile ndoa nayo ni jambo ambalo ni kazi ya mungu. Na hakuna anayeweza kutenganisha. Pia anasema moyoni mwake anawapenda wachina, amefurahishwa na vitendo vyao, amefurahia uhusiano na mipango yao kwa wamanchi wa Kenya, anatamani na hamu kwamba kama kusingekuwa na bahari na milima, basi angeanza safari ya kutembea kwa miguu ili aweze kufika China. Kwani maneno yake na sifa yake mara kwa mara, Radio China kimataifa imewafanya watu wa anakoishi kumpachika jina la Radio China kimataifa na "mingzi" jina Bw. China na "He" na wengine CRI hata "jintian" , na yeye anafurahi sana , kila siku anaomba mola, na atakapopata pesa ya kutosha kwenda ng'ambo ni lazima atafika China kwanza.

Tunamshukuru sana msikilizaji Mutanda Ayub Shariff kwa barua yake ya kutuelezea sherehe ya kuzinduliwa rasmi kwa kituo cha FM cha Radio China kimataifa huko Nairobi Kenya kwa jinsi alivyoishuhudia yeye mwenyewe. Tunashukuru kwa udhati wake kwa idhaa yetu, na ni matumaini yetu kuwa, ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo yake ili kutusaidia kuboresha vipindi vyetu.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-11