Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-13 16:45:18    
Harakati ya "supemaketi za upendo" inawanufaisha wananchi wenye shida za kiuchumi

cri

Katika eneo moja la makazi mjini Nanning, mkoani Guangxi kusini mwa China, kuna soko moja liitwalo "supemaketi ya upendo", bidhaa mbalimbali zinazohitajika katika maisha ya Wachina kama vile chupa za maji, mafuta ya kupikia, pamba n.k. zimejaa kwenye supemaketi hiyo. Lakini hii sio supemaketi halisi, na bidhaa hizo haziuzwi bali zinatolewa bure kwa familia zenye shida kubwa za kiuchumi katika mtaa huo wa makazi uitwao Xinzhu.

Supemaketi hiyo ni sehemu ya harakati ya supemaketi za upendo iliyoanzishwa na serikali ya mji wa Nanning, ambapo serikali inatenga fedha za kuanzisha supemaketi za upendo, viwanda na wafadhili binafsi pia kutoa mchango fulani. Hivi sasa katika mtaa huo wa makazi wa Xinzhu, familia 20 zenye shinda kubwa za kiuchumi zimenufaika na harakati hiyo, na kila familia inapewa bidhaa zenye thamani ya Renminbi Yuan 500 kutoka kwenye supemaketi hiyo ya upendo kwa mwaka.

Katika mtaa huo wa makazi, kuna familia moja ya Tang, hii ni familia yenye watu walemavu na inayopokea pesa za uhakikisho wa maisha kutoka serikalini. Mume na mke wote walikuwa wagonjwa lakini walikosa fedha za kulipia matibabu. Hivi sasa familia hiyo inapata bidhaa nyingi zinazohitajika maishani kutoka kwenye supemaketi ya upendo, na watumishi wa idara mbili za serikali walifadhili pesa ili waweze kutibiwa hospitalini.

Katibu mkuu wa kamati ya chama ya mtaa wa Xinzhu mjini Nanning, Bw. Huang Guobin alieleza kuwa, "Kuna viwanda, idara na watu binafsi wenye nia ya kutoa fadhila, lakini hawajui njia za kutoa fadhila hizo. Na harakati ya 'supemaketi za upendo' imewapa njia mwafaka."

Kuanzia mwaka jana mpaka hivi sasa, supemaketi 114 za upendo zimeanzishwa, ambazo zinalenga kuwasaidia watu wenye shida za kiuchumi katika mitaa mbalimbali ya makazi, kama vile familia zinazotegemea pesa za uhakikisho wa maisha kutoka serikalini, familia masikini, walemavu na watoto wao.

Ofisa anayeshughulikia harakati hiyo Bw. Wei Di alieleza kuwa, watu wenye shida za kiuchumi wanaweza kujaza fomu kutokana na hali halisi za maisha yao, fomu hizo zikishathibitishwa na watumishi husika, watu hao watapewa kadi au tikiti za kupewa bidhaa wanazohitaji kwenye supemaketi za upendo. Kwa watu wenye matatizo ya kutembea, wafanyakazi wa supemaketi za upendo wanapelekea bidhaa nyumbani kwao. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jumla ya familia 1,370 zilikuwa zinapata misaada kwenye harakati hiyo ya supemaketi za upendo, ambapo serikali pia ilitangaza hadharani hali za familia hizo zenye shida za kiuchumi, ili harakati hiyo iwe chini ya usimamizi wa jamii.

Mbali na mji wa Nanning, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Guangxi, harakati ya supemaketi za upendo pia inatekelezwa katika miji mingine mkoani humo. Takwimu zinaonesha kuwa, tangu mwaka 2004 harakati hiyo ilipoanza kutekelezwa mpaka hivi sasa, supemaketi za upendo zipatazo 146 zimeanzishwa mkoani Guangxi, ambapo harakati hiyo ilipata fedha zaidi ya Renminbi Yuan milioni 2, sawa na dola za kimarekani laki 2 na elfu 50, zikiwa ni pamoja na pesa zilizotengwa na serikali na zilizofadhiliwa na jamii. Kwa jumla familia zaidi ya elfu 5 zenye shida za kiuchumi zilipata misaada.

Mbali na kutoa misaada ya bidhaa, harakati hiyo ya supemaketi za upendo imeendelezwa na kuwa na huduma mpya mbalimbali. Supemaketi kadhaa za upendo zimewapatia watu wenye shida za kichumi kadi zenye nambari za simu za watu wanaojitolea, ambao ni pamoja na madaktari, mawakili na polisi, kwa hiyo wakitaka misaada ya wanaojitolea wanaweza kuwapata kwa kupiga simu wakati wowote. Na baadhi ya supemaketi za upendo hata zinawasaidia watu wenye shida za kiuchumi kwa kuwapatia nafasi za ajira, teknolojia na ujuzi, na misaada ya kisaikolojia.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-13