Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-13 16:48:45    
Hifadhi ya utamaduni wa makabila madogomadogo nchini China

cri

China ni nchi yenye makabila madogomadogo yapatayo 55, kila kabila lina utamaduni maalumu. Utamaduni wa jadi ni kielelezo cha kabila, lakini sambamba na maendeleo ya uchumi na jamii, utamaduni huo ni rahisi kupotea kama ukikosa hifadhi mwafaka. Kwa hiyo hifadhi ya utamaduni wa jadi wa kikabila, siku zote inapewa kipaumbele katika maeneo wanayoishi watu wa makabila madogomadogo.

Mkoa wa Yunnan ulioko mpakani kusini magharibi ya China, ni mkoa wenye makabila madogomadogo mengi kuliko mikoa mingine, ambapo wanaishi watu wa makabila madogomadogo 25. Na watu wa makabila 16 kati ya hayo pia wanaishi katika nchi za Myanmar, Thailand na Laos zinazopakana na mkoa wa Yunnan.

Naibu mwenyekiti wa Shirikisho la sanaa za kienyeji la Yunnan Bw. Wang Sidai anatoka kabila la Wayi. Naye anafuatilia shughuli za kuhifadhi utamaduni wa kikabila. Alisema "Katika mwaka 2002, mkoa wa Yunnan ulitangaza Utaratibu wa kuhifadhi utamaduni wa kikabila, kienyeji na wa jadi. Utaratibu kama huo ni wa kwanza nchini China uliotungwa na mkoa kwa ajili ya kulinda urithi wa utamaduni usioonekana."

Alifafanua kuwa, mafanikio mengi yamepatikana katika hifadhi ya utamaduni wa kikabila mkoani Yunnan, kwa vile makabila kadhaa yaliyomo mkoani humo yana idadi kubwa ya watu na maandishi, kwa hiyo yanafanya kazi ya hiari katika hifadhi ya utamaduni, na kazi za hifadhi ya utamaduni pia zilianza mapema. Na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali pia zinasaidia kuleta mafanikio hayo.

Kabila la Wayi ni kabila lenye watu wengi kuliko makabila mengine mkoani Yunnan, kabila hili lina watu zaidi ya milioni 4. Baadhi ya watu wa kabila hilo walihamia katika nchi za Vietnam na Laos mwanzoni. Wayi wana lugha na maandishi yao, pamoja na vitabu maarufu vya kale, vinavyohusu mambo mbalimbali. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, katika wilaya inayojiendesha ya Wayi iitwayo Chuxiong, ambayo wakazi wake wengi ni wa kabila la Wayi, ilianzishwa asasi inayofanya utafiti na kuhifadhi utamaduni wa kabila la Wayi. Asasi hiyo inabeba jukumu la kutafiti vitabu vya utamaduni wa kabila la Wayi pamoja na mila na desturi za watu hao katika siku za kale.

Baada ya kutangazwa kwa Utaratibu wa kuhifadhi utamaduni wa kikabila, kienyeji na wa kijadi mkoani Yunnan, serikali ya mkoa ilifanya uchunguzi juu ya hali ya wanamuziki na wacheza ngoma wa kabila la Wayi. Wasanii wa makumi kadhaa walipewa sifa ya waenezaji wa utamaduni wa Wayi, pia kupata misaada ya fedha. Serikali iliwapa kazi ya kuwafundisha vijana na kuwaelimisha utamaduni wa kabila la Wayi.

Sawa sawa na kabila la Wayi, kabila la Wadai pia ni miongoni mwa makabila yenye watu wengi mkoani Yunnan, kabila hilo lina watu zaidi ya milioni 1.1. Vile vile watu wa kabila la Wadai wanatapakaa kwenye sehemu mbalimbali katika nchi za Thailand, Vietnam, Myanmar na Laos zinazopakana na China.

Kabila la Wadai linajulikana kwa uhodari wa kuimba nyimbo na kucheza ngoma. Katika shughuli za kuhifadhi utamaduni wa kabila hilo, serikali ya mkoa wa Yunnan inajitahidi kufanya ushirikiano na nchi za Kusini Mashariki ya Asia. Kwa mfano mkoa wa Yunnan uliandaa kongamano la kimataifa la utamaduni wa kabila la Wadai, na ulishiriki kwenye tamasha la sanaa na utamaduni la mto Mekong lililofanyika huko Chiang Rai, nchini Thailand.

Mwaka jana wilaya ya Xishuangbanna wanakoishi watu wengi wa kabila la Wadai ilichapisha kitabu cha Orodha ya majina ya kwanza ya aina za utamaduni wa kikabila na kienyeji zilizohifadhiwa. Katika kitabu hicho, ziliorodheshwa sanaa na sikukuu za kabila la Wadai, zikiwemo uchongaji, picha za ukutani, ufundi wa kutengeneza miavuli, sikukuu ya kumwagiana maji na desturi ya mtu ya kutafuta mwalimu. Aidha, serikali ya wilaya hiyo iliwateua wasanii wazee zaidi ya 50 wa kabila la Wadai kuwa warithi wa utamaduni wa kikabila na kienyeji.

Naibu mwenyekiti wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la wilaya hiyo Bw. Zheng Peng alifahamisha kuwa, katika miaka ya karibuni serikali ya wilaya hiyo ilichukua hatua kadhaa za kuwahamasisha wanavijiji wahifadhi na kujenga makazi ya mtindo wa jadi wa kabila la Wadai.

 Nchini China kuna makabila 22 amabayo kila moja lina idadi ya watu isiyozidi laki moja. Kabila la Wabulang mkoani Yunnan na kabila la Wajing mkoani Guangxi ni miongoni mwa makabila hayo. Kwa kuwa makabila hayo yana watu wachache wanaoishi katika maeneo madogo, ni rahisi kwao kuathiriwa. Mbali na hayo, yanakosa uwezo wa kuhifadhi utamaduni na urithi wa kikabila, kazi za hifadhi ya utamaduni na urithi wa makabila hayo zinakabiliwa na hali ngumu.

Katika miaka ya karibuni, China iliongeza nguvu ya kuyasaidia makabila hayo yenye watu wachache ili yaweze kujiendeleza. Mwaka jana serikali ya China licha ya kutoa ahadi ya kutenga Renminbi Yuan bilioni 1.6 katika miaka mitano ijayo katika kuunga mkono maendeleo ya makabila hayo, mpango wa kupambana na umaskini ulivishirikisha vijiji zaidi ya 300 ambavyo wanaishi watu maskini wa makabila yenye watu wachache.

Naibu meya wa mji wa Fangchenggang, mkoani Guangxi Bw. Lin Xin wa kabila la Wajing alifurahia hatua hizo, alisema (sauti 5) "Fedha zilizotengwa na serikali kuu kwa ajili ya kabila letu la Wajing ni kiasi cha Yuan milioni 30. Mradi wetu wa kwanza ni kujenga jumba la makumbusho la kabila la Wajing, halafu tutajenga jumba la makumbusho la hali ya viumbe la kabila la Wajing."