Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-13 16:51:08    
Jumuyia ya kimataifa yatoa maoni tofauti kuhusu Iran kufanikiwa kupata uranium safi

cri

Tokea rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad tarehe 11 kutangaza kwamba Iran imefanikiwa kupata uranium yenye kiwango cha usafi 3.5%, pande mbalimbali zinazoshiriki utatuzi wa suala la nyuklia la Iran zinalaani kwa kauli moja, lakini zina maoni tofauti kuhusu namna ya kutatua tatizo hilo.

Msimamo wa Marekani unaonekana mkali zaidi. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice tarehe 12 alisema, tangazo la Tehran limethibitisha kuwa, Iran haikufuata matakwa ya jumyia ya kimataifa, Baraza la Usalama lazima lifikirie kuichukulia Iran "hatua kali" ili kulinda heshima ya jumuyia ya kimataifa. Condoleezza Rice hakutaja "hatua gani kali" itachukuliwa. Lakini msemaji wa ikulu ya Marekani Scott McClellan amesema wazi kwamba hatua hizo ni pamoja na kuiadhibu.

Msimamo wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jack Straw unaonekana pole kidogo. Tarehe 12 Bw. Kofi Annan alisema, anatumai katibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Mohamed el Baradei atakayefanya ziara nchini Iran hivi karibuni aweze kuishawishi Iran ikubali kurejea kwenye mazungumzo ili kupata ufumbuzi. Katika siku hiyo waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jack Straw alisema anafuatilia sana "ufanisi wa Iran wa kupata uranium safi", na kwamba ufanisi huo umeharibu imani ya jumuyia ya kimataifa kwa serikali ya Iran. Na kwa mara nyingine tena alihimiza Iran isimamishe mara moja shughuli nyeti za nyuklia na kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Nchi za Ufaransa, Ujerumani na Israel pia zililaani kitendo hicho cha Iran.

Msimamo wa Russia haukuwa wazi. Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov tarehe 12 alisema, "Iran imepiga hatua kwenye mwelekeo uso wa sahihi", alionya kuwa pengine hali itakuwa mbaya zaidi. Lakini Russia inapinga kabisa kuichukulia Iran hatua za kijeshi.

China, ambayo siku zote inatetea kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia imeonesha msimamo wake kupitia mwakilishi wake Bw. Wang Guangya, ikitaka pande zote husika ziwe na uvumilivu na zisichukue hatua yoyote inayoweza kusababisha hali kuwa mbaya zaidi.

Kwa ujumla, kitendo cha Iran kupata uranium safi kimepeleka suala la nyuklia la Iran kwenye kipindi muhimu sana. Hivi sasa jumuyia ya kimataifa imefananisha na hali ya Iraq iliyokuwa katika miaka kadhaa iliyopita. Lakini Iran kweli itavamiwa na jeshi la Marekani kama Iraq? Hilo ni suala linalozingatiwa zaidi. Wachambuzi wanaona kwamba maoni tofauti ya nchi hizo yanaonesha Marekan inapofikiria kuichukulia Iran hatua ya kijeshi itakumbwa na changamoto kubwa zaidi katika jumuyia ya kimataifa kuliko iliyopata ilipoivamia Iraq miaka kadhaa iliyopita.

Kutokana na vita vya Iraq kulaumiwa sana na jumuyia ya kimataifa, Uingereza imekataa kushirikiana na Marekani na kutaka kushirikiana na nchi za Ulaya kutatua suala la silaha za nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo, hali ambayo ni tofauti kabisa na Uingereza ilivyofuata kikaidi Marekani katika vita vya Iraq na kusababisha mfarakano wa nchi za Ulaya. Pili, Iran sio tu imefanikiwa kuzivutia nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, bali pia imeshirikisha Russia na kisha inajaribu kuzivutia nchi za Asia katika utatuzi wa suala lake la nyuklia, hali hiyo imesababisha mgongano wa kuzingatia maslahi kwa kila nchi na kuleta matata kwa mkakati wa Marekani.

Ingawa Iran inakumbwa na shinikizo kubwa kutoka jumuyia ya kimataifa, Iran inaendelea kushikilia msimamo wake wa kutoacha shughuli za nyuklia. Kutokana na msimamo huo dhabiti, Iran pengine itaendelea kupambana na changamoto ya Marekani. Lakini kutokana na sababu zilizotajwa hapo juu, Marekani itakuwa makini katika hatua ya kijeshi dhidi ya Iran. Kama ripoti ya "Siasa ya nyuklia ya Iran katika mazingira ya kimataifa" iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana ilivyosema "vita vya Iraq imebadilisha muundo wa kisiasa ya kikanda tu, lakini vita vya Iran itabadilisha muundo wa kisiasa wa dunia nzima."

Idhaa ya kiswahili 2006-04-13