Wajumbe kutoka nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani wanatarajiwa kukutana tarehe 18 huko Moscow, kujadilia njia za kutatua mgogoro wa nyuklia wa Iran. Mkutano huo umechukuliwa kuwa ni jitihada nyingine kubwa ya kidiplomasia kabla ya tarehe 29 mwezi huu ambapo mkurugenzi mkuu wa Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA atawasilisha taarifa mpya ya suala la nyuklia la Iran kwa Baraza la usalama.
Mwishoni mwa mwezi Machi Baraza la usalama lilipitisha kwa kauli moja taarifa inayoitaka Iran isimamishe shughuli zake za kusafisha uranium. Sasa siku karibu 20 zimeshapita baada ya kupitishwa kwa taarifa hiyo, lakini licha ya maendeleo yoyote kushindwa kupatikana, hali ya wasiwasi imezidi kuwa mbaya. Mkutano huo wa Moscow utafanyika katika hali hiyo.
Suala la nyuklia la Iran kwa mara nyingine tena lipo njia panda ya kuelekea utatuzi wa kidiplomasia au kupamba moto kwa mapambano. Mkuu wa Idara ya nishati ya atomiki ya Russia Bw. Sergei Kiriyenko hivi majuzi alisema Iran ina uwezo wa kusafisha uranium katika maabara kwa hivi sasa, lakini bado iko mbali sana kabla ya kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Ndiyo maana suala la nyuklia la Iran bado lingeweza kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia. Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Cui Tiankai ambaye atahudhuria mkutano wa Moscow amesisitiza kuwa, utatuzi wa suala la nyuklia la Iran kwa njia za mazungumzo na za kidiplomasia bado ni chaguo mwafaka kuliko nyingine, ambayo inalingana na maslahi ya pande mbalimbali. Amezitaka pande husika zijizuie na kuepuka kuchukua hatua zinazoweza kuongeza makali ya hali ilivyo sasa.
Kwa upande wa Marekani, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo Bw. Sean McCormack amesema Marekani itatafuta uungaji mkono wa washiriki wake kwenye mkutano wa Moscow, ili kuiwekea Iran vikwazo mbalimbali vikiwemo kufunga akaunti za fedha za Iran katika nchi za nje na kuwazuia viongozi wa Iran wasitembelee nje ya nchi hiyo. Lakini vikwazo hivyo havitahusika na sekta za mafuta ya petroli na gesi kutokana na "kuepuka kuwasumbua wananchi wa Iran", kama ilivyosema Marekani. Dalili ziemonesha kuwa, nchi za Umoja wa Ulaya zinakubali hatua hizo za Marekani. Ingawa watu wengi wanaona kuwa, bado upo uwezekano wa kuleta utatuzi wa kiamani wa suala la nyuklia la Iran, lakini juhudi za kuleta utatuzi wa kiamani zinakabiliwa na changamoto kubwa.
Iran imeeleza msimamo mkali kwa kuijibu Marekani. Amrijeshi wa jeshi la Iran Bw. Yahya Rahim-Safavi amesema nchi yake iko tayari kukabiliana na hali yoyote ile, ama vikwazo ama vita. Alisema vikosi vya Marekani vinavyowekwa katika Mashariki ya Kati vyote vinasimamiwa na Iran, na Marekani itakumbwa na hasara kubwa kabisa iwapo itaishambulia Iran.
Tangu rais Mahmud Ahmadinejad wa Iran ashike hatamu za serikali katikati ya mwaka jana, Iran imechukua hatua za kujilinda na haki ya nyuklia dhidi ya shinikizo la nchi za magharibi. Iran ilirudisha shughuli za kubadilisha uranium mwezi Agosti mwaka jana, na shughuli za kusafisha uranium katika maabara mwezi Januari mwaka huu. Tarehe 11 mwezi huu ambayo ni siku mbili kabla ya mkurugenzi mkuu wa IAEA, Bw. Mohamed ElBaradei kuizuru nchi hiyo, Iran ilitangaza bila matarajio kuwa, imefanikiwa kusafisha madini ya uranium na itajiunga kwa haraka na "klabu ya kimataifa ya teknolojia za nyuklia".
Magazeti ya Ulaya yanachambua kuwa, matangazo hayo yana lengo la kuilazimisha Marekani ifanye mazungumzo ya moja kwa moja na Iran, kwa vile Iran imeweka bayana kuwa, upande unaotoa uamuzi kuhusu suala la nyuklia la Iran sio Umoja wa Ulaya wala Bw. Baradei, bali ni Marekani.
Kutokana na mpango Iran na Marekani zitakuwa na mazungumzo kuhusu usalama na utulivu nchini Iraq. Wachambuzi wanaona kuwa, mazungumzo hayo pia yatahusika na suala la nyuklia la Iran. Iran inajaribu kuambatanisha suala hilo la nyuklia na suala la Iraq, ambalo ni tatizo sugu la Marekani. Kwa kulitumia suala la Iraq, Iran itailazimisha Marekani irudi nyuma na kukubali Iran ijiendeleze katika teknolojia za nyuklia. Kwa upande wa Marekani, haina mbinu zenye ufanisi za kuidhibiti Iran, kwa vile muda wa kufanya mashambulizi ya kijeshi bado haujawadia, pia si rahisi kuzishirikisha nchi nyingine katika kuiwekea Iran vikwazo.
Idhaa ya kiswahili 2006-04-17
|