Watu 9 wameuawa na zaidi ya 40 kujeruhiwa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga lililolipuka katika mji mkuu wa Israel, Tel Aviv tarehe 17 alasiri. Hili ni shambulio la kwanza la kutoa mhanga lililofanywa na makundi ya Palestina dhidi ya Israel tangu kundi la Hamas lianze kuongoza serikali mpya ya Palestina. Wataalamu wanachambua kuwa, tukio hilo litasababisha kupamba moto kwa mapambano ya kimabavu kati ya Palestina na Israel, ambalo pia itakuwa changamoto inayokabili viongozi wapya wa Israel na Palestina.
Bomu hilo lililipuka katika mkahawa ulioko karibu na kituo cha zamani cha mabasi ya abiria mjini Tel Aviv, ambalo limeleta vifo na majeruhi wengi kuliko mashambulizi mengine dhidi ya Israel mwaka huu. Kundi la Palestina la Jihad limetangaza kuhusika na shambulio hilo. Msemaji wa kundi hilo Bw. Khaled Al Batsh alisema, "Endapo Israel inaendelea kukalia ardhi ya Palestina, na kuwaua Wapalestina, makundi mbalimbali ya Palestina yataendelea na mapambano dhidi ya askari wa Israel na wakazi Wayahudi mpaka kukomesha ukaliaji huo wa ardhi na kuanzishwa kwa nchi ya Palestina."
Kundi la Hamas linaloongoza serikali ya Palestina limesema tukio hilo ni matokeo yasiyoepukika kwa uvamizi wa Israel, na ni kitendo cha kujilinda cha watu wa Palestina.
Lakini rais Mahmoud Abbas wa mamlaka ya utawala wa Palestina amelaani shambulio hilo kwa kupitia Bw. Saeb Erekat, aliyekuwa mjumbe wa kwanza wa mazumgumzo wa Palestina. Bw. Erekat alisema, "Kwa niaba ya Bw. Abbas, nalaani shambulio hilo. Tunalaani siku zote mashambulizi yoyote dhidi ya raia wa Israel na Palestina. Shambulio la namna hii litaharibu maslahi ya Palestina. Tunataka makundi mbalimbali ya Palestina yaache vitendo vya kimabavu."
Kwa upande wa Israel, imelishutumu kundi la Hamas kwa kuwajibika na tukio hilo. Bunge jipya la Israel liliapishwa saa kadhaa baada ya mlipuko huo kutokea mjini Jerusalem, ambapo kaimu waziri mkuu Bw. Ehud Olmert akifungua bunge hilo alisema Israel inafikiria namna ya kukabiliana na shambulio hilo. Alisema, (sauti 3) "Tunafanya uchunguzi juu ya kilichotokea na nani anapaswa kubeba lawama, halafu tutaamua wakati wa kuchukua hatua."
Sambamba na Bw. Olmert kutoa kauli hiyo, jeshi la Israel lilipeleka askari wengi na magari ya kijeshi kuingia Nablus, mji ulioko kando ya magharibi ya Mto Jordan kuwasaka wanamgambo wa Palestina. Wakati huo huo jeshi la Israel linaendelea na kampeni ya ulinzi wa kijeshi katika sehemu ya Gaza, ambapo Wapalestina karibu 20 wameuawa.
Profesa Gerald Steiburg kutoka Chuo kikuu cha Bar-Ilan cha Israel alieleza kuwa, baada ya kushinda uchaguzi waziri mkuu wa Israel Bw. Olmert anakabiliana na shambulio la kwanza la bomu ambalo limesababisha vifo na majeruhi wengi, kwa hiyo Israel itachukua hatua kali za kijeshi. Alisema, "Naona Israel itachukua hatua kali zaidi za kijeshi. Serikali ya Bw. Olmert inabidi kuwaoneshea wananchi wake kuwa, ina uwezo wa kuwalinda kama alivyokuwa waziri mkuu wa zamani Bw. Ariel Sharon."
Mkuu wa Taasisi ya masuala ya kimataifa ya Palestina Bw. Mahdi Abdel Hadi pia alieleza kuwa, tukio hilo linaweza kumpeleka Bw. Olmert awe na msimamo mkali, hata jeshi la Israel litaweza kuwaua kisiri maofisa wa kundi la Hamas. Alisema, "Bw. Olmert sasa yupo katika njia panda, ama kuunda serikali ya muungano na vyama vya mrengo wa kulia vyenye msimamo mkali, ama kushirikiana na vyama vya mrengo wa kushoto. Lakini shambulio hilo linaweza kumfanya Bw. Olmert achague vyama vya mrengo wa kulia."
Profesa Hadi alisema shambulio hilo pia ni mtihani unaopima uwezo wa utawala wa kundi la Hamas. Katika miaka mingi iliyopita Hamas inafuata makubaliano ya usimamishaji vita, lakini mlipuko huo unaonesha kuwa Hamas inashindwa kuyadhibiti makundi mengine ya Palestina. Hivi sasa kundi la Hamas linakabiliwa na shinikizo kutoka nje na ndani ya Palestina, ambapo misaada ya kifedha kutoka nje imesimamishwa na Wapalestina wengi wanalitaka liafikiane na Israel kuhusu kusimamisha vita na kutatua migongano kwa amani.
Idhaa ya Kiswahili 2006-04-18
|